Ijumaa tarehe 19 Oktoba mwaka 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 9 Safar 1440 Hijria sawa na Oktoba 19 mwaka 2018.
Katika siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia Ammar: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.

Siku kama ya leo miaka 1017 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."
Tarehe 9 Safar miaka 845 iliyopita yaani tarehe tisa Safar mwaka 595 Hijria, alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.
Miaka 237 iliyopita katika siku inayofanana na ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha majeshi ya Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi. Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza. Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Ali Hassan Salamah mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Salameh alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine.
Tarehe 27 Mehr miaka 31 iliyopita manowari za jeshi la Marekani zilishambulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran. Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya Kuwait iliyokuwa ikiusaidia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran, kuitihumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa imeshambulia meli yake ya mafuta. Marekani ilivishambulia visiwa vya mafuta vya Iran kwa madai kuwa meli ya Kuwait iliyoshambuliwa na Iran ilikuwa na bendera ya nchi hiyo.
Na siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina. Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa. Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka hapo 1991. Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia katika mashambulizi ya askari wa Serbia na dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.