Sep 26, 2018 00:32 UTC
  • Jumatano, Septemba 26, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 16 Muharram 1440 Hijria sawa na 26 Septemba, 2018.

Siku kama ya leo miaka 180 iliyopita sawa na tarehe 16 Muharram 1260 Hijria, Amir Abdul Qader al Jazairi alitiwa mbaroni baada ya kupita miaka 15 ya mapambano yake dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Sababu kuu iliyopelekea al Jazairi kutiwa mbaroni na kushindwa mbele ya vikosi vamizi vya Ufaransa ni kukosa kambi imara ya wapiganaji wake ndani ya ardhi ya Algeria na kulazimika kuweka kambi katika eneo la mpaka wa nchi hiyo na Morocco. Kwa kuzingatia kuwa mtawala wa Morocco pia alikuwa chini ya utawala wa Ufaransa, Abdul Qader al Jazairi alipigwa marufuku kuendesha mapambano yake akiwa katika eneo la mpakani. Mpigania uhuru huyo alifungwa jela miaka tisa nchini Ufaransa na kisha akaachiwa huru kwa sharti kwamba asirejee nchini mwake.

Amir Abdul Qader al Jazairi

Katika siku kama ya leo miaka 130 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.

Thomas Stearns Eliot

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.

Bendera ya New Zealand

Siku kama hii ya leo miaka 6 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus akitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Maya Nasri