Apr 03, 2018 13:15 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 31 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizunguumzia namna ambavyo Waislamu wa nchi za Magharibi hususan Uingereza wamekuwa na ada ya kugawa kadi za pongezi kwa mnasaba wa kuzaliwa Nabii Isa (as) na ambazo huwa zinaambatanishwa na aya za Qur'ani Tukufu na picha ya msikiti wa al-Aqsa mwishoni mwa kila mwaka wa Miladia. Na kama alivyosema Dakta Mohammed Fahim, mmoja wa viongozi wa taasisi ya Kiislamu ya mjini London, kadi hizo huwa zinagawiwa familia ya kifalme nchini humo, wawakilishi wa bunge, makanisa, vyuo vikuu, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, viongozi wa Umoja wa Ulaya na hata majirani na marafiki wa Kikristo.

Malikia Elizabeth wa Uingereza ambaye naye huwa anaagiziwa barua kutoka kwa Waislamu na kuzijibu

Suala la kuvutia zaidi ni kwamba, kwa miaka yote Malkia Elizabeth pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza huwa wanajibu jumbe za kadi hizo. Kufuatia hali hiyo Dakta Mohammed Fahim ameonyesha matarajio kwamba kadi hizo hatimaye zitaweza kusaidia kurekebisha mtazamo hasi wa jamii ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Magharibi kuhusu dini ya Uislamu na wafuasi wake kwa ujumla. Aidha baadhi ya Waislamu barani Ulaya sambamba na kuwadia tarehe ya kuzaliwa Nabii Isa (as) wamebuni njia bora kwa ajili ya kuitangaza dini ya Kiislamu kwa wafuasi wa dini ya Ukristo. Moja ya njia hizo ni ile iliyoshuhudiwa kwa mamia ya vijana wa Kiislamu wa Uingereza kufanya kampeni ya kukusanya taka na kufanya usafi katika mitaa ya nchi hiyo. Kampeni hiyo ilianzishwa miaka mitatu iliyopita kwa kuwashirikisha vijana Waislamu wenye kujitolea katika miji ya London, Glasgow-Scotland, Cardiff-Wales, Birmingham, Leicester, Manchester, Newcastle na miji mingine ya nchi hiyo.

Mtume Muhammad (saw) alihimiza usafi, udugu, upendo, amani na Uadilifu nk

Aidha vijana Waislamu asubuhi ya tarehe Mosi Januari sambamba na kubeba mifuko ya taka mikononi mwao, huingia mitaani ambapo kwa kuhisi wadhifa wao wa kidini na kiraia, huanza kufanya usafi mitaani. Katika uwanja huo, Kalim Ahmad, mmoja wa vijana wa Kiislamu waliowahi kushiriki zoezi hilo mjini Cardiff anasema: "Mtume Muhammad (saw) ametufundisha kwamba usafi ni sehemu ya dini yetu. Sisi tunafanya kazi hii ikiwa ni katika kuwafundisha vijana wenzetu ni namna gani raia wanatakiwa kuwa." Naye kwa upande wake Amir Ahmad, kiongozi wa kampeni hiyo kwa vijana wa Kiislamu wa mji wa Leicester pia anasema: "Uislamu unawataka watu wote kushiriki katika kazi na vitendo vya kheri, kama ambavyo pia unasisitizia kumfanyia mtu mwingine wema hata kama utakuwa ni mdogo sana." Mwisho wa kunukuu. Farhad Ahmad, msemaji wa kampeni hiyo ya usafi anasema: "Kwa mtazamo wa kidini, usafi na kulinda jamii ambayo tunaishi ndani yake, ni sehemu muhimu ya dini yetu ya Uislamu." Mwisho wa kunukuu. Kampeni ya 'Siku ya Kusafisha Mitaa Nchini Kote' ni sehemu ya kampeni ya miaka mitano iliyopewa jina la 'Rehma kwa ajili ya Mwanadamu' na ambayo inajumuisha zoezi la upandaji miti kwa akali elfu 10 na kuendesha vikao elfu tano vya usafi mitaani. Kwa hatua hizo Waislamu wanakusudia kuiarifisha dini ya Uislamu barani Ulaya mkabala na propaganda chafu na ukatili dhidi ya Uislamu zinazofanywa na watu wenye chuki na ubaguzi kuihusu dini hii.


*******************


Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilicho hewani ni makala ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nchi za Magharibi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Waislamu nchini Marekani ambao wanaishi kwa wasi wasi na mashaka makubwa

Ndugu wasikilizaji dini ya Uislamu ni dini ya amani, upendo, uhuru na usafi. Katika dini hii ya Allah hakuna kitu kinachoitwa kulazimisha wala utumiaji mabavu na ukatili dhidi ya mtu mwingine. Na moja ya akhlaqi bora zaidi za dini ya Uislamu, ni imani ambayo hupatikana kwa njia ya kusoma na kutafakari mafundisho yake ya kuvutia. Mwislamu anaweza kutumia daraja ya imani na utambuzi wa kina wa mafundisho ya dini hiyo kuishi peke yake au na jamii kwa mujibu wa roho ya upole, amani, udugu na kusaidiana. Kwa hakika Uislamu wa namna hiyo ambao ni tofauti na ule unaoenezwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, hauwezi kuwa chanzo cha vitendo vya ugaidi, ukatili na kuchupa mipaka. Kinyume na Waislamu wa Uingereza na Wales ambao wamekuwa wakijitahidi kila mwaka mpya wa Miladia kufanya usafi katika mitaa na barabarani ambalo ni moja ya matukufu muhimu ya dini ya Uislamu yaani usafi,  Waislamu wa Austria waliuanza mwaka mpya wa Miladia 2018 kwa wasi wasi mkubwa juu ya mustakbali wao. Hii ni kwa kuwa, Waislamu wa Austria waliuanza mwaka huu katika mazingira ambayo chama cha mrengo wa kulia na chenye misimamo mikali ya chuki na ubaguzi dhidi ya wahajiri na Kiislamu, kiliungana na chama cha misimamo ya wastani kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.

Wanawake wa Kiislamu katika nchi za Magharibi

Ndugu wasikilizaji, chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi haishii tu katika kuibua mipaka, mashinikizo au kuongeza maudhi dhidi ya wafuasi wa dini hii ya mbinguni. Moja ya pande za chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi, ni kuibua anga ya chuki na wasi wasi baina ya Waislamu. Chuki na wasi wasi hiyo hutokana na  utendajikazi wa viongozi wa Magharibi na vyombo vya habari vya mataifa hayo. Kuingia madarakani chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo mikali katika serikali ya umoja wa kitaifa, husababisha anga ya wasi wasi kati ya walengwa kama ilivyo nchini Austria hivi sasa. Mjini Vienna kuna msikiti wa Shura ambao kila siku ya Ijumaa Waislamu wengi hukutana hapo kwa ajili ya kushiriki swala ya Ijumaa. Msikiti wa Shura, ni moja kati ya misikiti 300 na maeneo ya kuswalia Waislamu nchini Austria. Tangu mwaka 1912 ambapo dini ya Uislamu ilitambulika rasmi nchini humo, Waislamu wamekuwa na haki sawa kama ilivyo kwa wafuasi wa dini ya Ukristo na Uyahudi katika ibada na mambo mengine ya kijamii.

Waislamu katika nchi za Kimagharibi wanajitahidi kuuonyesha Uislamu kuwa ni dini ya amani

Hata hivyo hii leo misikiti kadhaa yakiwemo makao makuu ya Kiislamu mjini Vienna, imesalia kimya bila kutolewa adhana humo, hali ambayo inawafanya Waislamu kuhisi vibaya na kuwa wametengwa na kubaguliwa na serikali kuhusiana na masuala ya dini.


******************


Omar al-Rawi, mmoja wa Waislamu wa Baraza la mji la Vienna, anaelezea kimya hicho cha misikiti kwa kusema: "Waislamu hususan wahajiri mjini Vienna wamekuwa na wasi wasi mkubwa kufika misikitini siku hizi. Waislamu wanasema kuwa, hatwendi misikitini kwa kuwa tunaweza kudhaniwa kwamba sisi ni watu wenye misimamo ya kufurutu ada na magaidi. Ni kwa ajili hiyo ndio maana tunapendekeza kutokuswali swala ya jamaa hadi pale hali ya mambo kuhusu wahajiri itakapokuwa imetulia." Mwisho wa kunukuu. Waislamu nchini Austria hawafurahishwi na serikali mpya ya umoja wa kitaifa kwa kuwa vyama viwili vinavyounda serikali hiyo vyote kwa pamoja vina mtazamo hasi dhidi ya Waislamu hao.

Heinz Fassmann, Waziri mpya wa Elimu wa Austria

Hivi karibuni Heinz Fassmann, Waziri mpya wa Elimu wa Austria akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti moja la nchi hiyo alisema kuwa, walimu hawaruhusiwi kuvaa hijabu mashuleni. Fassman aliyasema hayo baada ya kuulizwa msimamo wake juu ya suala la hijabu na kuongeza:"Mimi ninaunga mkono nchi ya Kisekulari, na ninaamini kwamba walimu hawaruhusiwi kuvaa hijabu." Mwisho wa kunukuu.


**********************


Kwa  hakika mtazamo wa viongozi wa serikali mpya ya Austria juu ya mavazi na itikadi ya Waislamu kwa ujumla ni jambo ambalo limewapa wasi wasi mkubwa wafuasi wa dini hiyo ndani ya nchi hiyo. Kwa msingi huo, hivi sasa Waislamu wa nchi hiyo ni lazima wajiandae kukabiliana na maamuzi dhidi ya dini yao ambayo yanatazamiwa kutolewa wakati wowote na serikali ya sasa. Ibrahim Olegan kiongozi wa taasisi ya Kiislamu nchini humo akijibu matamshi ya Heinz Fassmann, Waziri mpya wa Elimu wa Austria kuhusiana na suala la hijabu kwa walimu anasema:

Wanawake Waislamu wanaojistiri huko katika nchi za Magharibi

"Hijabu ni mstari mwekundu kwa sisi Waislamu na kwa msingi huo hatuwezi kuruhusu kitu kama hicho na kila mtu anatakiwa kufanya juhudi kwa ajili ya kuzuia marufuku hiyo. Ikilazimu basi tutawasilisha malalamiko yetu mahakamani." Mwisho wa kunukuu.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 31 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./


 

 

 

 

Tags