Mar 26, 2018 06:11 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Machi 26

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita...

Soka: Iran yakubali kichapo kutoka Tunisia

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekubali kichapo cha bao 1-0 kutoka Tunisia katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa Ijumaa usiku. Nusra mchezo huo umalizike kwa sare ya 0-0, lakini mchezaji wa safu ya ulinzi wa Iran, Milad Mohammadi alijifunga bao kimakosa katika dakika 71, baada ya kipa kutema mpira, katika mchuano uliopigwa katika Uwanja wa Michezo wa Stade 7 Novembre de Rades nchini Tunisia.

Jitihada za Iran za kusawazisha mambo katika dakika zilizosalia ziliambulia patupu. Itakumbukwa kuwa, Iran imecheza na Tunisia mara moja pekee huko nyuma, katika mchezo wa kirafiki wa Agosti mwaka 2002, uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Iran ilipochuana na Sierra Leone na kuinyoa 4-0

 

Jumamosi ya wiki jana, katika mchuano mwingine wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja Taifa wa Azadi hapa mjini Tehran, vijana wa Iran waliinyuka Sierra Leone mabao 4-0. Wanasoka wa Iran wanatumia mechi hizi kujitutumua misuli kuelekea Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Russia. Wairani hao wanatazamiwa kutoana udhia na Algeria nchini Austria Machi 27. Timu hiyo ya mpira wa miguu ya Iran imepangwa kuvaana na Morocco katika mchuano wa kwanza wa Kundi B katika Kombe la Dunia nchini Russia Juni 15, kabla ya kukutana na Uhispania na Ureno katika mechi nyingine za makundi Juni 20 na 25 kwa usanjari huo.

Taifa Stars yalimwa na Algeria

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars iligeuzwa kichwa cha mwendawazimu na kuchabangwa mabao 4-1 na Algeria katika mchuano wa kirafiki wa ugenini mjini Algiers, Alkhamisi usiku wa Machi 22. Magoli ya Algeria yalifungwa na Baghdad Bounedjah dakika ya 12 na 79, Shomari Kapombe wa Taifa akajifunga kwa kichwa dakika ya 44 huku Mualgeria Carl Medjani akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Tanzania, kupitia goli alilolifunga katika dakika ya 53.

Bao la kufutia machozi la Taifa Stars lilifungwa na mchezaji nyota wa Tanzania, Simon Msuva kunako dakika ya 21, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Said Ndemla.

Bendera ya Tanzania

 

Taifa Stars ilicheza dhidi ya Algeria ikiwa ni miaka mitatu imepita toka wakutane mara ya mwisho November 17 2015 katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2018, mechi ambayo ilichezwa Algeria katika uwanja wa Mustapha Tshacker na kumalizika kwa Tanzania kupoteza kwa magoli 7-0. Iwapo Stars wangelishinda mchuano huo dhidi ya vijana wa Kiarabu, yumkini wangekwea kwenye jedwali la FIFA, ambapo kwa sasa ipo katika nafasi ya 146, huku Algeria wakishika nafasi ya 60. Kocha wa Taifa Stars Salum Mayanga anasisitiza kuwa, kikosi chake kinatumia michuano hii ya kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya kikanda na pia kupanda kwenye jedwali la FIFA.

Kenya yalazimishwa sare na Wangazija

Mchezaji wa kimataifa raia wa Kenya Victor Wanyama na kiungo Clifton Miheso walifunga bao moja kila mmoja na kuisaidia Harambee Stars kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Comoros katika mechi ya kirafiki iliyopigwa katika uwanja wa Marrakech nchini Morocco Jumamosi. Kenya ilitangulia kuona lango kupitia kiungo huyu wa Tottenham Hotspur nchini Uingereza baada ya vijana wa Kingazija kucheza visivyo ndani ya kisanduku chao dakika ya nne.

Penalti hiyo ilipatikana baada ya Eric Johanna kutimka ndani ya kisanduku akifanya mashambulizi, lakini akaangushwa na beki wa klabu ya Chateauroux nchini Ufaransa, Chaker Alhadhur. Wanyama alifuma wavuni penalti hiyo baada ya kumwaga kipa Ahamada Ali. Kenya haikusalia kifua mbele kwa muda mrefu kwani Comoros ilitikisa nyavu kupitia kiungo wa Ajaccio nchini Ufaransa, Youssouf M'Changama dakika ya 20.  Bakar wa klabu ya Tours nchini Ufaransa ailipokea pasi nzuri kutoka kwa kiungo wa Nimes nchini Ufaransa, Chamed Nasser na kumwaga kipa bora wa Kenya mwaka 2017 Patrick Matasi dakika ya 73 na kuweka Comoros mbele 2-1. Nambari 105 duniani Kenya ilijinasua kutoka minyororo ya kupoteza dhidi ya nambari 132 duniani Comoros kupitia bao la Miheso dakika ya 84. Kakake Wanyama, McDonald Mariga kutoka klabu ya Real Oviedo nchini Uhispania alishirikiana vyema na Miheso wa Buildcon nchini Zambia kabla ya Miheso kukamilisha shambulizi hilo kwa kumwaga kipa wa akiba Hoima Ben Salim. Stars itamenyana na Jamhuri ya Afrika ya Kati hapo Machi 27 katika mechi nyingine ya kirafiki kabla ya kumaliza ziara ya Morocco.

 

Kwengineko, Senegal ilibanwa na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Uzbekistan mjini Casablanca katika mchezo mwingine wa kirafiki. Mjini Turin, Morocco ikiwa kwenye kiwango chake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Serbia.

Mjini Zurich, Uswisi mabao mawili ya Cristiano Ronaldo yalizima ndoto za nyota wa Liverpool, Mohamed Salah kuipa ushindi Misri dhidi ya Ureno katika mechi nyingine ya kirafiki.

Riadha: Mkenya ang'ara nusu marathon ya IAAF

Mwanariadha nyota wa Kenya, Geoffrey Kipsang Kamworor ameibuka kidedea katika mashindano ya dunia ya nusu marathon yaliyofanyika mjini Valencia nchini Uhispania Jumamosi usiku. Kamworor alikata utepe wa ushindi kwa kutumia saa moja.

Hii ni mara ya tatu kwa Mkenya huyo ambaye ni afisa wa polisi kushinda taji la IAAF World Half Marathon Championships na kutuzwa medali ya dhahabu. Binafsi anaitakidi kuwa, kuazima viatu vya bingwa wa olimpiki, Eliud Kipchoge ndiko kumempelekea aibuke mshindi kwenye mbio hizo za nyika. Rais Uhuru Kenyatta ameongoza Wakenya katika kumpongeza mwanariadha huyo kwenye mitandao ya kijamii. Kwa upande wa wanawake, raia wa Ethiopia Netsanet Kebede aliibuka mshindi katika mbio hizo za kilomita 21, kwa kutumia dakika 66 na sekunde 11, na kuvunja rekodi iliyowekwa na Mkenya Lornah Kiplagat miaka 11 iliyopita. Wakenya Joyciline Jepkosgei na Pauline Kavek walitwaa nafasi za pili na tatu kwa usanjari huo, na kurejea nyumbani na medali za fedha na shaba.

Siku ya Jumapili wanariadha wengine wa Kenya, Ezrah Kiprotich Sang na Polline Wanjiku Njeru waliibuka washindi katika mbio za Warsaw Half Marathon zilizofanyika nchini Poland. Sang alitwaa dhahabu kwa kumaliza mbio hizo za nusu marathon kwa kutumia dakika 61 na sekunde 37 katika safu ya wanaume, huko mwanadada Wanjiku Njeru akitwaa taji la wanawake kwa kutumia dakika 70 na sekunde 01.

…………………...TAMATI….……………