Apr 03, 2018 13:39 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 32 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulimaliza kwa kukunukulieni kauli ya Ibrahim Olegan kiongozi wa taasisi ya Kiislamu nchini Austria akijibu matamshi ya Heinz Fassmann, Waziri mpya wa Elimu wa nchi hiyo aliyesema kuwa, walimu wa kike hawaruhusiwi kuvaa hijabu mashuleni.

Heinz Fassmann, Waziri mpya wa Elimu wa Austria mwenye chuki dhidi ya Waislamu

Olegan alimjibu Fassmann kwamba, hijabu ni mstari mwekundu kwa Waislamu na ikilazimu basi Waislamu wataenda hata mahakamani kutetea haki yao hiyo. Aliongeza kwa kusema: "Wawakilishi kutoka jamii ya Waislamu hivi karibuni watakutana na Waziri na kujadiliana naye kuhusu suala hilo. Tunadhani kwamba kile kilicho nyuma ya maamuzi ya Waziri katika kupiga marufuku vazi la hijabu ya Kiislamu ni chuki dhidi ya Uislamu. Ingawa hata hivyo kabla ya hapo Waislamu wa Austria waliwekewa pia mipaka mingi kupitia sheria zilizopitishwa na bunge la nchi hiyo dhidi yao." Mwisho wa kunukuu. Katika miezi ya hivi karibuni Austria imepitisha sheria ya kupiga marufuku vazi la hijabu. Kabla  ya kupitisha sheria hiyo pia, serikali ilipiga marufuku kupokea fedha za misaada yoyote kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuzisaidia taasisi za dini ya Kiislamu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo sheria kama hiyo haijawahi kutolewa kwa wafuasi wa dini nyingine kama vile Ukristo na Uyahudi.

****************

Farid Hafez, mwandishi na mtafiti wa nchini Austria ambaye pia ni mwanachama wa kitengo kinachojishughulisha na masuala ya kijamii na elimu ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Salzburg anasema: "Kwa sasa Waislamu wa Austria wanapitia wakati mgumu zaidi, kuliko kipindi kilichopita cha mwaka 2000 na 2005.

Watoto wa Kiislamu nchini Austria wakijifundisha Qur'an Tukufu

Hii ni kwa kuwa chama cha Uhuru na chama cha Wananchi hapo kabla na katika kipindi cha miaka ya 2000 na 2005, viliunda serikali ya muungano wa kitaifa. Mara hii ili chama cha Uhuru kiweze kupata mafanikio zaidi kimekuwa kikiwashambulia vikali Waislamu badala ya Mayahudi." Mwisho wa kunukuu. Itakumbukwa kuwa katika kipindi cha miaka hiyo chama cha mrengo wa kulia chenye kufurutu ada cha Uhuru kwa kuwakosoa Mayahudi, kilifanikiwa kuingia serikalini. Hata hivyo kitendo hicho cha kuwabagua Mayahudi kililaaniwa vikali na Umoja wa Ulaya kiasi cha kuufanya umoja huo kupitisha azimio la muda dhidi ya serikali ya Vienna kutokana na muamala huo wa chama cha Uhuru.  Hata hivyo hali ya mambo ilibadilika miaka kadhaa ya baadaye na sasa chama hicho chenye kufurutu ada kimekuwa na mahusiano ya karibu sana na magenge ya Kizayuni. Serikali ya Vienna inakanusha kwamba inawabagua Waislamu nchini humo na katika uwanja huo serikali hiyo inadai kwamba moja ya malengo yake ni kuongeza usalama nchini Austria sambamba na kuijumuisha jamii bora ya wahajiri na wakimbizi waliopo nchini pamoja na jamii ya watu wa taifa hilo. Kulazimisha kutumika lugha ya Kijerumani katika shule za Austria, ni moja ya hatua hizo.

Waislamu nchini Austria wakiandamana kutetea vazi lao la hijabu ambao linapigwa marufuku na serikali

Kuhusiana na suala hilo, Farid Hafez anasema tena kwamba: "Hiyo ni sehemu ya mchezo wa kibaguzi na ambao kimsingi hauna mahusiano na uhalisia wa maisha yetu, bali ni moja ya matamshi ya kibaguzi ambayo yanajaribu kuwanyima watu wasio na uraia wa Austria haki zao." Mwisho wa kunukuu.

*************

Tukitoka nchini Austria sasa tuelekee nchini Uingereza ambayo inadaiwa kuwa moja ya nchi zenye demokrasia na uhuru wa kidini duniani. Hata hivyo pamoja na hali hiyo kumekuwepo na habari za ubaguzi wa kidini ndani ya nchi hiyo. Ndugu wasikilizaji historia ya Waislamu wa mji wa Wales, Uingereza inarudi nyuma hadi karne 12 zilizopita. Waislamu elfu 46 ni sehemu ya jamii ya watu milioni tatu wa eneo hilo (Wales).

Waislamu nchini Uingereza wakijivunia dini yao ya Uislamu inayolingania upendo na amani

Kwa mahesabu halisi ni kwamba jumla ya Waislamu elfu 45,950 wanaishi eneo hilo ambapo kila wakazi 60, yupo Mwislamu mmoja. Aidha ni kwamba Waislamu wa eneo la Wales ni wachache ikilinganishwa na idadi ya Waislamu wanaoishi Uingereza yote, ambapo kati ya raia 20 wa taifa hilo, mtu mmoja ni Mwislamu. Kwa upande wa mji wa Cardiff, ambao ni makao makuu ya mji wa Wales, kati ya kila watu 14, mtu mmoja ni Mwislamu. Kadhalika nusu nzima ya Waislamu wa Wales wanaishi katika maeneo mabaya zaidi ambapo ni asilimia 1.7 tu kati yao ndio wanaoishi katika maeneo yenye hadhi. Kiwango cha ukosefu wa ajira katika eneo hilo kiko juu sana, kama ambavyo idadi ya watu wenye umri mkubwa nayo iko juu. Moja ya matatizo ya wanawake Waislamu wa mji wa Wales, ni kutokuwepo mlingano wa mahitaji na mazingira yao ya kazi na pia desturi za kifamilia. Kuhusiana na suala hilo, Daud Salman mwenye umri wa miaka 69 na ambaye miaka 27 iliyopita alikuwa kiongozi wa makao makuu ya Kiislamu mjini Cardiff anazungumzia mabadiliko yanayoikumba jamii ya Waislamu wa Wales, ambapo yeye mwenyewe anahisi kuwepo ongezeko la unyanyasaji dhidi ya Waislamu mjini hapo.

Wanawake wa Kiislamu waliojistiri, hukumbwa na matatizo mengi wawapo barabarani nchini Uingereza

Salman anasema: "Wanawake wa Kiislamu waliojisitiri kwa hijabu wakati wanapokuwa barabarani, huwa wanakumbwa na vitisho vingi dhidi yao. Hii ni katika hali ambayo wanawake wa Kiislamu hawana tatizo lolote kwa jamii hiyo." Mwisho wa kunukuu. Naye Bi Rahimah Zaman, mmoja wa wanawake wa Kiislamu anaelezea ubaguzi mkubwa anaoushuhudia kazini kwake na shuleni kwa binti yake mwenye umri wa miaka 12 kwa kusema: "Maneno ambayo huwa wanaambiwa wanafunzi wa Kiislamu shuleni ni yenye kutisha sana. Aghlabu hata huwa wanatupiwa vitu kama ambavyo pia huwa wanazomewa bila sababu yoyote. Hata hivyo wanafunzi hao wa Kiislamu hawawezi kujibu miamala hiyo na badala yake huwa wanalazimika kukaa kimya." Mwisho wa kunukuu.

*****************

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi kinachokujia kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji hadi sasa maelfu ya wanawake wa Kizungu nchini Uingereza wamejiunga na dini ya Uislamu. Kwa mfano tu mwaka 2010 pekee jumla ya wanawake laki moja walio na umri wa wastani wa miaka 28 walisilimu.

Wanawake wa Kiislamu barani Ulaya

Kuhusiana na suala hilo Bi Rahimah Zaman anabainisha chuki na ubaguzi unaowalenga wanawake hao walioamua kuwa Waislamu kwa kusema: "Ninawafahamu wanawake kadhaa Wazungu waliosilimu ambao kutokana na ubaguzi na maudhi wanayokabiliana nayo, waliamua kuondoka katika mji wa Cardiff. Licha ya kwamba ni Wazungu sawa na majirani wao wa Kizungu, hata hivyo kutokana na wao kuvaa hijabu, ndio wakawa wanakumbwa na vitisho na chuki dhidi yao kiasi cha kuwafanya wahame mji." Mwisho wa kunukuu. Naye kwa upande wake Amanda Moriss, mwanamke mwenye asili ya Canada na ambaye alisilimu akiwa na umri wa miaka 25 anazungumzia ongezeko la ubaguzi na chuki dhidi ya wanawake na wasichana wa Kiislamu kwa kusema: "Ninawafahamu wasichana kadhaa ambao waliposilimu waliamua kulifanya suala hilo kuwa siri sambamba na kuzificha familia zao kadhia hiyo. Hii ni kwa kuwa kama wazazi wao wangefahamu kuwa ni Waislamu, basi wangewafukuza nyumbani." Mwisho wa kunukuu.

Dini ya Uislamu inayolengwa na maadui kwa kila upande

Kadhalika Amanda anaelezea kupanuka chuki hiyo hata kwa wazazi kwa kusema: "Kuna mwalimu mmoja aliyeandaa programu ya kutembelea misikiti na mahekalu ya Kiyahudi. Hata hivyo jumla ya wazazi 30 walikataa kuwaruhusu watoto wao kutembelea misikiti kwa kile walichodai kwamba eti wanaweza kufundishwa ugaidi." Mwisho wa kunukuuu. Takwimu ya idara ya makazi ya mji wa Wales inaonyesha kwamba, jumla ya makosa 2941 yanayotokana na chuki dhidi ya Waislamu yalisajiliwa na polisi wa mji huo kati ya miaka ya 2016 na 2017. Tangu mwaka 2001 Waislamu wa Wales walianza kushuhudia maudhi na mashambulizi yanayosababishwa na chuki na ubaguzi dhidi yao. Ana Mayah, katibu mkuu wa msikiti wa Shah Jalal wa mjini Cardiff na ambao upo katika kitovu cha mizozo ya ubaguzi anasema: "Moja ya maudhi ambayo binafsi nimeyashuhudia, ni wakati ambao tulikuwa tunatoka msikitini ambapo mtu mmoja alipotuona alishuha kioo cha gari yake na kuanza kututusi.

Waislamu

Kwa hakika chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu ni suala ambalo limekuwa rasmi katika fasihi ya kisiasa na kijamii katika nchi za Ulaya." Mwisho wa kunukuu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 32 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

Tags