Jumapili 19 Novemba, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 30 Swafar Mfunguo Tano 1439 Hijria, sawa na Novemba 19, 2017 Miladia.
Siku ya mwisho ya mwezi Swafar miaka 1438 iliyopita kulitokea tukio la Lailatul Mabiit na kuanza kwa hijra ya Mtume kutoka Makka kwenda Madina. Suala la hijra na kutoka Makka kuhamia Madina liliainishwa katika Baia ya Pili ya Aqaba. Makafiri wa Kikuraishi wa Makka walipopata habari hiyo walichukua uamuzi wa kutaka kumuua Mtume Muhammad (saw) na kwa sababu hiyo waliafiki pendekezo lililotolewa na Abu Jahl juu ya namna ya kutekeleza njama hiyo chafu. Kwa mujibu wa pendekezo hilo, kila ukoo kati ya koo zote za kabila la Kuraish ulitakiwa kumchagua kijana mmoja na wote kwa pamoja wavamie nyumba ya Mtume (saw) wakati wa usiku na kumuua akiwa amelala. Hata hivyo Mwenyezi Mungu SW alimjulisha Mtume wake kuhusu njama hiyo ya Makuraish na kumuamuru ahamie Madina usiku huo. Ili kuwapotosha makafiri wa Makka, Mtume (saw) alimtaka Imam Ali bin Abi Twalib (as) alale kitandani kwake. Usiku huo unajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Lailatul Mabiit kwa maana ya usiku ambao Ali bin Abi Twalib (as) alikubali kuhatarisha maisha yake na kulala kwenye kitanda cha Mtume Muhammad (saw) huku akijua kwamba Makuraishi watavamia nyumba hiyo na kumkata kwa mapanga mtukufu huyo.
Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1236 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na kuchukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao yake yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo. Imam AS anasema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe."
Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, alifariki dunia Franz Schubert mtunzi wa nyimbo maarufu wa nchini Austria. Schubert alizaliwa mwaka 1797 katika familia masikini. Tangu akiwa kijana mdogo alipendelea sana nyimbo huku akiwa na kipawa kikubwa katika uwanja huo na hivyo kuamua kusomea fani hiyo. Alianza kubuni nyimbo akiwa kijana na katika umri wake wote aliimba zaidi ya nyimbo 600. Hata hivyo licha ya kuimba nyimbo nyingi hususan mziki wa asili, bado hakuweza kujinasua kutoka kwenye umasikini. Hii ni kwa kuwa nyimbo zake hazikupokelewa kwa wingi na jamii ya wakati wake. Ni baada ya kufariki dunia ndipo nyimbo zake zikapewa umuhimu mkubwa katika jamii.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, alizaliwa huko Allah Abadi nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Anwar Sadat, rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari huko Baitul Muqaddas, Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel na kutiwa saini mkataba uliojulikana kama wa amani baina ya Tel Aviv na Cairo. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Saadat.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, viongozi wa jumuiya za kijeshi za nchi za Magharibi na Mashariki (NATO) na Warsaw walitiliana saini maafikiano ya usalama mjini Paris, Ufaransa. Mkataba huo ulihitimisha vita baridi baina ya kambi mbili hizo za Magharibi na Mashariki. Viongozi wa kambi hizo pia walikubaliana kumaliza vita vya propaganda kati yao na kupunguza silaha za jumuiya mbili hizo za kijeshi.