Dec 11, 2017 08:03 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Dec

Huu ni mkusanyiko wa matukio kadhaa ya spoti yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kutoka Iran, Afrika Mashariki na kwengineko......

Wanyanyua vyuma vizito wa Iran watwaa taji la kimataifa

Maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameendelea kutoa mkono wa tahania kwa mabarobaro wa nchi hii waliobuka kidedea katika mashindano ya kimataifa ya kunyanyua uzani mzito huko Marekani. Wanyanyua vitu vizito wa Iran waliibuka washindi kwa kuzoa jumla ya alama 509, na medali 5 za dhahabu, 3 za fedha na 6 za shaba. Wanamichezo wa Iran waliozoa medali za dhahabu ni Sohrab Moradi, dhahabu 3 na Ali Hashemi dhahabu 2. Mashindano hayo yanayofahamika kama World Weightlifting Championships kwa Kimobo yalifanyika kati ya Novemba 28 na Disemba 5 katika mji wa Anaheim huko Los Angeles nchini Marekani.

Katika ujumbe wa pongezi kwa wanamichezo hao wa Kiirani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amesema: "Ningependa kuipongeza timu ya taifa ya kunyanyua uzani mzito kwa kutwaa taji la kimataifa na kutuma miale ya furaha kwa Wairani wote. Kadhalika namshukuru na kumpongeza shujaa wetu, Alireza Karimi, ambaye alidumisha hadhi ya taifa hili." Naye Rais Hassan Rouhani amewapongeza wanamichezo hao, makocha na wasimamizi kwa ushindi huo alioutaja kuwa wa kifakhari na heshima, na wa kwanza kabisa katika historia ya mashindano hayo. Wengine waliotuma salamu za pongezi kwa ushindi huo ni Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran na Massoud Soltanifar, Waziri wa Vijana na Michezo wa Iran. Huku hayo yakiarifiwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na mwanamieleka bingwa wa Iran, Alireza Karimi, ambaye alikataa kushiriki mpambano wa fainali na Mzayuni katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Mieleka Wenye Miaka Isiyozidi 23 nchini Poland. Ayatullah Ali Khamenei alimpokea shujaa huyo pamoja na familia yake siku ya Jumapili Disemba 10 na kumpa bishara ya kupokea tuzo ya kiroho kutoka kwa Allah.

Kiongozi Muadhamu akimbumbatia mwanamieleka Alireza

Ifahamike kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiutambui utawala wa Kizayuni wa Israel, na wanamichezo wake wamekuwa wakisusia kukutana ana kwa ana na wachezaji wa Kizayuni. Karimi ambaye Novemba 26 alimchachafya raia wa Russia Alikhan Zhabrailov katika mpambano wa nusu fainali, alitazamiwa kuvaana na Mzayuni katika pambano la mwisho lakini akasusia mchezo huo, licha ya kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa amgaragaze na kutwaa ubingwa.  

Cecafa: Zenj yawashangaza wengi

Mchezo mzuri ulioonyeshwa na timu ya soka ya Zanzibar katika michuano yake yote iliyocheza kwenye mashindano ya Chalenji umelitia wasi wasi Shirika la Kukabiliana na Utumiaji wa Pufya WADA na Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), na kuibua hofu kwamba yumkini wachezaji hao wanatumia dawa za kuwaongeza nishati. Wachezaji hao ni Kiungo Mohamed Issa 'MO Banka', Fesal Salum 'Fei Toto' na Washambuliaji Ibrahim Hamad Hilika na Suleiman Kassim 'Seleembe'. Kama ilivyokuwa kawaida ya kupimwa kwa wachezaji hasa katika mashindano ya kimataifa mara hii wachezaji hao wa Zanzibar wamelazimika kupimwa ili kujua kama kuna chembechembe zozote za dawa hizo. Aidha WADA na CECAFA wameingiwa na wasi wasi kutokana na kiwango bora walichoonyesha Zanzibar katika Mashindano hayo huku ikiwaongoza mataifa kama Libya, Rwanda, wenyeji Kenya na kaka zao Tanzania Bara.

Nembo ya hirika la Kukabiliana na Utumiaji wa Pufya WADA

WADA na CECAFA walisema wana mashaka na wachezaji wa Zanzibar na jinsi walivyokuwa wanacheza na kuonesha dhamira yao baadae wakawataja wachezaji hao wanne akiwemo kiungo kinda Feisal Salum “Fei Toto” ambaye amechaguliwa kuwa nyota wa mchezo dhidi ya wenyeji Kenya ulomalizika 0-0. Ikumbukwe kuwa Tangu kuanza Mashindano haya Zanzibar inaongoza kutoa wachezaji bora wa mchezo yani Man of the Match ambapo mchezo wa awali mchezaji bora akitajwa kuwa Mohd Issa “Banka”, mchezo wa pili mchezaji bora wa mchezo akawa Ibrahim Hamad “Hilika”. Zanzibar Heroes imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hii ya Chalenji.  Wachezaji hao wa Zanzibar Heroes na mkufunzi wao wamekanusha vikali tuhuma hizo, wakisema kuwa wao ni safi,na wanachezo wa kujituma.

Licha ya madai hayo, aliyewahi kuwa mkufunzi wa timu ya timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ John Simkoko amesema Zanzibar Heroes wametoa funzo kwa timu za kanda hiyo na si ajabu kutwaa Kombe la Chalenji. Anasema: "Kama ukiwafuatilia kwa umakini hawa Zanzibar, si mara moja kufanya vitu kama hivi, nakumbuka wakati michuano hii inafanyika kule Ethiopia mwaka 2015 walitusumbua sana, hata wakati nafundisha Mtibwa nilishawahi kukutana na timu ya Zanzibar ambayo ni Mlandege kwenye michuano ya Kagame Cup, walinisumbua sana." Uganda Granes pia imetinga nusu fainali bada ya kusasambua Ethioia katika mchuano wake wa robo fainali Jumapili. Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi toka Disemba 3 katika viwanja vya Machakos na Kakamega na inatarajiwa kufikia tamati Disemba 17 mwaka huu.

Ronaldo atwaa tena Balon D'Or

Mchezaji soka mahiri wa klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo amejipiga kifua na kusema kushinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mara ya tano inathibitisha kuwa yeye ndiye mchezaji bora katika historia ya hivi karibuni.

Ronaldo akitoa hotuba fupi baada ya kupokea Tuzo ya Ballon d'Or

Usiku wa kuamkia Ijumaa, raia wa Ureno alitangazwa mchezaji bora wa dunia kwa mara ya tano na sasa anapepea katika anga moja na Lionel Messi wa Barcelona ambaye pia ametwaa tuzo ya Ballon d'Or mara tano. Ronaldo ambaye hivi karibuni alitangazwa kuwa mchezaji bora wa 2017 wa tuzo za Shirikisho la Soka Duniani FIFA, ana umri wa miaka 32 tu.

..............................TAMATI..........................