Ulimwengu wa Spoti, Jan 1
Mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita....
Handiboli: Iran yainyuka Slovania
Timu ya taifa ya handiboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kuigaragaraza Slovenia katika mchuano wa kirafiki licha ya kuupigia ugenini. Iran imeizaba Slovania alama 33-32 katika mchuano wa kujiandaa Mashindano ya Mabingwa wa Handiboli ya Asia mwaka huu 2018 nchini Korea Kusini.
Timu hiyo ya mpira wa mikono ya Iran iliekea Slovania kwa ajili ya kujitutumua misulu ikisubiri mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kwa Kimombo kama Asian Men's Handball Championship yang'oe nanga baadaye mwezi huu. Iran ipo katika Kundi A pamoja na Iraq na Japan, huku Kundi B likizijumuisha Australia, Bahrain, Oman na Uzbekistan. Mwenyeji Korea Kusini ipo katika Kundi C pamoja na Bangladesh, Imarati na India huku Kundi D likizileta pamoja China, New Zealand, Qatar na Saudi Arabia. Duru ya 18 ya mashindano hayo ya kikanda itapigwa mjini Suwon, huko Korea Kusini kati ya Januari 18 na 28, na mabingwa wataliwakilisha bara Asia katika mashindano ya dunia mwaka ujao 2019.
Yanga yadidimizwa na Mbao FC
Klabu ya Yanga ya Tanzania bara imefunga vibaya mwaka 2017 baada ya baada ya kuchabangwa mabao 2-0 na Mbao FC katika mchuano wa aina yake uliopigwa Jumapili katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza. Kiungo machachari wa Mbao FC, Habib Kiyombo ndiye aliyeoonekana nyota wa mchuano huo, kwani alifanikiwa kucheka na nyavu za Yanga mara mbili. Kiyombo alifunga bao la kwanza kunako dakika ya 53, na hata kamba ya mate kukauka, alipachika kimyani bao la pili kunako dakika ya 68.
Yanga iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi mbili za mwisho dhidi ya Mbao FC, na ilitazamiwa wangejitutumua ili kufuta uteja huo na kupata ushindi ambao ungeongeza matumaini ya kutetea ubingwa wao wa ligi msimu huu. Kwengineko, Kocha Masoud Djuma wa Simba amefanikiwa kutimiza ndoto zake za kuondoka na pointi tatu kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara baada ya kuibanjua Ndanda FC, mabao 2-0 na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwa kufikisha pointi 26 sawa na Azam FC ambayo nayo iliifunga Stand United mabao 3-0 uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Ushindi huo ni wasaba mfululizo kwa kwa Simba kuifunga Ndanda FC, ambayo tangu ipande dara misimu mitatu iliyopita haijaweza kupata ushindi mbele ya vinara hao ambao kwa sasa wana nolewa na kocha huyo wa muda baada ya Joseph Omog kufukuzwa kazi. Nahodha wa Simba John Bocco, ndiyo ameibuka shujaa katika mchezo huo baada ya kufunga mabao yote mawili na kumkaribisha vizuri kocha huyo ambaye amekabidhiwa kazi ya kukinoa kikosi hicho kilichopo kwenye presha kubwa ya kutaka ubingwa wa kwanza baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo.
Maandalizi ya CHAN 2018
Wachezaji 30 wa timu ya taifa ya soka ya Uganda, wametajwa kuanza maandalizi ya fainali ya kuwania taji la ska barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN 2018. Kikosi hicho kitapunguzwa na kufikia wachezaji 23, kuelekea michuano hiyo itakayofanyika nchini Morocco kati ya mwezi Januari na Februari. Uganda Cranes inaanza mazoezi siku ya Jumatano katika uwanja wa Namboole jijini Kampala. Kadhalika Rwanda imekitaja kikosi chake kitakachopambana katika mashindano hayo ya kikanda, wakiwemo wachezaji watatu ambao wakishuriki michuano ya Cecafa nchini Kenya mwezi uliopita. Amavubi ipo Kundi C ikiwa pamoja na Libya, Nigeria na Equatorial Guinea.
Ligi ya Premier
Klabu ya Arsenal imelipiza kisasi na kuicharaza Crystal Palace mabao 3-2 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza wa kufunga mwaka. Palace imekubali kichapo hicho licha ya kuwa pointi moja nje ya mduara hatari wa kutemwa. Matumaini ya Palace kuimarika zaidi yalizimwa baada ya Sanchez kufuma wavuni mabao mawili ya haraka.
Kwengineko Chelsea imeinyoa kwa chupa Stoke City kwa kuidhibu mabao 5-0 katika mchuano mwingine wa Ligi ya Premier. Vijana wa mkufunzi Antonio Conte wamefunga mwaka vizuri licha ya kukabiliwa na visiki chungu nzima mwanzoni mwa msimu. Mabao ya Rudiger, Drinwater, Pedro, William na zappacosta yalitosha kuidhalilisha Stoke.
Ushindi huo umewafanya vijana wa The Blues kusogea hadi katika nafasi ya pikli wakiwa na alama 45. Man City wamejikita kileleni wakiwa na alama 59 huku Man U wakiridhika na nafasi ya tatu kwa sasa wakiwa na pointi 44.
Na nikudokeza kuwa, siku chache baada ya staa wa zamani wa kimataifa wa Ivory aliyekuwa anavichezea vilabu vya Arsenal na Galatasaray Emmanuel Eboue atangaze kuwa amefilisika kutokana na mkewe kuchukua mali zote na kukiri kuwa limewahi kumjia wazo la kujiua. Eboue ameripotiwa kuwa baada ya kutalakiana na mkewe aliyekuwa amezaa nae watoto watatu, amepoteza utajiri wake wote kutokana wakati alipokuwa anacheza soka kila utajiri wake wote alikuwa kamuandikisha mkewe kitu ambacho kinamgharimu kwa sasa. Staa huyo amekiri kufilisika na kukosa pesa za kulipa wanasheria ili kumtetea lakini amefikia kukosa hata pakulala na pesa ya kupeleka nguo dry cleaner hivyo alilazimika kuwa anafua kwa mkono, siku moja baada ya taarifa hizo kutoka huku Eboue akitangaza. Klabu ya Galatasaray ya Uturuki ambayo amewahi kuichezea kwa kipindi cha baada ya kuondokaArsenal mwaka 2011, imetangaza kumpa kadhi ya ukocha msaidizi wa timu ya U-14 ya Galatasaray, kumpa makazi na kumlipa mshahara utakaomuwezesha kujikimu na kuishi vizuri.
...................................TAMATI..........................