Aug 07, 2017 06:32 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Agosi 7

Ufuatao ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Iran yazoa medali 6 katika Olimpiki ya Walemavu

Wanariadha bingwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa jumla ya medali 6 katika Mashindano ya Kimataifa ya Olimpiki ya Walemavu mwaka huu 2017 nchini Uswisi. Ali Sepahvandi aliipa Iran medali ya shaba katika mchezo wa kurusha kisahani, baada ya kukirisha umbali wa mita 32.9, huku Mohammadtaha Beygrezaei akishinda medali ya fedha katika mchezo wa kurusha mkuki. Mchezaji huyo alirusha umbali wa mita 25.3 katika kategoria ya F32/34. Mwanariadha nyota wa Iran, Mehrdad Moradi aliipa Iran medali ya dhahabu katika mbio za mita 100 kategoria ya T11/T13, kwa kutumia sekunde 11.33. Dhahabu nyingine ya Iran ilitwaliwa na Mohammadhassan Mirzaei Seghinsara katika mchezo wa kurusha kisahani, kwa kutupa umbali wa mita 25.9, kitengo cha F51/F57. Awali Wairani Aref Baharvand na Ashkan Cheraghi waliipa nchi yao medali za fedha na shaba, katika michezo ya kurusha kitufe, kategoria ya F36 na F35 kwa usanjari huo.

Iran yaibuka ya 4 Olimpiki ya Majeshi

Kikosi cha anga cha al-Mahdi cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeibuka ya nne katika Mashindano ya Olimpiki ya Majeshi ya Dunia yanayofanyika katika nchi mbalimbali duniani. Brigedi ya Anga ya Kikosi Maalumu cha Iran imeibuka ya nne katika mashindano hayo ya kimataifa yanayojumuisha michezo mbalimbali. Mashindano hayo ya dunia yamefanyika katika nchi za Russia, China, Azerbaijan, Belarus na Kazakhstan, na kuvileta pamoja vikosi mbalimbali vya majeshi ya China, Russia, Angola, Iran, Zimbabwe, Venezuela, Belarus, Uzbekistan, Misri. Mashindano hayo yamejumuisha ulengaji shabaha kwa aina tofauti za bunduki, utumiaji wa silaha za kisasa za kivita pamoja na vifaru na kadhalika. Kadhalika wanajeshi walioshiriki mashindano hayo walijitosa katika mbio mbali mbali. Mashindano hayo yanatazamiwa kufunga pazia lake Agosti 12.

Riadha: Mbio za London Marathon 2017

Mwanariadha nyota wa Kenya, Paul Tanui aliishindia nchi yake medali ya kwanza katika Mashindano ya Dunia ya London Marathon mwaka 2017 Ijumaa usiku. Mwingereza Mo Farah alidhihirisha kuwa yeye ni moto wa kuotea mbali kwa kunyakua taji lake la tatu mfululizo kwa kutumia dakika 26:49.51 katika uwanja wa Olympic jijini London. Mzawa huyu wa Somalia, ambaye hajawahi kushindwa katika mbio za mita 5,000 na mita 10, 000 katika Riadha za Dunia, Olimpiki na Bara Ulaya tangu mwaka 2012, alifuatwa kwa sekunde 0.43 na Mganda Joshua Cheptegei kabla ya Tanui kufunga tatu-bora kwa dakika 26:50.60.

Katika siku ya pili ya mashindano ya dunia ya riadha na wakenya watatu walifuzu kwa nusu fainali ya mbio za mita 800 upande wa wanaume. Katika mchujo wa kwanza wa mbio hizo, aliyekuwa bingwa wa dunia katika mashindano ya riadha kwa wakimbiaji walio chini ya umri wa miaka 20 Kipyegon Bett alifuzu kwa nusu fainali baada ya kumaliza wa kwanza. Habari njema kutoka London kwa Kenya ni kuwa, Mkenya Geoffrey Kirui ameshinda medali ya dhahabu kwenye mbio za nyika za masafa marefu kwa kutumia masaa 2, dakika 8 na sekunde 27 akifuatwa na Muethiopia na kisha Alphonce Simbu wa Tanzania ambaye aliwashangaza wengi akiibuka wa tatu na kutwaa fedha.

Katika siku ya tatu ya mashindano hayo ya riadha ya dunia jijini London nchini Uingereza, Mkenya Jirus Birech alimaliza katika nafasi ya tano na kufuzu kwa fainali kwa kutumia muda wa dakika 8 sekunde 23 nukta 84.

Raga: Uganda, si haba

Timu ya taifa ya raga ya Uganda imemaliza Raga ya Afrika (Africa Gold Cup) katika nafasi ya tatu baada ya kunyamazisha Zimbabwe kwa alama 38-12 jijini Kampala katika mechi yake ya mwisho Jumamosi. Namibia ilitawazwa mabingwa kwa kulaza Kenya 45-7 jijini Windhoek mnamo Julai 29. Mabingwa mara saba Namibia walimaliza makala ya mwaka huu wa 2017 kwa pointi 25 nao mabingwa wa mwaka 2011 na 2013 Kenya wakafunga mashindano katika nafasi ya pili kwa pointi 16. Uganda pia imemaliza mashindano haya ya mataifa sita kwa pointi 16. Timu itakayotemwa haitashiriki Gold Cup mwaka ujao 2018. Mashindano ya Gold Cup mwaka 2018 yatatumika kuchagua mwakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia mwaka 2019.

 

Gunners watwaa tena Kombe la Ngao ya Jamii

 

Klabu ya Uingereza ya Arsenal yenye makao yake jijini London imeweza kuzikonga nyoyo za mashabiki na wadau wa timu hiyo, baada ya kufanya kazi ya ziada na kuunyakua ubingwa wa Ngao ya Jamii. Ushindi huu kwa kiasi Fulani unafuta madhambi ya timu hiyo iliyoyafanya katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Gunners wametwaa Kombe la Ngao ya Jamii baada ya kuisasambua Chelsea katika mikwaju ya penalti na kuifunga mabao 4-1, katika mchezo wa aina yake uliopigwa katika uwanja wa Wembley. Arsenal imepata ushindi huo baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea ambao walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika kunako 46 likifungwa na Victor Moses. Hata hivyo vijana wa Arsene Wenger walijipapatua na kusawazisha mambo kupitia kwa kiungo Sead Kolasinac dakika ya 82. Mabao ya Oxlade-Chamberlain na Giroud katika mikwaju ya penati yalitosha kuwapaisha Wabeba Bunduki hao wa London.

Gunners wameshinda taji hilo kwa mara ya tatu sasa katika kipindi cha miaka minne, huku The Blues wakiambulia patupu katika kipindi hicho. Kwa ujumla Arsenali imetwaa Kombe la Community Shield mara 14 sasa, ya pili baada ya Man U ambao wameshindwa mara 18.

Neymar anunuliwa kwa thamani ya ndege ngapi?

Tunafunga kipindi kwa kutupia jicho kile ambacho kimejadiliwa na kuteka fikra za mashabiki wengi ndani ya siku chache zilizopita. Naam…nazungumzia mauzo yaliyovunja rekodi katika historia ya soka. Klabu ya Ufaransa ya Paris Saint Germain ililipa Yuro Milioni 222 kwa kumnunua mshambuliaji nyota wa Barcelona Neymar Jnr raia wa Brazil. Ununuzi huo wa mchezaji huyo wa miaka 25 umevunja rekodi ya awali iliyowekwa na Paul Pogba aliporejea Manchester United kutoka Juventus. Paul Pogba alinunuliwa kwa kima cha Yuro milioni 105. Neymar atakuwa analipwa Yuro milioni 45 kwa mwaka, mbali na marupurupu ya Yuro 865,000 kila wiki katika mkataba wake wa miaka mitano ya kwanza. Neymar amesema amejiunga na mojawapo ya klabu zenye ndoto kuu zaidi barani Ulaya. Neymar ambaye alijiunga na Barca mwaka 2013 alikuwa na haya ya kusema baada ya kupokewa na wasimamizi na mashabiki wa PSG mjini paris.

………………………TAMATI…………………..