Alkhamisi tarehe 11 Oktoba 2018
Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Safar 1440 Hijria sawa na tarehe 11 Oktoba 2018
Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.
Tarehe Mosi Safar miaka 1379 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wake katika mji wa Kufa, Iraq.

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza vilianza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.
11 Oktoba mwaka 1991 yaani siku kama ya leo miaka 27 iliyopita shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika nchi hiyo. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.
Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu. Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala.