Jumanne, Disemba 19, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 30 Mfungo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na Disemba 19, 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na 19 Disemba 1972, kiongozi wa wakati huo wa Uganda Jenerali Idi Amin Dada aliwapatia wafanyakazi wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi nchini humo makataa ya siku 12 wakubali kupunguziwa mishahara yao kwa asilimia 40 au waondoke nchini humo. Zoezi hilo liliwajumuisha karibu wafanyakazi 780 wa Kiingereza waliokuwa wakifanya kazi kwenye mashirika mbalimbali nchini Uganda.
Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, Sadeq Ganji mwambata wa Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Lahore Pakistan alishambuliwa kwa risasi na vibaraka wa ubeberu wa kimataifa na kuuawa shahidi. Kwa karibu miaka minne Ganji alikuwa akitekeleza jukumu lake la kutangaza na kuziarifisha thamani aali za Kiislamu na kupanua uhusiano wa kiutamaduni baina ya wananchi wa Iran na Pakistan. Sadeq Ganjia aliuawa shahidi akiwa amekaribia kurejea hapa nchini baada ya hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na wana utamaduni na shakhsia wa kielimu na kifasihi wa Lahore Pakistan.
Na katika siku kama ya leo miaka 230 iliyopita, mwafaka na tarehe 19 Disemba 1787, nchi ya Kiafrika ya Sierra Leone iliunganishwa na Uingereza, baada ya kupita miaka 327 tangu ardhi ya nchi hiyo igunduliwe na wazungu. Sierra Leone iligunduliwa na mtalii wa Uhispania na kukoloniwa. Katika miaka ya kukoloniwa kwake na Uhispania, maelfu ya wanaume na wanawake wa Sierra Leone walichukuliwa watumwa na kwenda kuuzwa katika masoko ya Ulaya. Mwenendo huo uliendelea pia baada ya Waingereza kuishinda Uhispania na kuanza ukoloni wa Uingereza nchini humo. Mwaka 1961 Sierra Leone ilianza kujitawala na kuwa na utawala unaosimamiwa na jeshi na mwaka 1971 ikawa na utawala wa Jamhuri.