Sep 28, 2018 23:12 UTC
  • Jumamosi, 29 Septemba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 29 Septemba 2018.

Tarehe 19 Muharram mwaka 61 Hijria, yaani miaka 1379 iliyopita msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa mji wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa mji wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah ***

Msafar wa mateka wa Karbala

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya Chuo Kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954. ***

Enrico Fermi

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Emile Zola alindika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal." ***

Emile Zola

Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mashhad. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la Munafikiin. Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah, na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa. ***

Sayyid Abdul Karim Hasheminejad

Na miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walikufa shahidi katika ajali ya ndege. Makamanda hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan-ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu. ***

Kutoka kulia:  Mashahidi Jahan-ara, Fakuri, Fallahi, Namjuu na Kolahduz