Apr 06, 2016 11:42 UTC
  • Familia Salama (1) Usalama wa Chakula

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu mpya wa makala kuhusu Afya ya Familia. Makala hizi zitaangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala yetu ya kwanza tutaangazia nafasi ya usalama wa chakula katika afya ya familia.

Hitajio la mwanadamu kwa chakula ni kati ya mahitajio yake muhimu zaidi ambayo huambatana naye kutoka wakati wa kuzaliwa hadi kuaga dunia.

Kiwango cha afya, kustawi kimwili na kiakili, utulivu wa kiroho, kupata uwezo na nguvu, kuongeza kizazi n.k yote hayo kwa njia moja au nyingine yanategemea afya bora na usalama wa chakula.

Tukisema usalama wa chakula tunakusudia kuwa, watu wote katika jamii waweze kupata chakula cha kutosha na katika kipindi chote cha umri. Usalama wa chakula huweza kudhaminiwa wakati kikapu cha chakula cha kila mwaka cha familia kinapodhaminiwa na kutayarishwa kwa njia sahihi ili kufaidi mwili mzima. Mbali na usalama wa chakula yaani mtu kuhakikishiwa kuwepo mlo au chakula suala jingine muhimu pia ni kiwango cha ubora wa kiafya wa chakula hicho. Ubora wa kiafya wa chakula kimsingi ni kuwa chakula kinacholiwa kisiwe na aina yoyote ya uchafu unaoonekana au usioonekana kwa macho ya kawaida. Hii ni kwa sababu kwa mfano kidhahiri kinaweza kuwa safi lakini kikawa na vijidudu au kemikali ambazo haziwezi kutambuliwa isipokuwa na wataalamu au katika maabara.

Utafiti wa kisayansi umebaini kuwa, katika miongo ya hivi karibuni sambamba na kustawi teknolojia na ongezeko la utumizi wa virutubisho katika vyakula na pia utumizi wa dawa za antibiotiki (viuaji sumu) na viuadudu au pesticides n.k katika uzalishaji chakula iwe ni katika mashamba au viwandani ni mambo ambayo yamekuwa na taathira hasi katika afya ya mwanadamu. Kemikali hizo zinazotumika katika viwanda au mashambani kuzalisha vyakula hupelekea mwanadamu kukumbwa na matatizo mengi kama vile saratani hasa miongoni mwa watoto na wazee. Kwa mujibu wa takwimu, kiwango cha maradhi yanayotokana na chakula chenye aina kadhaa za kemikali katika nchi zinazostawi ni asilimia 13 zaidi ya nchi zilizostawi.

Kwa mtazamo wa wataalamu wa lishe, vyakula visivyo salama na vyenye vijidudu yamkini vikasababisha matatizo ya kiafya kama vile kuharisha, kuenea vijidudu mwilini na pia kusababisha kudorora ustawi wa kimwili wa watoto, kuzuia uzazi na kusababisha saratani.

Wataalamu wa lishe wanataja nukta au kanuni kadhaa muhimu za kuhakikisha chakula ni salama kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu.

Awali ni usafi jikoni au sehemu ya kupikia chakula. Kati ya nukta muhimu za kutunza usafi ni kusafisha mikono kabla ya kushika vyakula. Kusafisha mikono mara kwa mara wakati unapotayarisha vyakula. Kusafisha mikono baada ya kutoka chooni na kusafisha vyombo ulivyotumia wakati wa kutayarisha chakula. Ni muhimu pia kulinda sehemu ya jiko na chakula dhidi ya wanyama haribifu. Sababu ya usafi jikoni ni kuwa, licha ya kuwa vimelea (parasites) vingi havileti magonjwa, kuna vimelea ambavyo husababisha magonjwa, vimelea vyenye kuleta athari mbaya za kiafya hupatikana kwa wingi katika udongo, maji , katika wanyama na binadamu. Vijidudu hivyo huwepo kwenye mikono na vitambaa vya kusafishia vyombo vya chakula. Kwa mfano ubao wa kukatia nyama ukichafuliwa unaweza kuchafua chakula na kusababisha magonjwa yanayotokana na chakula.

Kanuni nyingine muhimu ya kuhakikisha chakula ni salama ni kutenganisha chakula kilichopikwa na chakula kibichi.

Ni muhimu hasa kutenganisha nyama na samaki na vyakula vingine. Hali kadhalika ni muhimu kutumia vyombo tofauti kwa chakula kibichi na kilichopikwa. Aidha wataalamu wanasisitiza kuhusu kuhifadhi chakula kilichopikwa mahala pasafi na kuhakikisha hakichanganyiki na chakula kibichi. Hii ni kwa sababu vyakula vibichi, hasa aina ya nyama na mchuzi wake, vinaweza kuwa na vijidudu hata ambavyo vinaweza kuchafua vyakula wakati wa maandalizi. Kanuni nyingine ya kuhakikisha chakula ni salama ni kukipika mpaka kiive.

Wataalamu wanasema chakula kinapasa kupikwa hadi kiive hasa nyama, mayai na samaki. Shirika la Afya Duniani WHO linapendekeza kuwa vyakula kama supu na mchuzi unapasa kupikwa hadi nyuzi joto 70. Kwa vyakula aina ya nyama inapendekezwa kuhakikisha kuwa mchuzi hauna rangi ya pinki. Unashauriwa kutumia kipima joto ili kuweza kutambua ikiwa joto limefikiwa. Halikadhalika wataalamu wa lishe wanasema viporo vichemke kwa zaidi ya dakika tano. Hii ni kwa sababu upikaji mzuri wa chakula unaweza kuua vimelea hatarishi. Tafiti zimeonyesha kwamba chakula kilichopikwa kwenye nyuzi joto 70 ni salama. Vyakula vinayohitaji uangalizi wa kipekee ni pamoja na nyama ya kusaga, kababu, mapande ya nyama na kuku wazima.

Kanuni nyingine ya chakula salama ni kuhifadhi chakula kilichopikwa kwa uangalifu. Wataalamu wa lishe wanashauri kuwa usihifadhi chakula kilichopikwa katika joto la kawaida kwa zaidi ya saa mbili. Ikiwezekana hifadhi chakula katika sehemu baridi kama vile friji au jokovu vyakula vilivyopikwa na kupoozwa na pia vyakula ambavyo vinaharibika katika kipindi kifupi.

Joto linalofaa katika kuhifadhi chakula liwe na nyuzi joto chini ya 5. Hali kadhalika inashauriwa kuwa chakula kiliwe mara baada ya kupikwa. Nukta nyingine muhimu ni kuwa chakula kilichopikwa kisihifadhiwe kwa kipindi kirefu hata kama kitakuwa kimewekwa kwenye friji.

Nukta ya mwisho kuhusu chakula salama ni kutumia maji na malighafi safi. Iwapo una shaka na usafi wa maji hata yale ya mfereji, njia rahisi zaidi ya kuyafanya yawe salama kutumia ni kuyachemsha. Halikadhalika maziwa pia huweza kuwa salama baada ya kuchemshwa.

Aidha ni jambo la dhaura kuosha matunda na mboga za majani kwa maji salama. Nukta nyingine ya kudumisha afya ni kujiepusha kula vyakula vilivyomalizika muda wake wa matumizi.

Sababu ya kuzingatia nukta hizo ni kuwa, vyakula vibichi, maji na barafu, vinaweza kuingiwa na vijidudu hatari au kemikali. Hatua za kawaida za kuvisafisha vyakula na kuvimenya inapowezekana hupunguza athari mbaya za kiafya zinazotokana na matumizi mabaya ya vyakula hivyo.

Tunakomea hapa kwa leo wapenzi wasikilizaji, katika makala yetu ijayo tutazugumzia lishe ya mwanadamu.


Tags