Nov 11, 2018 12:35 UTC
  • Jumapili, Novemba 11, 2018

Leo ni Jumapili tarehe tatu Mfungo Sita, Rabiul-Awwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 11 Novemba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 999 iliyopita alifariki dunia Abul-Ula Ma’arri, malenga na mwandishi maarufu wa Kiarabu. Abul-Ula Ma’arri alizaliwa mwaka 363 Hijiria nchini Syria ya leo ambapo alisoma masomo ya msingi mjini Ma’arri, huku akiendelea na masomo yake ya lugha na fasihi katika miji mingine. Baadaye Abul-Ula Ma’arri alielekea mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo yake. Licha ya kwamba alikuwa kipofu, lakini alitokea kuwa malenga mashuhuri wa zama zake. Miongoni mwa athari za Abul-Ula Ma’arri ni pamoja na kitabu cha ‘Risaalatul-Ghufraan’ na ‘Al-Aamaal.’

Abul-Ula Ma’arri

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, alizaliwa Fyodor Dostoyevsky, mwandishi mkubwa wa Urusi. Akiwa kijana Dostoyevsky alijiunga na shule ya uhandisi wa masuala ya kijeshi, hata hivyo taratibu alianza kujifunza fasihi ya nchi tofauti za dunia na hatimaye mwishoni mwa kipindi cha masomo yake ya kijeshi akatokea kuwa mtaalamu katika uga wa fasihi. Mwaka 1849 Miladia, Fyodor Dostoyevsky alitiwa mbaroni na kuwekwa jela kwa kosa la kujishughulisha na harakati za kisiasa. Baada ya kutoka jela na kwa kutumia tajriba na uzoefu aliokuwa nao alitoa athari muhimu miongoni mwa fasihi za Russia. Dostoyevsky ameacha athari kadhaa katika uga wa fasihi na alifariki dunia mwaka 1881.

Fyodor Dostoyevsky

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), mtafiti na mtaalamu wa Hadithi wa Kishia. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Qazvin na baada ya hapo alielekea mjini Isfahan kwa ajili ya masomo ya juu. Aidha baada ya kustafidi na maulama wakubwa wa mji wa Isfahan alifanya ziara katika maeneo matakatifu ya nchini Iraq ambapo huko alikaa miaka kadhaa akijiendeleza kimasomo. Kisha alirejea mjini Qazvin na kuanza kazi ya ufundishaji na kutoa fatwa. Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini ameacha athari kadhaa kama vile’Mi’raajul-Wusuuli ila ilmul-Usuul’ chenye juzuu mbili, ‘Lawaamiu fil-Fiqhi’ chenye juzuu tatu na ‘Mir'aatul-Muraadi fi Ilmir-Rijaal.’

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.

Viongozi waliohusika katika utiaji saini

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.

Dakta Jonas Salk

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, nchi ya Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani. Katika karne ya 16 Miladia, Ureno iliyatumia maeneo ya pwani ya Angola kuanzisha vituo muhimu vya biashara na kupanua ukoloni wake wa kila upande katika maeneo hayo. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia ambapo nchi nyingi zilizokuwa zikikoloniwa zilikuwa zikijitangazia uhuru, waasi wa Angola pia walianzisha harakati za kupigania uhuru na hatimaye kufanikiwa kupata uhuru katika siku kama ya leo. Angola ina kilometa mraba 1246700 huko kusini magharibi mwa bara la Afrika, huku ikiwa inapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Namibia na Botswana.

Inakopatikana Angola

Na siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.

Yasser Arafat

 

Tags