Ijumaa, Septemba 22, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Muharram 1439 Hijria sawa na Septemba 22, 2017.
Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Hesabu ya mwaka wa Hijria ilianzishwa katika zama za utawala wa khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminiin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita yaani tarehe Mosi Muharram mwaka wa 7 tangu Mtume (saw) abaathiwe na kupewa utume kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu, Makuraishi walifunga mkataba wa kuweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake. Viongozi wa makafiri wa Makka ambao walikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kasi ya kustawi Uislamu na vilevile kutokana na kufeli njama zao za kuzuia kuenea dini hiyo, waliamua kuweka mzingiro wa kiuchumi ili kufanikisha malengo yao. Kwa msingi huo waliamua kuweka mkataba dhidi ya Waislamu. Mkataba huo uliwakataza watu wote kufanya muamala wa aina yoyote na wafuasi wa dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake walizingirwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika bonde lililojulikana kwa jina la Shiibi Abi Twalib wakisumbuliwa na matatizo mengi na mashinikizo ya kiuchumi na katika kipindi hicho Mtume (saw) alipoteza wasaidizi wake wawili muhimu yaani ami yake, Abu Twalib na mkewe kipenzi, Bibi Khadija. Waislamu hao walisimama imara kulinda imani yao na hawakutetereka hata kidogo licha ya matatizo makubwa waliyokabiliana nayo. Mzingiro huo wa kiuchumi dhidi ya Waislamu ulikomeshwa mwezi Rajab mwaka wa kumi baada ya kubaathiwa Mtume.
Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita Shaka kaSenzangakhona kiongozi wa kikabila na mwasisi wa ufalme wa Zulu huko Afrika Kusini ya sasa aliuawa na kaka zake wawili wa kambo. Shaka aliliongoza kabila kubwa la Zulu tangu mwaka 1815 na katika kipindi kifupi aliweza kuyaweka chini ya uongozi wake maeneo mengi ya Afrika Kusini. Baada ya kuuawa Shaka, kaka yake mmoja alichukua hatamu za uongozi na kuanzia mwaka 1830 hadi 1839 alipigana na wahamiaji wa Kiholanzi waliojulikana kama Boers. Hatimaye serikali ya Shaka ilipata pigo kutoka kwa Uingereza mwaka 1880 na kugawanyika katika serikali kadhaa zisizo na mamlaka kamili. Wazulu hii leo wanahesabiwa kuwa jamii yenye nguvu huko Afrika Kusini.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.
Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein yalianza mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.