Feb 05, 2018 23:14 UTC
  • Jumanne tarehe 6 Februari 2018

Leo ni Februari 19 Jamadil Awwal, 1439 Hijria sawa na 6 Februari, 2018.

Siku kama hii ya leo miaka 39 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini baada ya kutangazwa serikali ya muda ya Mapinduzi. Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Katika siku hiyo pia wananchi wa Iran na kwa sauti moja walitaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu. Siku hiyo pia Jenerali Robert E. Huyser, mjumbe maalumu wa Marekani aliyekuwa Tehran kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuubakisha madarakani utawala wa Shah Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa makamanda wa jeshi la Shah, alifunga virago na kurejea Marekani baada ya kushindwa kusitisha wimbi la Mapinduzi ya Kiislamu.

Jenerali Robert E. Huyser

Miaka 82 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo. Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri.

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo. Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani.

Siku kama ya leo miaka 528 iliyopita Abulfadhl Abdulrahman Suyuti, mashuhuri kwa lakabu ya Jalaluddin, faqihi, mpokezi wa hadithi na mtaalamu maarufu wa lugha wa zama hizo alifariki dunia mjini Cairo. Jalaluddin Suyuti alizaliwa mwaka 849 Hijria na alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana. Jalaluddin Suyuti kwa miaka kadhaa alijifunza masomo ya fiqih, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na lugha na kupata mafanikio makubwa. Msomi huyo wa Cairo ameandika vitabu vingi vya thamani na miongoni mwavyo ni "Al Iqtirah", "Al Kitabul Kabir" na "Tarikhul Khulafaa".

Na Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, sawa na tarehe 6 Februari 1904, vilianza vita kati ya Japan na Russia, baada ya majeshi ya Japan kuvishambulia vikosi vya Russia huko China. Japan iliyokuwa imejizatiti vyema kijeshi, mwaka 1895 iliishinda vibaya China na kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo. 

Vita vya Japan na Russia