Jumapili Mei 28, 2017.
Leo ni Jumapili tarehe Pili Ramadhan 1438 Hijria, mwafaka na tarehe 28 Mei 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1098 iliyopita, alifariki dunia mjini Damascus, Syria Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi, fasihi, mtaalamu wa lugha na mtaalamu wa sheria za Kiislamu wa karne ya nne ya Hijiria. Nahawandi alizaliwa kusini magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Baghdad, Iraq na kupata kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha kwa wasomi wakubwa wa zama zake kama vile Ibn Durayd. Baada ya muda Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi alitokea kuwa mwalimu katika uga huo. Mwaka 311 Hijiria alielekea Sham ambapo aliishi huko hadi mwisho wa uhai wake. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha ‘Aamal Zajaji’ ‘Iidhaahul-Kaafi’ na ‘Iidhahu fi ilalin-Nahw.’
Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa mjini Paris mwaka 1801 Miladia na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo kupendelea sana kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, kulimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Kadhalika Eugène Burnouf alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Moja ya kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa athari za Eugène Burnouf.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanza shughuli zake za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia. Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo hapo mwaka 1993.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi. Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa. Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.
Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya nyuklia. Majaribio hayo yalifanyika wiki mbili baada ya India, jirani yake hasimu, kufanya majaribio ya nyuklia. Kwa msingi huo mashindano ya majaribio ya mabomu ya nyuklia yakaibuka kati ya maadui hao wawili wa muda mrefu. Majaribio ya nyuklia ya Pakistan yaliibua hasira ya nchi za Magharibi ambazo ziliamua kuiwekea vikwazo vya kiuchumi. Pamoja na hayo, lakini hadi sasa Pakistan haijakubali mashinikizo ya nchi hizo ya kuitaka itie saini mkataba wa kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia NPT.