Mar 04, 2018 16:18 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (108)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia maudhui ya kuchunga staha, umakini, utulivu na kufanya mambo kwa umakini na kutafakari kabla ya kufanya jambo husika na kujiepusha na pupa na papara katika mambo.

 

Tulisema kuwa, moja ya sifa muhimu kabisa za kimaadili na zenye nafasi ya aina yake katika maisha ya mtu binafsi, familia, jamii na hata katika mahusiano na mdakhala wa kisiasa na kiuchumi wa mtu ni utulivu na staha. Aidha tulibainisha kwamba, utulivu, subira na umakini katika mambo, humfanya mtu achukue hadhari na kuwa na hali ya kutaamali na kutafakari katika kuzungumza na kufanya mambo. Tulinukuu pia hadithi kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib AS inayosema: Subira na utulivu katika kufanya mambo na kujiweka mbali na pupa na haraka humuepusha muumini na udhaifu na hali ya kulegalega. Kadhalika tulibainisha umuhimuu wa mtu kuchunga hadhi na heshima yake ambapo anapaswa kuchunga wapi pa kuzungumza na nini cha kuzungumza ili asije akashusha hadhi na heshima yake mbele ya wengine suala ambalo litamfanya aonekane duni na asiye na hadhi na heshima.

 Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 108 ya mfululizo huu, kitazungumzia suala la ushindani na kubainisha maana hasa ya ushindani na kueleza ushindani mbaya na mzuri katika maisha yetu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Moja ya misukumo muhimu kwa ajili ya kufanya harakati, hima na idili kwa shabaha ya kufikia malengo ni kushindana. Ushindani salama na usio na rafu ndani yake na ambao unachunga na kuheshimu vigezo vya kimaadili pamoja na miamala ya kiutu na kibinadamu ni jambo la kupendeza kwa mujibu wa akili na sheria. Katika aya ya 48 ya Surat al-Maida, Mwenyezi Mungu anawashajiisha watu ili washindane. Aya hiyo inasema: Basi shindaneni katika mambo ya kheri.

Basi shindaneni katika mambo ya kheri.

 

Aina hii ya ushindani katika mambo haina maana kufanya uharibifu au kumuondoa uwanjani mpinzani, bali ni hatua ambayo inalenga kurekebisha au kuboresha zaidi mambo. Kwa hakika ushindani ni moja ya misukumo muhimu ya mwanadamu kwa ajili ya kufanya harakati.

Chimbuko la ushindani linaweza kuwa ni kuhisi mapungufu, husuda, masikitiko ya kukosa kitu, kuondokana na mapungufu na kupata ukamilifu. Kwa msingi huo, ushindani unaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili. Ushindani chanya na hasi yaani ushindani unaofaa na usiofaa.

Kwa mtazamo wa Uislamu ni kuwa, fursa ndogo ya umri kwa wanadamu hapa duniani, ni mithili ya uwanja wa mashindano ambapo kila mtu anapaswa kufanya hima na idili kwa kasi kubwa ili aweze kufikia daraja ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.

Ili kufikia lengo hilo, kuna haja ya kutumia mbinu, mikakati na nyenzo mwafaka katika fremu ya misingi ya kimaadili. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Bwana Mtume saw anaeleza falsafa ya kubaathiwa na kupewa Utume akisema: Nimetumwa (kama Mtume) ili kuja kukamilisha maadili.

Kwa muktadha huo basi, ushindani salama unapaswa kuwa ni wenye kuchunga kikamilifu suala la maadili na kuwa katika fremu ya vigezo na miamala ambayo inapendwa na akili na sheria na kwamba, ushindani wowote ule ambao uko nje ya misingi na vigezo hivi, utatambuliwa na kuhesabiwa kuwa ni ushindani usio salama na ambao una rafu na mchezo mchafu ndani yake.

Kwa hakika mwanadamu daima huwa na hamu na shauku ya kuwa mkamilifu na mkamilifu zaidi na ni kwa sababu hiyo ndio maana hufanya harakati na shughuli hizi na zile. Hii hali ya kutaka kuwa kamili zaidi na mbora zaidi ni katika kujilinganisha na wenzake na ndio maana kuna hisia ya kushindana.

Hata hivyo, hisia ya kushindana au kuwa na hamu na shauku ya kuwa bora na bora zaidi, kuna tofauti kubwa na sifa mbaya na chafu kama kujiona, kutakabari na kujikweza. Ukweli ni kuwa, kama hisia ya kutaka ushindani itakuwa katika mambo ya kimaada na mabaya, hali hiyo itapelekea kuibuka mizozo na mivutano katika uhusiano wa mtu na jamii. Lakini kama ushindani huo utakuwa ni katika masuala ya kimaanawi na kimaadili na kwamba, kila mtu awe na kasi na ushindani katika mambo mazuri na ya kheri na awe akipigania kuwa mstari wa mbele na kuwatangulia wengine katika kutenda mema, basi hatua hiyo itahesabiwa kuwa ni nzuri na ya kimaadili.

 

Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib as anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Enyi watu! shindaneni na wengine katika kufanya mambo mema na kuweni na kasi katika kunufaika na fursa.

Wapenzi wasikilizaji ushindani ni aina fulani ya mashindano ambapo upande mmoja kati ya pande mbili ambao utafanya hima na idili zaidi huibuka na ushindi. Katika aya nyingi katika Qur'ani, Mwenyezi Mungu anautambulisha ushindani kama kitu chenye thamani na anawashajiisha watendao wema kufanya ushindani. Aya ya 22 hadi ya 26 za Surat al-Mutafifin zinasema:

"Hakika watu wema bila ya shaka watakuwa katika neema. Wakae juu ya viti vya enzi wakiangalia. Utatambua katika nyuso zao mng'aro wa neema, Watanyweshwa kinywaji safi kiliyo tiwa muhuri. Muhuri wake ni miski. Na katika hayo washindanie wenye kushindana."

Bwana Mtume saw ambaye ni mbora wa viumbe, alikuwa akiwatahadharisha sana Waislamu kuhusiana na kushindana katika mambo ya dunia kutokana na hasara na hatari zinazopatikana katika hilo. Lakini katika upande wa pili, alikuwa akiwashajiisha Waislamu kufanya ushindani katika taqwa, kumcha Mwenyezi Mungu na kujikurubisha kwa Mola Muumba kupitia amali njema , matendo mema na stahiki.

Aidha Mtume alikuwa akiwashajiisha pia Waislamuu kufanya ushindani katika kufanya kazi zenye sudi na faida ambazo zinaimarisha moyo wa ushujaa na ujasiri. Kwa mfano alikuwa akiwashajiisha kufanya mashindano ya upandaji farasi na kulenga shabaha na hata mwenyewe alikuwa akishiriki katika michezo hiyo.

Imam Ali bin Hussein Zeinul Abidin as asimulia kwamba: Baada ya wapiganaji wa Kiislamu kurejea kutoka katika vita vya Tabouk, Mtume saw alitoa amri ya kufanyika mashindano ya ngamia. Usama bin Zeid ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo na ambaye alimtumia ngamia wa Mtume katika mashindano hayo aliibuka na ushindi. Watu wote walioshiriki katika mashindano hayo wakawa wakisema kwamba, Mtume saw ndiye aliyeshinda. Lakini Mtume saw alisema kuwa, Usama ndiye aliyeshinda.

Kwa hakika ushindani mzuri ni ule ambao una vigezo vya Kimwenyezi Mungu ndani yake. Aina hii ya ushindani ndani yake kuna hamu na shauku ya kumili kuelekea katika ukamilifu. Mshindani mwenye kumtafuta Mwenyezi Mungu na mwenye akili huwa hapendi watu wengine wawe nyuma, bali hupenda kuona watu wote wanakuwa wema na wazuri na yeye awe mwema zaidi miongoni mwao, watu wote wawe wenye nguvu, imara na madhubuti na yeye awe mwenye nguvu zaidi na watu wote wafanye harakati kuelekea mbele lakini yeye awe mbele yao zaidi.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Imam Ali AS anasema kuwa, kushindana na watu wenye akili kunarekebisha maadili na tabia.

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati, ni matumaini yangu kuwa mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa leo.Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini……