Nov 27, 2018 15:23 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 14 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia suala la uhuru kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyopewa kipaumbele na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (MA). Tulisema kuwa suala hilo limekuwa likipiganiwa na pande na watu tofauti mashuhuri katika historia. Leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

Sambamba na Imam Khomeini (MA) kukubali na kuunga mkono uhuru, aliutaja pia kuwa ni moja ya haki za kidhati, kifitra na kiasili za mwanadamu. Aliamini kwamba, uhuru si katika haki zinazotolewa na mtu kama zawadi kwa mtu mwingine, bali ni miongoni mwa haki asilia za wanadamu. Hata kama kila jamii au serikali ina haki ya kuweka vizuizi na kubana uhuru kwa kiwango fulani kwa ajili ya kudhamini nidhamu katika jamii na usalama  wake, lakini haina haki ya kuvuruga misingi na nguzo za uhuru huo. Kiufupi ni kwamba, kwa mtazamo wa Imam Khomein, uhuru upo katika dhati ya mwanadamu na katika msingi wa ubinaadamu wake. Sisitizo la kutaka wananchi washirikishwe katika mfumo na maamuzi ya serikali, uchaguzi na mambo mengine muhimu serikalini ni mifano ya wazi ya umuhimu uliopewa suala la uhuru katika maneno na matamshi ya Imam Khomeini (MA). Imam sambamba na kutambua uhuru mbalimbali wa mtu binafsi, wa kijamii na kisiasa, uhuru wa kutoa maoni, itikadi na kujieleza, uhuru wa kuunda vyama na mikusanyiko na ushiriki katika kuchukua maamuzi, nukta kama vile kutosababisha madhara kwa maslahi fulani, kutofanya njama dhidi ya serikali, ufisadi, kulinda misingi ya akhlaqi, aliichukulia akili na sheria ya dini kuwa vipimo muhimu vya uhuru. Katika uwanja huo Imam Khomein aliamini kuwa uhuru unaopaswa kubanwa na kupokonywa mtu ni ule unaodhuru utu wake na kuhatarisha maslahi ya kijamii.

**********

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, dini ya Uislamu ndio mfumo pekee unaodhaminia mwanadamu uhuru halisi. Anasema: “Uislamu ni dini inayotuweka huru na  kutudhaminia uruhu salama na sahihi.” (Hotuba ya Imam ya tarehe 8, 3, 1358). Katika radiamali yake kuhusiana na utawala wa kidikteta wa Shah ambao kwa uongo, ulidai kuwapatia uhuru raia wa Iran anasema: “Amepeana uhuru??!!, Kwani uhuru ni wa kupeanwa?! Neno hilo lenyewe kimsingi ni hatia. Kudai kuwa tumepeana uhuru, ni hatia. Uhuru ni mali ya watu. Sheria imepeana (imetoa) uhuru, Mwenyezi Mungu amepeana uhuru, Uislamu umepeana uhuru, katiba imetoa uhuru kwa wananchi. Ni upuuzi gani huo kudai kuwa tumewapa wananachi uhuru?...Wewe ni nani hadi utoe uhuru huo? Una uwezo gani wewe? ” Hotuba ya tarehe 10/3/1357. Aidha shakhsia huyo alielezea kuwa serikali ya Kiislamu ni ile inayowadhaminia watu uhuru  wa hali ya juu na kutowafanya waiogope . Imam Khomeini (MA) anasema: “Hakuna ukandamizaji katika Uislamu. Ndani ya Uislamu kuna uhuru kwa ajili ya watu wa matabaka yote, wanawake kwa wanaume, weupe kwa weusi,  kwa ajili ya wote. Kuanzia sasa wananchi wanatakiwa waogopane wao kwa wao na sio waiogope serikali. Jiogopeni nyinyi wenyewe ili msifanye makosa. Serikali ya uadilifu inazuia maovu, inatoa adhabu, hivyo sisi wenyewe tunatakiwa tujiogope ili tusifanye makosa, kwa njia hiyo serikali ya Kiislamu haitoenda kinyume. Hapo serikali haitowakandamiza wananchi.” Hotuba ya tarehe 12/1/1358.

*******

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 14 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Uhuru wa kiitikadi, kifikra na kujieleza, ni miongoni mwa aina za uhuru muhimu. Moja ya maswali ambayo yalikuwa yakiulizwa na weledi wengi katika kipindi cha kujiri Mapinduzi ya Kiislamu, ni kwamba je, baada kuundwa serikali iliyosimama juu ya misingi ya Uislamu, kungekuwepo tena na nafasi ya uhuru wa kifikra na wa kujieleza nchini? Hata hivyo miezi mitatu kabla ya kufikiwa Mapinduzi, Imam Khomeini (MA) akijibu swali la mwandishi wa habari  huko Noofel Luchatou nchini Ufaransa, aliyetaka kujua iwapo utatumika uhuru wa kiitikadi na kujieleza wa Wamarksi ndani ya utawala wa Kiislamu alisema: “Katika utawala wa Kiislamu, watu wote wana uhuru katika itikadi zao zote.” Kadhalika Imam katika kujibu swali kuhusu hatima na mustakbali wa raia wasiokuwa Waislamu na wale wasioamini itikadi ya madhehebu inayotawala nchini katika serikali ya Kiislamu alisema: “Ndani ya Uislamu kunatekelezwa demokrasia na katika kubainisha itikadi zao na matendo wananchi wako huru, maadamu tu wasifanye njama dhidi ya serikali katika matendo yao.” Aidha akielezea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari alisema: “Vyombo vyote vya habari vina uhuru iwapo tu havitachapisha makala au kutoa taarifa zenye kudhuru taifa.” Hotuba ya tarehe 20/10/1357. Katika uwanja huo, Imam Khomeini aliutaja uhuru kuwa ni tunu na amana ya Mwenyezi Mungu ambayo watu wote wanatakiwa kuitumia vyema na kwa maslahi ya taifa. Imam anasema: “Sisi wote hivi sasa tupo huru na katika mtihani, Mwenyezi Mungu atatujaribu ili kuona je, tumeutumia vyema uhuru huo kwa manufaa ya taifa, Uislamu na nchi? Je, tumepasi mtihani huu au la.......?” Mwisho wa kunukuu. Hotuba ya tarehe 11/3/1358.

*******

Uundwaji wa vyama na mirengo ya kisiasa na kiraia, ni miongoni mwa nguzo muhimu za uhuru. Katika jamii iliyo na demokrasia, mirengo yote ya kijamii huwa huru katika kuunda vyama vya kisiasa au asasi za kiraia, na serikali haitakiwi kufanya jambo lolote la kuzuia uundwaji wa asasi hizo. Imam Khomeini sambamba na kukubali suala hilo aliamini kwamba, serikali ya Kiislamu inapasa kufungamana pia na misingi ya demokrasia na kutozuia uundwaji au shughuli huru za vyama vya kisiasa nchini. Imam alisema: “Mikusanyiko na vyama vya wananchi viko huru maadamu havitahatarisha maslahi ya wananchi, na dini ya Kiislamu imeainisha mipaka katika shughuli zao zote.” Hotuba ya tarehe 11/8/1357. Akifafanua suala la kutofungamana na madola ya kigeni kama moja ya vigezo muhimu vya shughuli za vyama na mirengo ya kisiasa nchini sambamba na kujibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua mtazamo wake juu ya shughuli za vyama vya kisiasa vya mrengo wa kushoto visivyofungamana na madola ya kigeni katika serikali ya Kiislamu alisema: “Katika Jamhuri ya Kiislamu kila mtu amedhaminiwa haki ya uhuru wa kiitikadi na kujieleza, lakini haturuhusu mtu au kundi lolote kufungamana na madola ya kigeni au kufanya hiana.” Hotuba ya tarehe 29/8/1357.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 14 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.