Feb 05, 2018 07:12 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo: Morocco yatwaa taji la CHAN, Iran yazinyuka China na Myanmar Futsal

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa RT na karibu tutupie jicho matukio mawili matatu ya michezo yaliyogonga vichwa habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....

Iran yamaliza ya 2 katika michezo ya Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka katika nafasi ya pili katika mashindano ya michezo mbalimbali ya mabingwa wa bara Asia. Wanamichezo wa Iran wamezoa medali kochokocho kwenye mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama Asian Indoor Athletics Championships yaliyofanyika katika Ukumbi wa Michezo wa Aftabe Enghelab katika mji mkuu wa Iran, Tehran. Iran ya Kiislamu imejikusanyia medali tano za dhahabu, 9 za fedha na 10 za shaba.

Wairani wazoa medali chungu nzima

Kazakhstan ndiyo iliyoibuka kidedea katika mashindano hayo, kwa kuzoa medali saba za dhahabu, nne za fedha na moja ya shaba, huku Qatar ikimaliza katika nafasi ya tatu kwa kutia kibindoni medali tano za dhahabu, tatu za fedha na shaba mbili. Duru ya nane ya mashindano hayo ya kikanda iling'oa nanga Februari Mosi na kutamatika Februari 3, kwa kuwaleta pamoja wanamichezo 360 kutoka nchi 22 za Asia.

Futsal: Iran yazinyuka Myanmar na China

Timu ya mripa wa miguu unaochezewa ukumbini maarukufu kama futsal ya Iran imeanza vyema mashindano ya bara Asia ya mchezo huo kwa kuinyoa bila maji Myanmar. Vijana wa Iran waliibamiza Myanmar magoli 14-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi C uliopigwa katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Taipei mjini Taipei.

Timu ya taifa ya Futsal ya Iran

Katika mechi ya pili ya makundi, Iran iliigaragaza China magoli 11-1. Duru ya 15 ya mashindano hayo ya bara yaitwayo AFC Futsal Championship inatazamiwa kufunga pazia lake Februari 18. Iran ipo katika kundi pamoja na mibabe ya Asia katika mchezo wa futsal ikiwa ni pamoja na China, Iraq na Mynamar.

CHAN: Morocco bingwa wa Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Morocco imeibuka kidedea katika michuano ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) baada ya kuisasambua Nigeria mabao 4-0 katika mchuano wa fainali uliopigwa Jumapili usiku mjini Casablanca. Vijana wa Kiarabu ambao walikuwa wanaupiga nyumbani waliupa maana msemo usemao 'mcheza kwao hutuzwa'. Mchezaji wa Morocco Zakaria Hadraf ndiye aliyekuwa nyota ya mchezo huo kwa kufanikiwa kupachika wavuni mabao mawili. Alipaichika kimyani bao la kwanza muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko, baada ya kuchongewa krosi saafi na Abdeljalil Jabira. Walid El Karti aliwaongezea wenyeji Morocco bao jingine kabla ya kiungo mahiri Ayoub El Kaabi, ambaye amefunga jumla ya mabao tisa kwenye mashindao hayo, kupiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la vijana wa magharibi mwa Afrika.

Wachezaji wa Morocco wakitunukiwa Kombe na medali

Wenyeji Morocco walikuwa wa kwanza kufuzu fainali baada ya kuichabanga Libya mabao 3-1 katika mchuano wa nusu fainali uliochezwa Jumatano usiku katika uwanja wa Mohammed wa Tano, mjini Casablanca. Nigeria nao walitinga fainali kufuatia ushindi wa bao 1-0, katika mchuano dhidi ya Sudan uliochezwa katika uwanja wa Marrakech. Hii ndio mara ya kwanza kwa Morocco na Nigeria kufika katika hatua ya fainali ya michuano hii. Kwa ushindi huo, mwenyeji Morocco ambayo italiwakilisha bara Afrika katika Kombe la Dunia mwakani nchini Russia, imezawadiwa dola milioni 1.25 za Marekani. Kwengineko Sudan ilimaliza katika nafasi ya tatu katika michuano hiyo ya CHAN na kutunukiwa medali ya shaba, baada ya kuishinda Libya mabao 4-2 baada ya kupigwa kwa mikwaju ya penalti. Mchuano huo ulikwenda katika hatua hiyo baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada. Huu ni ushindi mkubwa kwa Sudan inayofunzwa na kocha kutoka Croatia Zdravko Logarusic na matokeo haya yamewashangaza wengi ambao hawakuipa nchi hiyo nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano haya.

Raga: Kenya yatinga robofainali

Timu ya taifa ya mchezo wa raga ya Kenya almaarufu Shujaa imetinga robofainali ya Raga ya Dunia ya Hamilton Sevens nchini New Zealand, bila kushindwa katika Kundi D siku ya Jumamosi. Vijana wa kocha Innocent Simiyu walitikiswa kidogo katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Samoa kabla ya kuishinda 19-14 na kisha kupata ushindi sawa na huo dhidi ya Canada katika mechi ya pili kabla ya kufuzu robofainali, baada ya kutoa sare ya 19-19 walipovaana na Marekani. Shujaa ilihitaji ushindi ama sare katika mechi yake ya mwisho dhidi ya kocha wake wa zamani Mike Friday, ambaye anainoa Marekani, ili itinge robofainali.

Ligi ya Premier

Tunatamatisha kwa kutupia jicho matokeo ya baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Klabu ya Manchester United iliichachafya Huddesfield mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Jumamosi uwanjani Old Trafford. Na ili kuonyesha thamani yake na ari ya ujio wake Man U, kiungo mpya wa klabu hiyo Alexis Sanchez ndiye aliyefunga bao la pili katika mchuano huo, kunako dakika ya 68, baada ya Romelu Lukaku kufunga la kwanza.

Huku hayo yakijiri, Arsenal walikuwa wenyeji wa Everton katika uwanja wao wa Emirates na walifanikiwa kupata ushindi mnono wa magoli 5-1. Goli la nne la Arsenal la dakika ya 37 lilifungwa na Pierre Emerick Aubameyang, ikiwa ni siku chache tu toka staa huyo ajiunge na klabu hiyo. Magoli mengine ya Arsenal yalifungwa na Aaroon Ramsey aliyefunga hat-trick dakika ya 6, 19, 74, Koscielny dakika ya 14 na Pierre Emerick Aubameyang dakika ya 37. Hatrick ya Ramsey ingali gumzo vinywani mwa mashabiki wa soka ya Uingereza.

Lukaku

Kwengineko Manchester City wanaoongoza ligi kwa sasa kwa alama 69 walilazimishwa sare ya 1-1 na Burnley, namna ambavyo mabingwa watetezi Leicester City walivyofanywa na Swansea. Man U wapo katika nafasi ya pili wakiwa na alama 56, huku Liverpool ambayo Jumapili ilivaana na Tottenham na kutoa sare ya mabao 2-2, kwa sasa ikifunga orodha ya tatu bora kwenye msimamo wa Ligi ya Premier. Mabao mawili ya Liverpool siku ya Jumapili yalifungwa na kiungo nyota raia wa Misri ns mshindi wa tuzo ya CAF, Mohammed Salah. Hata hivyo Tottenham walisawazisha mambo kupitia magoli ya Mkenya Victor Wanyama na Harry Kanes.

…………………….TAMATI…………………

 

 

Tags