Jun 30, 2018 09:02 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (58)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 58.

Tukiendelea na maudhui yetu ya kujadili mchango chanya ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa wakati wa uenyekiti wake katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, ni kwamba, katika kadhia ya Palestina, na kwa kuzingatia uzito wa suala hilo, hatua za kujitanua, kandamizi na za kigaidi za utawala wa Kizayuni zililaaniwa vikali katika kipindi hicho. Vile vile kwa kutilia maanani kwamba katika kipindi hicho Israel iliendeleza sera za ujenzi wa vitongoji na suala hilo kuzusha wasiwasi mkubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu, Iran ilitekeleza diplomasia amilifu na makini ya kutumia uwezo wa nchi za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika kipindi cha uenyekiti wake wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitumia, kwanza fursa hiyo kuzitangaza kwa uwazi zaidi kwa walimwengu hatua za kinyama za utawala wa Kizayuni; na pili iliuwekea mbinyo na mashinikizo utawala huo na kuwaonyesha viongozi wake kwamba Ulimwengu wa Kiislamu unaguswa na kutoneshwa mno na kadhia ya Palestina. Katika kipindi hicho aidha, ilifanya jitihada nyingi kwa lengo la kutatua migogoro ya Ulimwengu wa Kiislamu katika nchi za Lebanon, Iraq, Afghanistan, Kosovo na Chechnya na kuweza kuandaa mazingira muafaka ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na kupatikana sauti moja baina ya nchi wanachama wa OIC.

 

Kikao cha Tehran kilikuwa na mafanikio mengi ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa Umma wa Kiislamu na kwa maana hiyo kwa Jumuiya yenyewe ya nchi za Kiislamu pia. Kwa upande wa kisiasa, mbali na kupatikana mafanikio muhimu ya kuwepo sauti moja ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu ya kukabiliana na nadharia ya Mpambano wa Staarabu na kupokelewa nadharia ya Mazungumzo Baina ya Staarabu, yalipatikana pia mafanikio mengine ya kisiasa kama kujengwa hali ya kuaminiana kati ya nchi wanachama wa OIC na kuanzishwa uhusiano kati ya Jumuiya hiyo na Jumuiya za Kimataifa kama Umoja wa Mataifa na ECO na maazimio kadhaa yakapitishwa kuhusiana na masuala hayo. Umoja wa mabunge ya nchi za Kiislamu ni maudhui nyengine iliyofuatiliwa katika kikao cha Tehran. Kwa upande wa kiuchumi pia yalipitishwa maazimio mawili yaliyokuwa na umuhimu mkubwa zaidi kuliko mengine. Moja ni azimio la kuasisi soko la pamoja la Kiislamu na jengine ni kuuandaa na kuuweka tayari Umma wa Kiislamu kwa ajili ya kuingia katika karne mpya ya 21. Na kwa upande wa kiutamaduni pia kulikuwa na matunda kadhaa yaliyopatikana ikiwemo kufanyika kikao cha Waislamu walio jamii za wachache katika nchi nyengine pamoja na kuandaa kalenda ya pamoja ya mwandamo wa mwezi na Sikukuu za Kiislamu na kuandaa kamati ya Kiislamu ya uratibu wa hatua za pamoja, ambayo ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa ajili ya kupatikana sauti moja na kuwepo muelekeo mmoja katika Umma wa Kiislamu.

Mwenendo chanya wa matukio ya kuleta mshikamano, muelekeo mmoja na sauti moja baina ya nchi wanachama wa OIC uliendelea pia baada ya kikao cha Tehran. Wakati wa tukio la Septemba 11 mwaka 2001 na kushambuliwa majengo pacha katika mji wa NewYork, Marekani, japokuwa tukio hilo liliibua uhasama na uadui usio na sababu dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu, lakini kwa namna fulani lilipelekea pia kupatikana umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Kwa mfano wakati Marekani ilipozidisha vitisho vya kuishambulia kijeshi Iraq, mnamo tarehe 5 Machi mwaka 2003 yaani takribani mwezi mmoja kabla ya Marekani kuishambulia kijeshi nchi hiyo, Jumuiya ya OIC ilifanya kikao cha dharura, ambapo katika kikao hicho nchi wanachama zilipinga na kulaani hatua yoyote ya kutaka kuishambulia kijeshi Iraq na kusisitiza kuungwa mkono amani na usalama wa nchi hiyo. Nchi hizo aidha zilitangaza kuwa haipasi nchi yoyote mwanachama wa OIC kushiriki katika uvamizi uliopangwa kufanywa dhidi ya Iraq. Msimamo huo ulionyesha kwamba hata katika hali mbaya kabisa na ya uwepo wa fikra mseto ndani ya OIC, nchi za Kiislamu zinaweza kudumisha mshikamano baina yao na kuwa na msimamo wa aina moja katika masuala ya maslahi yao ya pamoja na katika kukabiliana na adui wa pamoja wa Umma wao.

 

Hali iliyokuwa imetawala zaidi katika kipindi hicho ambacho kilianzia mwaka 1997 katika mkutano wa Tehran hadi lilipoibuka vuguvugu la Umma wa Waislamu katika nchi nyingi za Kiarabu baina ya mwaka 2011 na 2012 ilikuwa ni kuwepo muelekeo na sauti moja kati ya nchi za Kiislamu. Jumla ya mikutano sita katika ngazi ya viongozi wa nchi wanachama na vikao viwili vya dharura vilifanyika katika kipindi hicho. Katika mkutano wa tisa uliofanyika mwaka 2000 nchini Qatar mbali na kutangazwa msimamo wa pamoja wa kukabiliana na hatua za kujitanua za utawala wa Kizayuni, nchi wanachama zilitoa mkono wa pongezi pia kwa taifa la Lebanon kwa kukabiliana na uchokozi wa Israel. Katika vikao vya OIC vilivyofuatia pia, ambavyo vilifanyika katika nchi za Saudi Arabia, Malaysia na Senegal nchi wanachama ziliendelea kuchukua misimamo ya mielekeo ya pamoja hasa katika masuala yaliyohusiana na hatua za Marekani na Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina, Lebanon na Syria yakiwa yametawala taarifa za pamoja za mwishoni mwa vikao hivyo. Kwa mfano katika kikao cha 11 kilichofanyika mwaka 2008 nchini Senegal, nchi wanachama wa OIC, sio tu zililaani jinai na hatua za kinyama za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na Lebanon lakini pia zililaani na kupinga hatua za Marekani za kuiwekea Syria vikwazo vya upande mmoja. Mbali na kutangaza mshikamano wao na taifa la Syria, nchi hizo zilisisitiza pia kwamba sheria ya kuliadhibu taifa hilo la Kiarabu iliyotangazwa na Marekani ni batili.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa katika kipindi hicho mielekeo ya busara na ya wastani ilishuhudiwa katika misimamo ya msingi iliyochukuliwa na nchi wanachama wa OIC, na kuwa na mchango athirifu wa kupatikana sauti ya pamoja kati ya nchi za Kiislamu. Hiyo ilikuwa harakati iliyosimama mkabala na dhidi ya matapo mawili, ambayo yalikuwa kila mara yakivuruga umoja na utangamano wa Ulimwengu wa Kiislamu: Tapo la kwanza ni la misimamo ya kufurutu mpaka katika kuamiliana na dunia nzima kupitia makundi kama Taliban; na la pili ni la wafanya mapatano na maadui hususan Israel. Kudhihiri na kupata nguvu mmea huo wa misimamo ya busara na wastani ndani ya OIC na kuongezeka hamu ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na ndani ya jumuiya yenyewe, kulitoa fursa kwa viongozi wa nchi za Kiislamu ya kutumia uwezo na fursa hizo kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano zaidi, sambamba na kutumia suhula zilizoko katika OIC ili kuweza kufikia lengo hilo.

Mkutano wa 12 wa viongozi wa OIC ulipangwa kufanyika Machi 15, mwaka 2011 katika mji wa Sharm Sheikh, Misri, lakini haukuweza kufanyika baada ya kuanza vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu katika eneo na kuanza mapinduzi ya umma na machafuko ndani ya nchi hiyo. Matukio hayo yalikuwa chachu ya kufufuka tena mivutano na utengano baina ya nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, OIC maudhui ambayo inshallah tutakuja kuizungumzia katika sehemu ya 59 ya kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags