Jumanne tarehe 27 Februari, 2018
Leo ni Jumanne tarehe 10 Jamadithani 1439 Hijria sawa na Februari 27, 2018.
Miaka 812 iliyopita katika siku kama hii ya leo ya tarehe 10 Jumadi Thani alifariki dunia arif na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Sheikh Fariduddin Attar Naishaburi. Attar Naishaburi alizaliwa mwaka 513 Hijria na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya ulimwengu wa Kiislamu ya kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Baadhi ya nukuu za kihistoria zinasema msomi huyo kubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi katika mashambulizi ya Mogul.
Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantwiqut Twair."
Tarehe 27 Februari miaka 116 iliyopita alizaliwa mwandishi wa riwaya wa Kimarekani, John Steinbeck katika jimbo la California. Alijiunga na chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 17 na kuacha masomo kabla ya kupata shahada yake. Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi. Kitabu cha kwanza cha riwaya cha mwandishi huo ni Cup of Gold akichokiandika akiwa na umri wa miaka 27. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari tofauti, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away, Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.
Miaka 82 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ivan Petrovich Pavlov, tabibu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya biolojia wa Russia akiwa na umri wa miaka 87. Alizaliwa mwaka 1849 katika familia ya kidini na mwaka 1879 alihitimu elimu ya udaktari. Tabibu huyo alikuwa na shauku kubwa ya kufanya utafiti kuhusu miili ya wanyama inavyofanya kazi. Aidha alifanya utafiti mkubwa kuhusu mzunguko wa damu. Mwaka 1904 Pavlov alitunukiwa tuzo ya Nobel.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 27 Fabruari 1942 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, yalianza mashambulizi makubwa ya ndege za Japan dhidi ya vituo vya majini vya nchi waitifaki. Mashambulizi hayo yalitokea katika Bahari ya Java. Idadi kubwa ya meli za kivita za Marekani, Australia na Uingereza zilikuwa zimejizatiti katika bahari hiyo. Mapigano hayo makubwa yalimalizika kwa kuzama idadi kubwa ya meli za nchi hizo tatu na kupata ushindi manowari za kijeshi za Japan.
Na siku kama ya leo miaka 7 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Najmuddin Erbakan akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Najmuddin Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Najmuddin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.