Oct 04, 2018 22:55 UTC
  • Ijumaa tarehe 5 Oktoba 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 25 Muharram 1440 Hijria sawa na tarehe 5 Oktoba 2018.

Siku kama ya leo miaka 1344 inayosadifiana na tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, aliuawa shahidi Ali bin Hussein mwenye lakabu ya Sajjad na Zainul Abidiin AS, mtoto wa Imam Hussein bin Ali AS, na mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Zainul Abidiin AS alizaliwa mjini Madina mwaka 38 Hijria. Mtukufu huyo alichukua jukumu la kuwafikishia Waislamu ujumbe mzito wa mapambano ya baba yake baada ya kuuawa shahidi huko Karbala. Imam Sajjad AS ameuachia Umma wa Kiislamu kitabu cha Al Swahifatu Sajjadiyya' chenye thamani kubwa ambacho kimejaa dua zenye mafunzo na maarifa ya Kiislamu.

Tarehe 25 Muharram miaka 187 iliyopita, lilichapishwa gazeti la kwanza la Iran lililojulikana kwa jina la Kaghaze Akhbar. Gazeti hilo lilichapishwa na Mirza Swaleh Shirazi mjini Tehran, likiwa na kurasa mbili kubwa. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa mwezi na lilizungumzia habari za Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki.

Kaghaze Akhbar

Nakala pekee iliyobakia ya gazeti hilo imehifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Uingereza.

Tarehe 5 Oktoba miaka 154 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mwanaviwanda mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema.

Louis Jean Lumiere

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran.

Imam Khomeini

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake.

Slobodan Milosevic

Na tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994 kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanadamu.

Siku ya Kimataifa ya Mwalimu