Jan 23, 2018 07:22 UTC
  • Aya na Hadithi (5)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Hii ni siku nyingine tunapokutaka katika kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho huchambua masuala mbalimbali kwa msingi wa Aya za kitabu kitakatifu cha Qur'ani na Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) na Maimamu watoharifu wa Nyumba yake (as).

Wapenzi wasikilizaji, katika kipindi kilichopita tulijadili Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Ja'ffar As-Swadiq (as) ambayo inazungumzia tiba ya Qur'ani kuhusiana na hali nne ambazo humsababishia mwanadamu matatizo na kumletea huzuni moyoni. Katika kipindi hicho tulijadili na kufafanua suluhisho na tiba ya Qur'ani Tukufu kuhusiana na hali ya kwanza nayo ni hofu inayomkumba mwanadamu anapokabiliwa na hatari. Katika kipindi cha leo, kwa uwezo wake Mweyezi Mungu, tutazungumzia tiba nyingine za Qur'ani kuhusiana na hali nyingine tatu zilizosalia. Hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi ili tupate kunufaika kwa pamoja na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili, karibuni.

 

Ndugu wasikilizaji, kabla ya kuzingatia Hadithi Tukufu tutakayoizungumzia leo, ni muhimu kwanza kuashiria hapa kwamba Aya na Hadithi Tukufu za Bwana Mtume (saw) zinasema wazi kwamba Mwenyezi Mungu aliwateremshia wanadamu Qur'ani ambayo humo mna tiba kwa ajili yao. Hivyo basi, kama zinavyosisitiza Hadithi, tunapasa kutafuta humo tiba ambayo itatuwezesha kutibu na kutatua matatizo yetu mengi ambayo tunakabiliwa nayo katika maisha yetu ya kila siku. Hili ndilo jambo ambalo Hadithi Tukufu zinatusaidia kulifikia. Moja ya Hadithi hizo ni Hadithi hii ambayo imenukuliwa na Sheikh Swaduq katika vitabu vyake kadhaa vya kuaminika, kikiwemo kitabu cha Man La Yahdhuruhu al-Faqih. Katika kitabu hicho Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema: ''Ninashangazwa na mtu anayehofia mambo manne ni vipi hakimbilii mambo manne: Ninashangazwa na mtu aliye na woga vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya liliowagusa (173-174).

Ninashangazwa na mtu aliyehuzunika ni vipi hakimbilii kauli yake (Mwenyezi Mungu inayosema: Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na ghamu (dhiki). Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa waumini (Anbiyaa 87-88).

Ninashangazwa na mtu anayefanyiwa makri, ni vipi hakimbilii kauli yake (Mwenyezi Mungu) inayosema: Nami ninamkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu akisema mara tu baada ya kauli hii: Basi Mwenyezi Mungu akamlinda na ubaya wa makri (hila) walizozifanya (al-Mu'min 44-45).

Na Ninamshangaa mtu anayetaka dunia na mapambo yake ni vipi hakimbilii kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Mashaallah! Alitakalo Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu nimemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu akisema mara tu baada ya kauli hii: Ikiwa unaniona mimi nina mali kidogo na watoto kuliko wewe, basi asaa (huenda) Mola wangu akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako (al-Kahf 39-40). Na asaa hapa ina maana ya wajibu, yaani inayowajibisha (inayoleta) heri.'

 

Kwa hivyo ndugu wasikilizaji, tiba ya pili ya Qur'ani Tukufu ambayo anatuelekeza kwake Imam wetu as-Swadiq (as) ni kutamka dhikri ya:  Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Hii ndiyo tiba inayotibu hali ya huzuni inayotukumba tunapokuwa katika mazingira ya huzuni inayosababishwa na mabalaa mbalimbali yanayotusibu maishani. Dhikri hii inatokana na Aya mbili za 87 na 88 za Surat al-Anbiyaa ambazo zinahadithia kisa cha Nabii Yunus (as). Hebu tutegee sikio Aya hizo ambapo Mwenyezi Mungu Suhbanahu wa Taala anasema: Na Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu. Basi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na ghamu (dhiki). Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa waumini.

Kwa kuzingatia kwa makini Aya mbili hizi wapenzi wasikilizaji, tunafikia natija hii kwamba tiba ya Qur'ani katika kukabiliana na balaa lolote linaloweza kumfika mwanadamu inapatikana katika kunyenyekea na kuomba mja dua ya ikhlasi mbele ya Mwenyezi Mungu pamoja na kukiri kwake juu ya Tauhidi na Umola wake Mungu Muumba. Katika unyenyekeaji na uombaji duo huo, mja pia anapasa kumuondolea Mwenyezi Mungu sifa zote mbaya zinazokwenda kinyume na uadilifu wake, ukiwemo uwezekano wa yeye kudhani kuwa huenda ameteremshiwa balaa hilo kinyume na uadilifu wake Mola. Anapokuwa katika hali hiyo anapasa kukiri bayana kwamba yeye ndiye aliyefanya dhambi iliyomtumbukiza kwenye balaa hilo na hiyo ndiyo maana ya dhikri hii ya Qur'ani Tukufu inayosema: Hapana mungu isipokuwa Wewe Subhanaka uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.

Na Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya pili: Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa waumini. Katika Aya hii kuna bishara nzuri nayo ni kwamba wokovu unaotokana na dhikri hii haumuhusu Nabii Yunus (as) peke yake bali unawajumuisha waumini wote wanaotawasali na kumtegemea Mwenyezi Mungu kwamba, iwapo watatumia tiba hii ya Qur'ani bila shaka watapata kuondokewa na huzuni na balaa lolote linalowasibu maishani.

 

Ndugu wasikilizaji, ama tiba ya tatu ya Qur'ani Tukufu inajumuisha hali zote za hila na makri zinazomsibu mu'mini kama zile zilizomsibu Mumini wa Aal Firauni (MA). Ufunguo wa tiba hii ni dhikri ambayo imekuja katika Aya ya 44 ya Surat al-Ghafir ambayo inasimulia kisa cha kuvutia cha Mu'mini huyu mwema. Dhkri hiyo inasema: Nami ninamkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yangu. Hakika Mwenyezi Mungu anawaona waja wake.

Kumkabidhi Mwenyezi Mungu mambo ya mja ni kuthibitisha imani ya kwamba Yeye ndiye anayeona na kujua kwa kina kila jambo la mja na kwamba Yeye ndiye suluhisho na tiba ya makri na hila zozote anazokabiliwa nazo mwanadamu kutoka kwa maadui au shetani.

Kwa haya wasikilizaji wapenzi, inabakia tiba ya nne ya Qur'ani Tukufu ambayo imetajwa kwenye Hadithi tunayoijadili hapa nayo ni ile inayoondoa udhia unaowapata masikini kutokana na matajiri kujigamba mbele yao kwa mali zao. Hili ndilo jambo tutakalolijadili katika kipindi chetu kijacho cha Aya na Hadithi, Inshallah. Basi hadi wakati huo, kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, hatuna la ziada isipokuwa kukuageni huku tukikutakieni kila la kheri maishani. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.