Ulimwengu wa Spoti, Disemba 25
Hujambo mpenzi mwanaspoti wa RT na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho matukio yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita katika nyuga za spoti, kitaifa na kimataifa. Usibanduke kando ya radio yako hadi tamati ya kipindi……karibu….
Mwanamieleka wa Iran atawazwa bingwa wa dunia
Mwanamieleka nyota wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hassan Yazdani Cheratki ametangazwa kuwa mwanamieleka bora zaidi wa mtindo wa frestyle mwaka huu 2017. Cheratki pamoja na Yasemin Adar wa Uturuki na Helen Marioulis wa Marekani ndiyo wanaoongoza orodha hiyo ya Jumuiya ya Mieleka Duniani UWW. Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya United World Wrestling, mwanamieleka huyo wa Kiirani ameonyesha mchezo wa kuridhisha katika mapambano yake 16 mwaka huu.
Muirani mwingine asusia kupambana na Mzayuni
Mwanamasumbwi bingwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Ijumaa alisusia kushiriki mpambano dhidi ya hasimu wake kutoka Israel, katika Mashindano ya Ndondi ya Vijana ya Kombe la Agalarov. Mobin Abbasi alikataa kuvaana na Muisraeili huyo kwenye pambano la wanamasumbwi wenye kilo 52 huko Azerbaijan.
Mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kwa Kimbombo kama Agalarov Cup Youth Boxing Tournament yalianza Disemba 20 na kufunga pazia lake Disemba 25 katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku. Hivi karibuni, mwanamieleka bingwa wa Iran, Alireza Karimi, alikataa kushiriki mpambano wa fainali na Mzayuni katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Mieleka Wenye Miaka Isiyozidi 23 nchini Poland. Karimi ambaye Novemba 26 alimchachafya raia wa Russia Alikhan Zhabrailov katika mpambano wa nusu fainali, alitazamiwa kuvaana na Mzayuni katika pambano la mwisho lakini akasusia mchezo huo, licha ya kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa amgaragaze na kutwaa ubingwa. Ifahamike kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiutambui utawala wa Kizayuni wa Israel, na wanamichezo wake wamekuwa wakisusia kukutana ana kwa ana na wachezaji wa Kizayuni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikutana na mwanamieleka bingwa wa Iran, kwa suhujaa wake na kudumisha haidhi ya taifa hili kwa kususia kugaragazana na Mzayuni.
Dakta Shein awapokea Zanzibar Heroes na kuwatuza
Wachezaji wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanziba Heroes’ wamemshukuru Rais wa serikali ya mapinduzi Zanzibar Dokta Ali Mohamed Shein kwa kuipatia timu hiyo pamoja na viongozi wake zawadi ya shilingi million tatu kila mmoja pamoja na viwanja 33 vya kujengea nyumba.
Wachezaji hao wamesema jambo ambalo limefanywa na Rais Shein limewajengea motisha ya kujituma tena pale mashindano hayo yatakapofanyika kwani wameona ni wazi sasa serikali imewakumbuka. Wachezaji hao wanasema watajituma zaidi ili waweze kurudisha fadhila kwa Rais Shein ambaye ameonesha kuwaunga mkono kutokana na juhudi zao.
Zawadi hizo zilitolewa usiku wa Jumapili Disemba 24 katika halfa iliyofanyika kwenye ukumbi wa baraza la zamani la Wawakilishi mjini Unguja, ambapo Rais Shein aliandaa dhifa ya chakula cha jioni kwa ajili ya kuwapongeza vijana wa Zanzibar Heroes kwa kushika nafasi ya pili kwenye michuano ya CECAFA. Hata hivyo mkufunzi wa Zanzibar Heroes Hemed Suleiman 'Morocco' alikuwa na kilio kimoja tu.
Tuzo za CAF
Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, limetangaza orodha ya wachezaji watatu wa kike na kiume wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa mwaka wa 2017. Mshindi atatangazwa tarehe 4 mwezi Januari mwaka 2018, jijini Accra nchini Ghana.
Mchezaji bora kwa upande wa wanaume
- Mohamed Salah (Misri & Liverpool)
- Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Dortmund)
- Sadio Mane (Senegal & Liverpool)
Mchezaji bora kwa upande wa wanawake
- Asisat Oshoala (Nigeria & Dalian Quanjian)
- Chrestina Kgatlana (Afrika Kusini & UWC Ladies)
- Gabrielle Aboudi Onguene(Cameroon & CSKA Moscow)
Klabu ya bora ya mwaka
- Al Ahly
- TP Mazembe
- Wydad Athletic Club
Timu bora ya taifa
- Cameroon
- Egypt
- Nigeria
Timu bora ya taifa kwa upande wa wasichana chipukizi
- Ghana -Chini ya miaka 20
- Nigeria -Chini ya miaka 20
- Afrika Kusini
Tuzo hii imekuwa ikitolewa tangu mwaka 1992.
Riadha: Mkenya atwaa taji la Sanyo Half Marathon
Mwanariadha wa Kenya anayeishi nchini Japan Pauline Kamulu ameibuka mshindi wa mbio za kilomita 21 za Sanyo Half Marathon siku ya Jumamosi. Mkenya huyo alishinda duru ya ya 36 ya mashindano hayo kwa kutumia saa 1, dakika 8 na sekunde 4, huu ukiwa ni muda ni rekodi mpya ya Sanyo Half Marathon. Alifuta rekodi ya saa 1, dakika 8 na sekunde 17 ambayo Mkenya mwenzake Sally Chepyego aliweka aliposhinda taji la mwaka 2015, alipomlemea Rei Ohara ambaye alikuwa anatetea taji hilo. Miyuki Uehara na Mao Ichiyama waliridhika na nafasi za pili na tatu kwa kutumia saa 1, dakika 9 na sekunde 13 na saa 1, dakika 9 na sekunde 14, kwa usanjari huo.
El-Clasico: Madrid yasasambuliwa na Barca
Mchuano wa kukatana shoka wa el-Clasico uliopigwa Jumamosi katika uwanja wa Santiago Bernabeu ungali gumzo miongoni mwa mashabiki na wafuatiliaji wa soka duniani. Katika kitimutimu hicho cha Disemba 23, Barcelona ilipata ushindi mkubwa wa mabao 3-0 iliposhuka dimbani kuvaana na Real Madrid ugenini, katika mechi muhimu ya kuwania Ligi Kuu ya Soka nchini Uhispania ukipenda La Liga. Vijana wa Madrid walilemewa licha ya kuupigia nyumbani, na kuruhusu mabao ya Luis Suarez, Lionel Messi na Aleix Vidal kuwafanya waondoke uwanjani vichwa chini mikono nyuma.
Hii ni ni mara ya kwanza Barcelona imeweza kushinda mechi tatu za ugenini mfululizo katika uwanja wa Bernabeu. Matokeo haya yameonekana kama ya kulipiza kisasi baada ya kufungwa na wapinzani wao mabao 5-1 mwezi Agosti. Ushindi huu wa Barcelona, unaiweka alama 14 mbele ya Real Madrid katika harakati za kutafuta ubingwa msimu huu. Barca inaongoza rekodi ya kutofungwa na Real katika michuano 25 iliyocheza katika miaka ya hivi karibuni. Barcelona inaongoza msimamo wa ligi kwa alama 45, huku Real Madrid ikiwa katika nafasi ya nne kwa alama 31.
...................................TAMATI.............................