Oct 06, 2018 23:00 UTC
  • Jumapili, Oktoba 7, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 27 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijiria, sawa na tarehe 7 Oktoba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa kwa mabomu baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala dhalimu wa kizazi cha Banii Umayyah, Yazid bin Muawiyya. Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika medani ya Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume kuchukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mabomu.

Al Kaabah, Nyumba ya Mwenyezi Mungu

Siku kama ya leo miaka 239 iliyopita, alifariki dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.

Sheikh Abdullah Tostari

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo.

Picha ya hati ya katiba hiyo

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan.

Sohrab Sepehri

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Bendera ya Ujerumani

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Hussein Muhammadi Laini, faqihi mkubwa. Ayatullah Laini alizaliwa mwaka 1343 Hijiria katika moja ya vijiji vya mji wa Behshahr nchini Iran. Akiwa kijana mdogo aliondokewa na baba yake na hivyo kubakia chini ya usimamizi wa mama yake. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Najaf, Iraq ambapo aliishi kwa kipindi cha miaka 12 akisoma kwa maulama wakubwa akiwemo Sayyid Mahmoud Hashemi Shahroudi na Mirza Hashem Amoli. Baada ya kuchukua ijaza (idhini) kadhaa za Ijtihadi na kufikia nafasi ya marjaa, alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji. Aidha Ayatullah Hussein Muhammadi Laini alishiriki katika harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala kibaraka wa Shah. Ayatullah Hussein Muhammadi Laini alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Ayatullah Hussein Muhammadi Laini

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan kuuangusha utawala wa Taliban na hata baada ya kuuawa Mulla Omar, kiiongozi wa kundi hilo la kigaidi, lakini bado kundi hilo lina ushawishi mkubwa nchini humo.

Uvamizi wa kidhalimu wa Marekani dhidi ya Afghanistan