Alkhamisi tarehe 4 Oktoba, 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Muharram 1440 Hijria sawa na tarehe 4 Oktoba, 2018.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Imam Khomeini Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu alihama kutoka Iraq na kuelekea Paris Ufaransa. Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu alichukua uamuzi huo wa kufanya hijra hiyo ya kihistoria pale utawala wa zamani wa Iraq ulipokuwa ukijiandaa kuzuia mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikifanya kila linalowezekana ili kulinda uhusiano wao na utawala wa Shah ulimtaka Imam kuacha kufanya shughuli zozote za kisiasa na kipropaganda dhidi ya utawala wa Shah. Hatimaye katika siku kama ya leo Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu alielekea Paris Ufaransa kufuatia kushadidi mashinikizo ya utawala wa Baath wa Iraq na baada ya Kuwait kupinga Imam kuelekea nchini humo.
Tarehe 4 Oktoba miaka 90 iliyopita, tabibu Alexander Fleming ailivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe 6 Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe 4 Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.
Miaka 168 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia Haj Mulla Muhammad Taqi Istarabadi. Mullah Muhammad Taqi bin Muhammad Ismail alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Alipata ruhusu ya daraja ya ijtihad katika elimu ya fiqhi kutoka kwa Muhammad Taqi bin Muhammad Rahiim Tehrani aliyekuwa maarufu kwa jina la Sahib Hidayatul Mustarshidiin na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa Najaf na Karbala nchini Iraq kwa kipindi cha miaka 14. Mulla Muhammad Taqi Istirabadi alihamia Tehran mwaka 1271 Hijria na kabakia katika mji huo hadi alipoaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.