Oct 12, 2018 23:11 UTC
  • Jumamosi, 13 Oktoba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 3 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 13 Oktoba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2557 mji wa kihistoria wa Babel ulitekwa na Kourosh, mwasisi wa utawala wa kizazi cha Hakhamaneshi nchini Iran. Ili kuweza kuudhibiti mji huo ambao ulikuwa na ngome kubwa na imara, Kourosh aliamuru kubadilishwa mkondo wa Mto Tigris uliokuwa ukipita katikati ya mji wa Babel. Kwa utaratibu huo askari wa Kourosh walitumia njia ya zamani ya maji ya mto huo kuingia na kisha kuuteka mji wa Babel. Mji huo ulioko kusini mwa eneo la Mesopotamia katika Iraq ya sasa, ulikuwa katika kilele cha maendeleo na nguvu kubwa katika kipindi hicho.***

Mji wa kihistoria wa Babel

 

Miaka 1383 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria na kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na alikuwa mashuhuri kwa elimu kubwa na maarifa, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama hizo. Kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu na mtu aliyebobea katika maarifa. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu adhimu wa kuzaliwa Imam Baqir (AS). ***

 

Katika siku kama ya leo miakka 136 iliyopita, alifariki dunia mwandishi na mwanafalsafa wa Kifaransa, Joseph Arthur Gobineau. Gobineau alizaliwa mwaka 1816 mjini Paris na baada ya kumaliza masomo yake alijishughulisha na uandishi wa habari. Aidha Gobineau aliwahi kuwa katibu na balozi wa Ufaransa nchini Iran na kupata kujifunza lugha za Kifarsi na Kiarabu. Mwandishi huyo wa Kifaransa aliamini kuwa watu weupe hasa wale wenye asili ya Aryan ndio watu bora zaidi na kuhusiana na suala hilo akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na kutokuwepo usawa kati ya wanadamu. Nadharia ya kuwa kizazi cha Aryan ndicho kizazi bora zaidi kuliko vizazi vingine vya wanadamu ni moja ya sababu zilizompelekea Adolf Hitler kuanzisha Vita vya Pili vya Dunia na kuua kwa umati watu wasiokuwa wa asili ya Aryan. ***

Joseph Arthur Gobineau

 

Na siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, bunge la kimaonyesho la Iran lilipasisha sheria iliyowapa washauri wa kijeshi wa Marekani nchini kinga ya kutofikishwa mahakamani iwapo wangepatikana na hatia ya aina yoyote. Kwa mujibu wa sheria hiyo, wahalifu wa Kimarekani wangehukumiwa nchini kwao kama watatenda jinai nchini Iran, na mahakama za Iran hazikuwa na haki ya kushughulikia kesi zao. Sheria hiyo ilitambuliwa kuwa dharau kwa taifa la Iran na iliyokiuka wazi kujitawala kwa nchi. Kwa msingi huo hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) siku kadhaa baada ya kupasishwa sheria hiyo bungeni alitoa hotuba ya kihistoria akieleza taathira zake na kumshambulia vikali Mfalme Shah na Marekani. Baada ya hotuba hiyo Imam Khomeini alikamatwa na kupelekwa uhamishoni. ***

Capitulation