Sep 16, 2018 09:44 UTC
  • Jumapili, Septemba 16, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 6 Muharram 1440 Hijria, sawa na tarehe16 Septemba 2018, Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie. Huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.”  Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.” Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kufahamu kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad lilifahamu nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwatan illa Billah.”

Kaburi la Habib Bin Madhahir

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, yaani sawa na tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa wa mjini Madina. Barua hiyo ilisema: "Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nasi atapata daraja ya kuuawa shahidi na ambaye hatajiunga nasi hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na jumbe kadhaa, miongoni mwa jumbe hizo ni kwamba Imam Hussein alikuwa akijua kuwa angeuawa shahidi yeye na masaba zake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote waliofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote wangeuawa na kumtaka mtu yeyote aliyekuwa na malengo mengine ghairi ya hayo arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1034 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alifahamika kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihi ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

Kaburi la Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi

Siku kama ya leo, miaka 282 iliyopita, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo.

Daniel Gabriel Fahrenheit

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, Mexico ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Mexico ni nchi yenye historia kongwe inayorejea nyuma karibu miaka elfu tano kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS. Wahispania waliwasili Mexico mwaka 1518 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kutumia vibaya hitilafu za ndani na kutofahamu wananchi malengo waliyokuwanayo wavamizi hao. Mexico inapakana na Marekani na Guatemala na akthari ya wananchi wake ni wakatoliki. Mji mkuu wa Mexico ni Mexico City na sarafu ya nchi hiyo ni Peso ya Mexico huku lugha rasmi ya nchi hiyo ikiwa ni Kihispania.

Bendera ya Mexico

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo Omar Mukhtar alilazimika kurejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano wakiwa na lengo la kuitawala Libya walianzisha vita na dola la Uthmania. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha kumnyonga katika siku kama ya leo.

Omar al Mukhtar

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia. Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusomea huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Uvumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.

Sir Ronald Ross

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, mji mkuu wa Poland Warsaw ulizingirwa na Wajerumani katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Poland yalianza siku 15 kabla ya hapo. Licha ya kuwa Poland ilikabiliwa na mashambulio ya pande mbili ya Ujerumani na Umoja wa Kisovieti, lakini jeshi lake lilisimama kidete na kuuhami mji wa Warsaw. Hata hivyo baada ya siku 11 za kusimama kidete na kuuawa watu wengi waliokuwa wakiulinda mji wa Warsaw, mji huo ulidhibitiwa na kuangukia mikononi mwa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi.

Mji mkuu wa Poland, Warsaw

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944.

Kuanza utawala wa Reza Khan

Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando yake. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Zilzala ya Tabas