Sep 09, 2017 02:34 UTC
  • Jumamosi, Septemba 9, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Tatu Dhulhaji 1438 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 9 Septemba 2017 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita, kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran. Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu.

Baada ya kujiuzulu mfalme Justinian mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma. Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45. ***

Vita vya miaka saba baina ya tawala mbili za Iran na Roma zilizokuwa na nguvu 

Miaka 1428 iliyopita katika siku kama ya leo, Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu mpende atakayempenda, na mfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlu-Baiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama. ***

Tukio la Ghadir

Katika siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Imam Ali bin Abi Twalib as alikubali kuchukua jukumu la Ukhalifa na uongozi wa Waislamu baada ya Waislamu kumsisitizia mno akubali kuchukua jukumu hilo. Baada ya Khalifa wa Tatu Othman bin Affan kuuawa watu walimiminika kwa wingi katika nyumba ya Imam Ali kwa ajili ya kumpa baia na kiapo cha utii. Awali Imam Ali as alikataa kuchukua jukumu la uongozi wa Waislamu, jukumu ambalo alikuwa amepatiwa na Allah na Mtume wake kabla ya kufariki dunia na kurejea kwa Mola wake Mtume Muhammad saw.  Hata hivyo baada ya watu kumsisitizia mno na watu kukubali masharti yake, Imam Ali as alikubali kuchukua hatamu za uongozi wa Waislamu. Katika kipindi kifupi cha miaka minne na miezi 9 ya uongozi wake, Imam Ali as alifanya marekebisho kadhaa muhimu kubwa zaidi likiwa ni kutekeleza uadilifu wa kijamii. Hata hivyo maadui wa Uislamu walishindwa kuvumilia uadilifu huo na hivyo kupelekea kutokea vita vitatu baina ya Waislamu na hatimaye akauawa shahidi katika njia hiyo. ***

Ukhalifa wa Imam Ali bin Abi Twalib as

Siku kama ya leo miaka 766 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hisabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat. ***

Khwaja Nasiruddin Tusi

Miaka 189 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia. Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hicho ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokipa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.***

Leo Tolstoy

Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, kulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati. ***

Mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita yaani tarehe 18 Shahrivar 1348 Hijria Shamsia, alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsia jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika katika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupi fupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupi fupi. ***

Jalal Aal Ahmad

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, aliaga dunia Mao Tse Tung (Mao Zedong) kiongozi wa Uchina. Tse Tung alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake. Mao alikuwa akisisitiza juu ya kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo alipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina. ***

Mao Tse Tung

Na siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, nchi ya Tajikistan ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Umoja wa Kisovieti.  Katika karne ya 6b Miladia, Tajikistan ilikuwa sehemu ya utawala wa Hakhamaneshian wa Iran na katika karne ya 9 Miladia ikakombolewa na Waislamu. Kijiografia Tajikistan ipo katikati mwa Asia ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 143,000 na inapakana na nchi za China, Uzbekistan, Afghanistan na Kyrgyzstan na mji mkuu wake ni Dushanbe. Sarafu ya nchi hiyo ni Somoni huku lugha ya taifa ikiwa ni Kitajiki.

Bendera ya Tajikistan

 

 

Tags