Ulimwengu wa Michezo, Apr 23
Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita......
Voliboli ya Walemavu: Iran yatamba mjini Tabriz
Timu ya taifa ya voliboli ya kuketi chini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza kwa kishindo Mashindano ya Dunia ya Voliboli ya Walemavu yanayofanyika katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Timu hiyo imepata ushindi mkubwa katika mechi zake nne za kwanza, ambapo katika mchuano wa Jumapili, iliilaza Ujerumani seti 3-0. Kabla ya hapo timu hiyo ya Iran iliibamiza Ukraine pia seti 3-0 za (25-14, 25-18 na 25-18) katika mchezo uliopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Sadra mjini Tabriz siku ya Jumamosi. Siku ya Ijumaa jioni, wanamichezo hao wa Kiirani walipata ushindi wa pili katika mashindano hayo ya kimataifa yajulikanayo kwa Kimombo kama World Para Volley Men's World Super 6 Sitting Volleyball Competition baada ya kuisasambua Bosnia, siku moja kabla ya kuibamiza Russia seti 3-0 za (25-22, 25-20 na 25-17). Mashindano hayo ya dunia ya voliboli ya kuketi chini yalianza Aprili 19 na yatanazamiwa kumalizika Jumanne hii ya Aprili 24. Iran ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo.
Droo ya Kombe Shirikisho, Afrika Mashariki yatamba
Shirikisho la Soka Afrika CAF siku ya Jumamosi lilichezesha droo ya Kombe la CAF na kupanga makundi manne yatakayowania taji hilo zikiwemo klabu za kanda ya Afrika Mashariki. Klabu ya Yanga ya Tanzania imepangwa katika Kundi D lenye timu za Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sports ya Rwanda na USM Alger ya Algeria. Timu zitakazopeta katika hatua hii ya makundi zitatinga robo fainali. Timu nyingine ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Al Hilal ya Sudan imeangukia katika Kundi B lenye timu za Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco, El Masry ya Misri na Desportivo do Songo ya Msumbiji. Aidha, kundi A kuna timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Raja Club Athletic ya Morocco, AS Vita ya Kongo DR na Aduana Stars ya Ghana.
Kwenye kundi C kuna timu za Enyimba ya Nigeria, Williamsville ya Ivory Coast, Club Athletic Renaissance ya Congo na Djoliba AC Bamako ya Mali. Klabu hizo zimetinga mzima mzima hatua ya makundi ya kuwania Taji la Shirikisho la Soka barani Afrika baada ya michuano ya muondoano kumalizika siku ya Alkhamisi. Licha ya kufungwa bao 1-0 na Welayta Dicha ya Ethiopia, ushindi wa Yanga wa mabao 2-0 nyumbani uliwasaidia kufuzu katika hatua hiyo. Yanga imefuzu hatua hiyo kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kushinda 2-0 nyumbani na kisha kufungwa bao 1-0 mjini Awasa, Ethiopia dhidi ya wenyeji wao, Welayta Dicha. Kocha na wachezaji wa klabu hiyo ya Tanzania wamepokea vizuri hatua ya kujikatia tiketi ya kushiriki mechi za makundi licha ya kulazwa bao moja bila jibu ugenini.
Nayo Gor Mahia ya Kenya ambayo imeweka historia kwa kufuzu katika hatua hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 31 iliposhinda taji la Afrika, licha ya kufungwa na SuperSport United mabao 2-1 ugenini, ushindi wao wa bao 1-0 hapo awali uliwasaidia. Licha ya kuwa mashabiki wa Kogalo kama wanavojulikana nyumbani kuwa na matarajio hapo awali kwamba klabu yao angelifunga mabao mengi zaidi, lakini wanasema hawajakata tamaa, na wanatazamia kung'ara zaidi katika mechi zijazo za Kombe la Shirikisho.
Mambo yalikuwa mazuri pia kwa Rayon Sport ya Rwanda ambayo licha ya kupoteza kwa mabao 2-0 baada ya kufungwa na Costa do Sol ya Msumbiji, ushindi wake wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ulitosha kuwapaisha. Kwa mujibu wa CAF, mechi za raundi ya kwanza zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao wa Mei.
Kenya yatamalaki London Marathon
Mwanariadha nyota wa Kenya Eliud Kipchoge ameibuka kidedea katika mbio za London Marathon mwaka huu 2018. Hii ni mara ya tatu kwa mwanariadha huyo bingwa kuibuka mshindi. Katika mashindano hayo siku ya Jumapili katika mji mkuu wa Uingereza, London uliokuwa ukishuhudia jua la utosini, Kipchoge ambaye alianza vyema mbio hizo alimaliza kwa kutumia muda wa saa mbili dakika nne na sekunde 27.
Mwenyeji Mo Farah alikuwa akiongoza mwanzoni mwa mbio hizo za kilomita 42 kabla ya kupoteza mwelekeo na kumaliza katika nafasi ya tatu, dakika tano nyuma ya Kipchoge. Mwanariadha kutoka nchini Ethiopia Tola Shura Kitata amemaliza katika nafasi ya pili akiwa nyuma kwa sekunde 33 dhidi ya Kipchoge. Mwanadada Vivian Cheruiyot wa Kenya ameshinda kwa upande wa wanawake kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika 18 na sekunde 31. Amesema ushindi huo umemridhisha kwani alikuwa anakimbia kwa kasi yake mwenyewe. Wanariadha zaidi ya 40,000 walishiriki katika mashindano hayo ya London Marathon katika kipindi hiki msimu wa joto kali nchini humo.
Hatimaye Wenger akubali kuondoka Arsenal
Wanasema hayawi hayawi hatimaye huwa. Ndio msemo unaoonekana kupata maana wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule, tukijerejelea habari ya meneja wa zaidi ya miongoni miwili wa klabu ya Uingereza ya Arsenal, Arsene Wenger kukubali kuipungia mkono timu hiyo. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Wenger amesema: "Baada ya kutafakari na kufanya mazungumzo na klabu, nahisi ni wakati muafaka kujiuzulu mwisho wa msimu huu. Nashukuru kwa kupata fursa ya kuihudumia klabu hii kwa miaka mingi. Niliongoza klabu hii na moyo wangu wote pamoja na maadili. Nataka kuwashukuru wafanyikazi, wachezaji Mkurugenzi na mashabiki ambao wameifanya klabu hii kuwa ya kipekee. Naipenda klabu hii na nitaishabikia maisha yangu yote.'' Wenger anaacha nyuma ya historia ya asali-chungu miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo yenye mamilioni ya wafuasi kutoka pembe mbalimbali za dunia. Mashabaki wa Gunners Afrika Mashariki wana maoni tofauti kuhusiana na kadhia hiyo ya kujiuzulu au kuuzuliwa Wenger.
Kabla hajatua Arsenal mwaka 1996, Wenger alikuwa akiifunza klabu ya Monaco inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa na baada ya kutua jijini London, alifanikiwa kushinda mataji mawili ya ligi mfululizo na vile vile FA. Tangu msimu wa 2003/04 alipokiongoza kikosi chake cha enzi hizo kutwaa ubingwa wa ligi bila ya kupoteza mechi, imekuwa ni miaka 10 sasa bila yake kushinda kombe hilo la ligi kuu ya EPL. Miongoni mwa majina yanayotajwa kuwa yumkini yatarithi mikoba ya Wenger ni mkufunzi wa zamani wa Barcelona Luis Enrique, mwenye umri wa miaka 47, Mkufunzi wa Ujerumani Germany Joachim Low, mkufunzi wa Juventus Max Allegri, kocha wa Monaco Leonardo Jardim na Brendan Rodgers anayeinoa klabu ya Celtic. Mkufunzi wa zamani wa Chelsea Carlo Ancelotti, 58, amesema kuwa atakubali ombi kutoka kwa Arsenal. Vijana wa Arsenal siku ya Jumapili walianza kumuaga kwa namna yake Wenger, kwa kuisasambua West Ham mabao 4-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Mabao ya Gunners yalipachikwa kimyani na Nacho Monreal, Aaron Ramsey huku Mfaransa Alexandre Lacazette akifunga mawili katika dakika za lala salama. Hata hivyo licha ya ushindi huo Arsenal walisikitishwa na kitendo cha kupigwa kiatu mchezaji wake wa safu ya kati, Mohammed Elneny ambaye alilazimika kutolewa uwanjani kwa machela. Raia huyo wa Misri amepata majeraha mabaya ikiwa ni chini ya miezi miwili kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia nchini Russia, ambapo Mafarao ni miongoni mwa nchi chache zinazoliwakilisha bara Afrika katika michuano hiyo.
……………………………TAMATI…………………….