Jul 06, 2018 04:25 UTC
  • Ijumaa, tarehe 6 Julai, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 22 Shawwal 1439 Hijria sawa na tarehe 6 Julai 2018.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na Tanzania, Zambia na Msumbiji.

Bendera ya Malawi

Tarehe 6 Julai miaka 43 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia.Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 huku ikipatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.

Bendera ya Comoro

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.

William Faulkner

Na siku kama ya leo miaka 164 iliyopita alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii.

George Simon Ohm