Jumatatu tarehe 15 Oktoba 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 5 Safar 1440 Hijria sawa na 15 Oktoba 2018.
Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita Ruqayyah binti mchanga wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya. Ruqayyah alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha. Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid Muawiya akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wanahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein (as) kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mchana ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho.

Siku kama ya leo miaka 476 iliyopita alizaliwa Abolfath Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme mwenye nguvu wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah ambaye baada ya kufariki dunia baba yake Homayun, alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza akiwa chini ya usimamizi wa Bairam Khan aliyekuwa na cheo cha naibu mtawala. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abolfath Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan, kilicho kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno huku akifanikiwa pia kuleta nidhamu nchini India. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita yaani tarehe 15 Oktoba mwaka 1894, ilianza kesi ya Alfred Dreyfus mjini Paris Ufaransa. Dreyfus alikuwa afisa wa jeshi la Ufaransa mwenye asili ya Kiyahudi ambaye kesi yake ni miongoni mwa matukio yaliyozusha makelele mengi katika karne ya 19 nchini humo. Afisa huyo wa jeshi alituhumiwa kuisaliti nchi yake na kutoa siri za jeshi la Ufaransa kwa Ujerumani. Alivuliwa cheo chake na akahukumiwa kifungo cha maisha jela. Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, ilithibitika kwamba Alfred Dreyfus hakuwa na hatia yoyote. Kwa utaratibu huo aliachiwa huru na kurejeshewa heshima na vyeo vyake. Hukumu ya kifungo cha maisha jela ya Dreyfus na kisha kutambuliwa kwake kuwa hakuwa na hatia, kadhia ambayo inatambuliwa kwa jina la Dreyfus Affair, ilitumiwa na Wazayuni katika propaganda za urongo kudai kwamba Wayahudi wamedhulumiwa barani Ulaya. Wazayuni walitumia vibaya kadhia hiyo kujiimarisha zaidi.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, mwakilishi wa Imam Khomeini (MA) na Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran Ayatullah Ashrafi Isfahani, aliuawa shahidi na vibaraka wa kundi la MKO akiwa katika mihrabu ya ibada. Ayatullah Ashrafi Isfahani aliongoza wananchi wa Kermanshah katika harakati na mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah. Aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na aliuawa shahidi katika mihrabu akisalisha Swala ya Ijumaa.
Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika.
