Jumapili, Mei 20, 2018
Leo ni Jumapili tarehe nne Ramadhan mwaka 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 20 Mei mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 863 iliyopita, alifariki dunia, Ibn Khorasani, msomi mkubwa wa elimu ya nahau, malenga na mwandishi wa mjini Baghdad, Iraq. Ibn Khorasani alizaliwa mwaka 494 Hijiria mjini Khorasan, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo alielekea Baghdad, lraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa mjini hapo alifanikiwa kuhitimu masomo yake kwa maulama wakubwa wa zama hizo. Alikuwa na utaalamu mwingi wa elimu tofauti hususan katika fani ya lugha ya Kiarabu na mashairi.

Siku kama ya leo miaka 831 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim, Hibatullah bin Jaafar aliyepewa lakabu ya Qadhi Said Ibn Sinaul-Mulk, malenga na mtaalamu wa fasihi wa Misri. Abul-Qasim aliyekuwa akiitwa kwa jina la babu yake Sinaul-Mulk, alizaliwa mjini Cairo mwaka 545 Hijiria katika familia ya Kiislamu. Alisoma mjini Alexandria elimu ya Qur’ani, nahw, hadithi na elimu nyingine kutoka kwa wasomi wakubwa wa mji huo. Akiwa kijana alifikia daraja ya juu katika uwanja wa mashairi na lugha na kuanza kusoma mashairi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na mashairi yaliyobeba madhumuni tofauti, miongoni mwayo yakiwa ni kuhusu tukio chungu la Ashura na mauaji ya kidhulma ya Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mwanauchumi wa Uingereza. Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja. Vitabu muhimu vya mwanauchumi huyo wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy" na "Principals of Political Science". Mill aliaga dunia mwaka 1873.

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita jamhuri huru ilitangazwa huko Cuba na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492 Miladia, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba.

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita Yemen ilipata pigo mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta'if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizan na Asir kwa muda wa miaka 40. Wakati wa kugawika Yemen katika pande mbili, yaani kaskazini na kusini na kwa kuzingatia kuwa upande wa kaskazini ulikuwa ukipambana na upande wa kusini ambao ulikuwa ukipata uungaji mkono kutoka kwa Saudia, hivyo ule wa kaskazini ulishindwa kufuatilia kadhia ya maeneo yake hayo. Hata hivyo baada ya maeneo ya kusini na kaskazini kuungana mwaka 1990, Yemen ilianza kufuatilia maeneo hayo ya Najran, Jizan na Asir yenye utajiri wa mafuta. Aidha Saudia ilianzisha vita vipya dhidi ya Yemen mwezi April 2015 kwa ajili ya kuyadhibiti zaidi maeneo hayo.

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita mnamo tarehe 20 mwezi Mei mwaka 1960, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilitangaza kupata uhuru wake chini ya mfumo wa jamhuri na siku kama hii hujulikana kama siku ya taifa nchini humo. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Cameroon kwa miaka kadhaa ilikoloniwa na Ufaransa na Uingereza na mwaka 1946 Miladia, Umoja wa Mataifa ukaziweka chini ya mamlaka yake ardhi zote za nchi hiyo. Hata hivyo katika mwaka 1959 Miladia, udhibiti huo uliondolewa na mwaka mmoja baadaye Cameroon ikatangaza uhuru wake kwa jina la Jamhuri ya Cameroon. Kufuatia kutangazwa kuwa huru nchi hiyo, katiba ya Cameroon ikapasishwa kupitia kura ya maoni na nchi hiyo ikakubaliwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita yaani tarehe 30 Ordibehesht mwaka 1361 Hijria Shamshia, marhumu Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani mmoja wa shakhsia muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Spika wa Bunge la Iran wakati huo, alitoa pendekezo la kuundwa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad. Awali fikra hiyo ilitolewa katika Jumuiya Kiislamu ya Vyuo Vikuu. Baadaye pendekezo hilo liliwasilishwa kwa Imam Khomeini, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye aliliunga mkono na kutoa kiwango fulani cha fedha kama msaada kwa Chuo Kikuu hicho. Hii leo Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad ndicho Chuo Kikuu kikubwa zaidi kisicho cha kiserikali nchini Iran.

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.
