Apr 03, 2018 13:55 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 33 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia aina mbalimbali za hujuma na mashambulizi yanayowakumba Waislamu wa nchini Uingereza ambapo tulisema kuwa, ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu, vimekuwa rasmi katika fasihi ya kisiasa na kijamii katika nchi za Ulaya. Ndugu wasikilizaji, hata kama zamani viongozi wa nchi za Ulaya walikuwa hawadhihirishi mirengo yao iliyo dhidi ya dini ya Uislamu, lakini hivi sasa hawana kizuizi chochote katika kubainisha chuki yao kali dhidi ya dini hiyo na wafuasi wake.

Viktor Orbán Waziri Mkuu wa chama cha mrengo wa kulia na chenye misimamo mikali nchini Hungary

Katika uwanja huo, Viktor Orbán Waziri Mkuu wa chama cha mrengo wa kulia na chenye misimamo mikali nchini Hungary mwanzoni mwa mwaka huu wa 2018 alitoa matamshi mapya ya chuki katika kupinga kupokelewa barani Ulaya wahajiri ambapo alisema: “Sisi hatuwatambui watu hao kama ni Waislamu pekee, bali tunawahesabu kuwa ni wavamizi wa Kiislamu dhidi ya nchi zetu.” Mwisho wa kunukuu. Kwa imani ya Viktor Orbán, wahajiri na wakimbizi, ni wahujumu uchumi ambao wanatafuta maisha mazuri ndani ya mataifa hayo ya Ulaya. Akifafanua kuwa Ulaya inaundwa na jamii yenye tamaduni tofauti anasema: “Kuingia Waislamu ndani ya nchi hizo kutapelekea kuundwa jamii ya aina moja, (yaani jamii ya Kiislamu pekee) na Hungary haikubali suala hilo na hakuna sababu ya kutokea kwake.” Mwisho wa kunukuu.

******************

Ndugu wasikilizaji, chuki dhidi ya wahajiri na wakimbizi katika nchi nyingi za Ulaya imeunganishwa na chuki dhidi ya Uislamu. Hii ni kusema kuwa, makundi yanayoendesha kampeni za chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya na kwa kisingizio cha kuathiri uchumi, tamaduni na muundo wa kijamii wa mataifa hayo kutokana na uwepo wa wahajiri, yanakusudia kuwawekea mashinikizo na vikwazo chungu nzima Waislamu wanaoishi nchi hizo. Mmoja wa wanasiasa maarufu wanaofanya kampeni za chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya ni Miloš Zeman, Rais wa Jamhuri ya Czech.

Miloš Zeman, Rais wa Jamhuri ya Czech.

Zeman amepata umaarufu kutokana na hatua yake ya kupinga Waislamu na wahajiri kuingia Ulaya Mashariki. Aidha Zeman ni mwenye chuki kali dhidi ya dini ya Uislamu ambapo hata aliutaja mgogoro wa uhajiri mwaka 2015 kuwa ni ‘uvamizi ulioratibiwa dhidi ya Ulaya’ huku akisisitiza kwamba, ni suala lisilowezekana kuwajumuisha Waislamu katika jamii ya Ulaya. Itakumbukwa kuwa, Jamhuri ya Czech ni miongoni mwa nchi za Ulaya ambazo, makundi ya mrengo wa kulia na yenye kufurutu ada katika ulingo wa kisiasa yamekuwa na nafasi athirifu zaidi. Katika uwanja huo katikati ya mwezi Disemba uliopita mji wa Prague, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa mrengo wa kulia na wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na uhajiri kutoka nchi tisa za Ulaya. Viongozi hao wanatumia fursa iliyopo kuratibu mpango wao dhidi ya dini ya Uislamu kwa kuufanya kuwa nara ya kufanikisha kupitishwa sheria kali ya kuwabana Waislamu wanaoishi nchi hizo. Hank Wendoun, mkuu wa kampeni ya uchaguzi wa chama kinachoongoza chuki dhidi ya Uislamu cha ‘Uhuru’ nchini Uholanzi, hivi karibuni alinukuliwa akitoa maneno ya kutaka kuchomwa moto misikiti yote ya nchi hiyo. Kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, ni kwamba chama hicho cha Uhuru kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa bunge mwaka jana.

Wanawake Waislamu barani Ulaya wanatetea vazi lao la hijabu

Kiongozi mkuu wa chama hicho chenye misimamo ya kigaidi dhidi ya Waislamu ni, Geert Wilders ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na kuwa na chuki kali dhidi ya dini hii ya mbinguni. Katika mahojiano ya redio moja nchini Uholanzi, Hank Wendoun, alisema kuwa anapendekeza kuchomwa moto misikiti yote ndani ya taifa hilo. Wakati mwendesha kipindi alipomuulia kama yupo tayari kurekebisha meneno yake, alisema kuwa ‘binafsi anapinga uwepo wa misikiti nchini humo na anatumai kuona misikiti hiyo ikipigwa kufuli ndani ya nchi hiyo.’

*******************

Tunaweza kusema kuwa, hakuna nchi hata moja barani Ulaya ambayo haishuhudii ubaguzi wa kutisha dhidi ya dini ya Kiislamu na wafuasi wake.

Kiongozi mkuu wa chama chenye misimamo ya kigaidi dhidi ya Waislamu Geert Wilders.

Luxembourg ni nchi ndogo na iliyoendelea barani Ulaya. Ndani ya nchi hiyo ambayo ni mara chache sana kutajwa jina lake hadi kunapofanyika kikao cha viongozi wa Umoja wa Ulaya, Waislamu pia wanashuhudia mienendo ya ubaguzi dhidi yao. Kufuatia hali hiyo jamii ya Waislamu wa nchi hiyo na katika kupambana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu, iliamua kuanzisha kituo ambacho lengo lake ni kufuatilia na kukusanya ripoti, matukio na nyaraka muhimu zinazohusiana na chuki na ubaguzi dhidi yao. Kituo hicho cha ufuatiliaji matukio ya ubaguzi dhidi ya Uislamu na ambacho kiko chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kiutamaduni nchini Luxembourg kilifunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu. Aidha kituo hicho kiliasisiwa na Mwislamu mmoja ambaye yeye, mke na rafiki yake walikumbwa na hujuma ya chuki dhidi ya Uislamu, ambapo baada ya hapo waliamua kuasisi kituo hicho ili kukusanya matukio na taarifa zote zinazohusiana na wimbi hilo la kigaidi dhidi yao nchini humo.

Waislamu nchini Luxembourg

Kwa mujibu wa msimamizi wa kituo hicho, wajumbe wa kundi la watu wanne ambao ndio walioasisi kituo hicho, walitaka kusalia bila kufahamika majina yao, kwani kama wangetambuliwa na vyombo vya habari, basi nao wangejikuta ni wahanga wa chuki dhidi ya Uislamu nchini humo. Mmoja wa waasisi wa kituo hicho anasema: "Binafsi nimepata tajriba mara kadhaa ya hujuma za chuki dhidi ya Uislamu ambapo, mimi, mke na rafiki yangu kwa ujumla tulikumbwa moja kwa moja na shambulizi lililosababishwa na chuki dhidi ya Uislamu. Ninafahamu wadhifa wangu kwamba ni kuwalinda Waislamu wenzangu." Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa tathmini za hivi karibuni hadi sasa Luxembourg ina Waislamu elfu 10 hadi 15.

*****************

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hii ikiwa ni sehemu ya 33. Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema, mwaka 2018 ulianza na wasi wasi mkubwa kwa Waislamu wa Austria. Katika uwanja huo televisheni ya Euro News ilitoa ripoti juu ya vitendo vya chuki kuwalenga Waislamu kutokana na serikali mpya ya umoja wa kitaifa nchini humo.

Mwanamke wa Kiislamu nchini Luxembourg

Ripoti hiyo ilieleza kwamba katika mipango na ratiba za serikali hiyo mpya, Uislamu umetajwa mara 21 hususan katika uga wa kiusalama. Serikali ya umoja wa kitaifa nchini Austria inaundwa na wahafidhina na wale wa mrengo wa kulia wenye kufurutu ada. Kaulimbiu ya serikali hiyo ni 'Mshikamano kwa ajili ya Austria Yetu', huku ikiwa pia na baadhi ya ibara zinazoonyesha kwamba Uislamu ni dini ya kufurutu ada. Mwaka 2017 ulikuwa mwaka ambao vyama vya mrengo wa kulia na vyenye chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya vilifanikiwa kuzivutia fikra za walio wengi. Hata nchini Austria mrengo huo wa kufurutu ada ulifanikiwa pia kuingia serikalini. Chama cha Uhuru cha mrengo wa kulia na chenye siasa kali na kile cha Wananchi kinachoongozwa na Sebastian Kurz, kwa pamoja vilikubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Sebastian Kurz, alipowahi kukutana na Waislamu wakati akihudumu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Austria

Hivi sasa vyama hivyo vinadhihirisha siasa zao hususan kuhusiana na suala la uhajiri na kutaka kuanzishwa mashinikizo na mibinyo zaidi dhidi ya Waislamu. Mienendo hiyo ndio imewafanya Waislamu wa Austria kupatwa na wasi wasi zaidi, hasa kutokana na wao kunyooshewa kidole kwamba ni tishio dhidi ya usalama wa taifa na kijamii nchini humo. Hii ni katika hali ambayo Austria sio kama Ufaransa au Uingereza, ambazo zilishuhudia mashambulizi ya kigaidi miaka miwili iliyopita. Kwa mujibu wa takwimu, katika miaka ya hivi karibuni Austria haijashuhudia hujuma kama hizo kiasi cha kufikia kuwataja Waislamu kuwa ni hatari kwa usalama wa kitaifa. Katika hali hiyo Waislamu wa nchi hiyo wanaendelea kukabiliwa na aina mbalimbali za ubaguzi na chuki dhidi yao.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 33 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags