Dec 03, 2018 06:51 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Disemba 3

Haya ni baadhi ya matukio ya spoti yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa....

Soka ya Walemavu; Iran yatwaa Ubingwa

Timu ya taifa soka ya wachezaji wenye utindio wa ubongo (cerebral palsy) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya mabingwa wa mchezo huo ya bara Asia, ya mwaka huu 2018. Hii ni baada ya kuigaragaza Australia mabao 7-0 katika fainali iliyopigwa Alkhamisi. Rasul Atashaafrouz alifanikiwa kufunga mabao matatu ya hatrick huku Abbas Torabi akitiwa wavuni mawili. Abdorezza Karimizadeh na Farzad Mehri walifunga bao moja kila mmoja na kuihakikishia Iran ushindi huo mnono. Nahodha wa timu hiyo ya Iran Karimizadeh alitawazwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengine kwenye mashindano hayo, kwani alifanikiwa kucheka na nyavu mara 13. Ilikuwa mbwembwe na vifijo pale Iran ilipotunukiwa taji hilo. Siku hiyo hiyo ya Alkhamisi, Jordan iliibanjua Thailand mabao 8-2 na kuibuka mshindi wa tatu. Iran siku ya Jumamosi ilishuka dimbani kuvaana na Thailand katika mchuano wake wa ufunguzi, ambapo waliigeuza timu hiyo kichwa cha mwendawazimu na kuinyoa mabao 7-1 bila maji. Mashindano hayo yanayofahamika kama Asia-Oceania Championship yameandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka ya Wachezaji Wenye Utindio wa Ubongo (International Federation of Cerebral Palsy Football). Australia pia ilianza vyema kwa kuichachafya Korea Kusini mabao 11-0, kwenye mashindano hayo ya siku nane yaliyomalizika Novemba 30.

Soka ya Wanawake; Iran yamaliza ya 2

Timu ya taifa ya soka ya wanawake wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya mabingwa wa mchezo huo yaliyofanyika huko Uzbekistan. Hii ilikuwa ni duru ya kwanza ya mashindano hayo ya kieneo, yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Asia ya Kati CAFA (Central Asian Football Association). Katika mchuano wake wa mwisho wa mashindano hayo ya CAFA Women's Championship, Iran iliisasambua Kyrgyzstan mabao 5-0.

Timu ya soka ya wanawake wa Iran

Awali timu hiyo ya taifa ya wanawake wa Iran ya Kiislamu ilizichabanga Afghanistan na Uzbekistan katika michuano ya awali kwenye mashindano hayo ya kieneo. Mwenyeji Uzbekistan imeibuka kidedea na kutwaa taji la CAFA mwaka huu 2018 kwa upande wa wanawake, kwenye mashindano hayo ya kibara yaliyoanza Novemba 23 na kufikia tamati Disemba Mosi.

Fainali ya Soka la Wanawake Afrika

Timu ya taifa ya soka ya wanawake wa Nigeria imetwaa ubingwa wa Kombe la Afrika mwaka huu 2018 baada ya kuisasambua Afrika Kusini mabao 4-3 katika mikwaju ya penati. Fainali hiyo ya kukata na shoka ililazikimika kuingia katika upigaji penati, baada ya kumalizika dakika 90 za ada na 30 za nyongeza bila timu yoyote kuona lango la mwingine. Kipa wa Nigeria, Tochukwu Oluehi ndiye alikuwa nyota wa mchuano, baada ya kuokoa mkwaju wa Linda Motlhalo.

Nigeria vs Afrika Kusini

Super Falcons wa Nigeria waliingia kwenye mashindano haya kama mabingwa watetezi, na katika fainali hii walilazika kucheza kufa kupona, ikizingatiwa kuwa katika mchuano wa mwanzoni mwa mashindano hayo, walikuwa wamenyukwa na Banyana Banyana.  Mechi hiyo ya fainali ilipigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Accra jijini Ghana.

Mwamuzi wa mchuano huu alikuwa Gladys Lengwe kutoka Zambia. Nigeria, ambao ni mabingwa watetezi, walifuzu katika hatua ya fainali baada ya kuishinda Cameroon kwa mabao 4-2, katika mechi ya nusu fainali, huku Afrika Kusini wakiishinda Mali mabao 2-0. Siku ya Ijumaa, Cameroon iliishinda Mali mabao 4-2 katika mechi muhimu ya kumtafuta mshindi wa tatu. Mataifa mengine yaliyoshiriki katika michuano hii ni pamoja na wenyeji Ghana, Algeria na Equitorial Guinea. Nigeria imeshinda taji hili mara 10, mwisho ilikuwa ni mwaka 2016. Afrika Kusini haijawahi kushinda taji hili lakini imefika fainali mara nne, mwaka 1995, 2000, 2008 na 2012. Nigeria, Cameroon na Afrika Kusini, zimefuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2019 jijini Paris nchini Ufaransa.

Klabu Bingwa Afrika; Simba na Gor zaanza vyema

Miamba ya soka nchini Kenya, klabu ya Gor Mahia wameanza vyema kampeni yao ya kutwaa taji la klabu bingwa barani Afrika baada ya kuwalaza Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa bao moja kwa nunge.  Kogalo walihitaji bao la Bernard Ondiek zikisalia sekunde chache kukamilika kwa mechi iliyopigwa ugani Kasarani.

Sasa Kogalo watasafiri ugenini kabla ya kujua iwapo watasonga kwenye raundi ya pili na makundi mtawalia. Kwenye mechi nyengine, Simba ya Tanzania iliigaragaza Mbabane Swallows mabao 4-1. Nkana FC iliiadhibu UD Songo mabao 2-1, Al Merreikh ikaichapa Vipers Sports Club mabao 2-1 huku mchuano wa APR na Club Africain ukiishia kwa sare tasa. Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliinyoa kwa chupa Light Stars na kuipa kichapo cha mbwa cha mabao 5-0. 

Dondoo za Hapa na Pale

Shirikisho la Soka Afrika CAF limeitoa Cameroon tonge mdomoni. Ndivyo unavyoweza kueleza hali iliyojiri baada ya kikao cha kamati ya utendaji cha shirikisho hilo ilipokutana katika mji mkuu wa Ghana, Accra, na kukubaliana kwa kauli moja juu ya kuipokonya Cameroon uenyeji wa fainali za mataifa ya Afrika Afcon zilizopangwa kuchezwa mwakani 2019. CAF wametangaza kuipokonya uenyeji Cameroon na kutangaza taifa linalotaka kuwa mwenyeji litume maombi ndani ya mwezi mmoja tokea sasa, kabla ya shirikisho hilo kufunga zoezi hilo na kufanya uamuzi baada ya kupitia maombi ya mataifa hayo. Uamuzi huo wa CAF unakuja ikiwa zimepita siku chache toka shikisho hilo litume wajumbe wake nchini Cameroon kwenda kukagua mazingira ya kufanyika michezo hiyo ya kikanda. Duru za habari zinasema miundombinu isiyoridhisha na hali mbaya ya usalama ndiyo imepelekea CAF kufikia maamuzi hayo.

Kwengineko, timu ya taifa ya soka Kenya, Harambee Stars, imefuzu katika fainali ya mataifa bingwa mwaka 2019. Hatua hii imekuja, baada ya uamuzi wa Kamati kuu ya CAF, kuamua kuiondoa Sierra Leone katika michuano ya kufuzu,baada ya kufungiwa na Shirikisho la soka duniani FIFA. Kenya ambayo ipo katika kundi F, pamoja na Ghana na Ethiopia, itakuwa miongoni mwa timu mbili zitakazofuzu, hata iwapo itashindwa katika mechi yake ya mwisho ya kundi hilo mwezi Machi mwaka 2019.

Mbali na hayo timu ya raga ya Kenya iliaga mapema mbio za kugombea ubingwa wa duru ya Raga ya Dunia ya wanawake ya Dubai Sevens baada ya Lionesses kupoteza mechi yake ya pili mfululizo kwa kulimwa 27-12 na Jamhuri ya Ireland katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Alkhamisi.

Na Arsenal wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani wamefanikiwa kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote wa mashindano msimu huu kwa mchezo wao wa 19 sasa, baada ya kuifunga Tottenham magoli 4-2. Magoli ya Arsenal yakifungwa na Pierre Aubameyang kwa penati dakika ya 10 na 56, Alexander Lacazatte dakika ya 74 na Lucas Torreira dakika ya 77.

Magoli ya Tottenham yalifungwa na Eric Dier dakika ya 30 na Harry Kane kwa mkwaju wa penati dakika ya 43. Arsenal sasa wanajiweka nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya EPL na kuwashusha Tottenham Hotspurs hadi nafasi ya tano, wakiwa wote wana point 30 ila wanatofautiana kwa magoli magoli ya kufunga na kufungwa.

…………………..TAMATI……………..