Jumapili, 30 Septemba, 2018
Leo ni Jumapili tarehe 20 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 30 Septemba mwaka 2018 Miladia.
Siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, yaani sawa na tarehe nane Mehr, aliaga dunia Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi mmoja wa malenga na washairi mahiri wa Iran. Moulavi alikuwa mshairi mkubwa na mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa mwaka 604 Hijria katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya leo. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Manavi.

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika.

Na leo tarehe 30 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Viziwi. Lengo la siku hii kupewa jina hilo ni kutaka kuimarisha utamaduni wa kuwa na mawasiliano na watu wenye ulemavu huo, kustawisha maarifa ya lugha ya ishara na kuwazindua wanasiasa na watu wa kawaida kuhusu matatizo ya watu wa tabaka hilo.
