Jul 09, 2017 17:16 UTC
  • Jumapili Julai 9, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 14 Shawwal 1438 Hijria, sawa na Julai 9, 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 865 iliyopita, alifariki dunia Ghotbeddin Ravandi, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, elimu ya hadithi, theolojia na mfasiri mkubwa wa Qur'ani Tukufu wa Kiislamu katika karne ya sita Hijiria. Tokea akiwa kijana mdogo, Ghotbeddin Ravandi alipata kujifunza elimu mbalimbali kama vile fiqhi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake. Akiwa na umri wa karibu miaka 80 Ravandi tayari alikuwa ameandika vitabu vingi vikiwemo, 'Tafsiri ya Qur'ani' 'Risaalatul-Fuqahaa' 'Ayatul-Ahkaam' na 'Asbaabun-Nuzuul.'

Ghotbeddin Ravandi,

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, nchi ya Argentina ilijipatia uhuru wake. Kufikia mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, Argentina ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia jeshi la Uhispania lilianza kudhoofika kutokana na kupambana mara kwa mara na jeshi la Uingereza. Kutokana na kwamba Waingereza nao pia walikuwa wakiikodolea macho ya tamaa ardhi ya Argentina, waliudhibiti mji wa Buenos Aires, ambao ni mji mkuu wa taifa hilo. Hata hivyo raia wa Argentina walipambana vikali dhidi ya jeshi vamizi la Mwingereza na kufanikiwa kulifurusha ambapo walipata uhuru wao katika siku kama ya leo. Argentina ina ukubwa wa kilomita mraba 2780000 katika bahari ya Atlantic huko Amerika ya Latini, huku ikipakana na nchi za Chile, Bolivia, Paraguay na Uruguay.

Argentina

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, yaani sawa na tarehe Tisa Julai mwaka 1856 Miladia, alizaliwa Nikola Teslam mwanafizikia maarufu wa Yugoslavia. Katika kipindi cha masomo yake, Nikolas alipendelea sana masomo ya fizikia na kutokana na ufahamu wake wa hali ya juu, akapewa lakabu ya 'Mwenye Kipawa'. Baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya umeme alianza kufanya utafiti mwingi katika fani hiyo, na kufikia hatua kubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafizikia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux). Nikola Teslam alifariki dunia tarehe 10 Mei 1943 Miladia akiwa na umri wa miaka 87.

Nikola Teslam

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena. Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.

Bendera ya utawala haramu wa Israel

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita mapinduzi ya Nojeh yaliyokuwa yakisimamiwa na Marekani nchini Iran yaligunduliwa na kuzimwa. Njama hiyo ya mapinduzi iliratibiwa na Shirika la ujasusi la Marekani (CIA likishirikiana na baadhi ya vibaraka wa jeshi la anga la utawala wa Shah kwa shabaha ya kumuua Imam Khomeini, kuangamiza utawala wa Kiislamu hapa nchini na kumrejesha madarakani Shapur Bakhitiyar. Waratibu wa njama hiyo ya mapinduzi walikusudia kufanya mashambulizi dhidi ya makazi ya Imam Khomeini mjini Tehran na kumuua na kisha kushambulia kituo cha kuongozea ndege cha uwanja wa Mehrabad. Hata hivyo njama hiyo iligunduliwa na kusambaratishwa na waratibu wa njama hiyo kutiwa mbaroni na kuhukumiwa.

Kambi ya jeshi la anga ya Shahid Nojeh Hamadan

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika.

Umoja wa Afrika (AU)

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.

Sudan Kusini