Alkhamisi tarehe 22 Machi, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Rajab 1439 Hijria sawa na tarehe 22 Machi, 2018.
Leo tarehe 22 Machi ni Siku ya Maji Duniani. Kukua kwa kasi jamii ya watu na kuongezeka matumizi ya maji, kukatwa miti ovyo, kuharibiwa misitu na mabadiko ya tabia nchi, kupanuka kwa miji na ongeseko la viwanda na mbinu zisizofaa za kilimo, ujenzi wa mabwawa na kadhalika vimesababisha uharibifu wa mfumo wa upatikanaji wa maji katika upeo wa dunia na kuhatarisha maisha ya viumbe hai hususan mwanadamu. Kwa sababu hiyo mwaka 1992 kulifanyika mkutano wa kimataifa katika mji wa Rio De Janeiro huko Brazil ambao uliitanghaza siku hii ya leo kuwa Siku ya Maji Duniani kwa ajili ya kuwazindua wanadamu na kuwakumbusha umuhimu wa maji.

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita aliuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin mwanachuoni na mwasisi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pamoja na watu wengine 10. Sheikh Ahmad Yassin aliuawa shahidi baada ya kumaliza swala ya Alfajiri katika msikiti mmoja ulioko eneo la Ukanda wa Gaza, wakati aliposhambuliwa na helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel. Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati ya Hamas mwaka 1987 akishirikiana na wanamapambano wengine kadhaa wa Kipalestina na miaka miwili baadaye alifungwa jela na utawala ghasibu wa Israel. Mauaji ya mpigania uhuru huyo ambaye alikuwa kiwete na kipofu wakati wa kuuawa kwake, yalidhihirisha tena ugaidi wa kiserikali wa utawala haramu wa Israel.

Tarehe Pili Farvardin 1361 Hijria Shamsia, ambayo ni sawa na tarehe 22 Machi mwaka 1982 Miladia, (miaka 36 iliyopita), ilianza operesheni kubwa ya 'Fat-hul Mubiin' ya wapiganaji shujaa wa Kiislamu huko kusini magharibi mwa Iran kwa shabaha ya kuyarejesha nyuma majeshi vamizi ya Iraq. Kwenye operesheni hiyo iliyopelekea kukombolewa miji ya Dezful, Andimeshk, Shush na mamia ya vijiji vya eneo hilo, wanajeshi wasiopungua elfu 25 wa Iraq waliuawa na wengine elfu 15 kukamatwa mateka.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, inayosadifiana na 22 Machi 1945, iliundwa Jumuiya ya Waarabu kutokana na mapendekezo ya Farouk, aliyekuwa mfalme wa wakati huo wa Misri na kutiwa saini makubaliano hayo ya kuundwa jumuiya hiyo na serikali za Syria, Iraq, Saudi Arabia, Misri na Yemen mjini Cairo. Lengo la kuanzishwa jumuiya hiyo lilikuwa ni kuhifadhiwa ardhi zote, kujitawala nchi wanachama, kuwepo ushirikiano wa karibu wa kisiasa kiuchumi na kiutamaduni kati ya wanachama.

Siku kama ya leo leo miaka 137 iliyopita ulianzishwa Muungano wa Soka wa Kimataifa kwa shabaha ya kusimamia mashindano ya mpira wa miguu kote duniani. Kabla ya kuundwa muungano huo, mashindano ya soka yalikuwa yakifanyika katika nchi mbalimbali kwa sura isiyokuwa rasmi. Muungano huo ulibadilisha muundo wake na kujulikana baadaye kwa jina la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na liliandaa pambano rasmi la kwanza la kimataifa mwaka 1901, kati ya Uingereza na Ujerumani.

Miaka 847 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alifariki dunia malenga wa Kiislamu Muhammad ibn Ali al-Wasiti maarufu kwa jina la Ibnul Muallim. Alizaliwa mwaka 501 Hijiria. Mashairi ya malenga huyo yalibeba ujumbe wa maadili na tabia njema na masuala mengine yanayohusu. badhi yya mashairi yake pia yanahusiana na maudhui za irfani. Athari pekee ya Ibnul Muallim ni diwani ya tungo za mashairi ya malenga huyo.
