Jumamosi, Machi 31, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Rajab 1439 Hijria sawa na tarehe 31 Machi 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1462 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatu Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini pia Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge. ***

Miaka 1160 iliyopita alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi hafidh wa Qur'ani tukufu na mpokeaji hadithi mashuhuri wa Kiislamu. Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na hadithi. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wa Imam Bukhari na kitabu chake maarufu zaidi ni Jamiu Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya hadithi katika madhehebu ya Suni.***

Katika siku kama ya leo miaka 422 iliyopita yaani tarehe 31 Machi mwaka 1596, alizaliwa Rene Descartes mwanafalsafa, mwanahisabati na mwanafizikia wa Kifaransa. Descartes alifikia daraja ya uhadhiri wa Chuo Kikuu baada ya kuhitimu masomo ya falsafa na hisabati. Aidha msomi huyo wa Kifaransa kipindi fulani alifanya safari katika nchi mbalimbali na baadaye aliishi Uholanzi na kuanza kufanya utafiti. Rene Descartes aliitambua hisabati kuwa elimu kamili miongoni mwa elimu nyinginezo na kutaka kutumiwa elimu hiyo katika fani nyinginezo za kielimu. Miongoni mwa vitabu vya mwanafalsafa huyo ni Principles Of Philosophy, The Passions of the Soul na Discourse on the Method.***

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, garimoshi lililokuwa likitoka Cairo Misri likielekea katika bandari ya Haifa huko Palestina lililipuliwa kwa bomu, ikiwa ni katika kuongezeka mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina yaliyokuwa yakifanywa na Wazayuni maghasibu. Wapalestina 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika jinai hiyo iliyofanywa na kundi moja la Kizayuni. Siku nne kabla ya mlipuko huo, garimoshi jingine lililipuliwa huko Palestina na Wazayuni wenye silaha, na kuuwa Wapalestina 24 na kujeruhiwa wengine 61. ***

Na katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zilisimamisha uanachama wa Misri katika jumuiya hiyo na nchi nyingi wanachama zikakata uhusiano wao na Cairo. Nchi za Kiarabu zilionesha radiamali hiyo kali kwa Misri baada ya rais wa zamani wa Misri Anwar Sadat kusaini hati ya mapatano ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel mwezi Januari mwaka 1978.
