Dec 22, 2018 09:22 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 795 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 45 na 46 ambazo zinasema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّقُوا مَا بَيْنَ أَيْدِيكُمْ وَمَا خَلْفَكُمْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Na wanapo ambiwa: Ogopeni yaliyoko mbele yenu na yaliyoko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...

وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ

Na haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.

Katika aya tulizosoma kwenye darsa kadhaa zilizopita zilizungumziwa alama za uwezo na adhama ya Allah SW katika ulimwengu wa maumbile. Aya tulizosoma hivi punde zinaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba: kundi moja miongoni mwa watu, badala ya kuzingatia hayo na kumuelekea Mwenyezi Mungu na Mitume wake na kupata mafunzo kutokana na ishara hizo za uwezo wa Mola linaamua kujitenga na kuipa mgongo haki. Pale watu wa aina hiyo wanapotakiwa wajihadhari na mienendo na matendo yao ili wasije wakafikwa na adhabu za duniani na akhera, wao huwa hawajali, bali huendelea kufanya mambo yao yasiyofaa. Ilhali, laiti kama wataacha mambo hayo na kurejea kwenye haki watapata rehma za Allah; na Yeye Mola atawasamehe makosa yao yaliyopita. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ishara za uwepo na adhama ya Allah SW katika ulimwengu ni nyingi mno lakini watu wanaokubali na kuyaamini hayo ni wachache. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa njia ya kupatia rehma za Allah iko wazi muda wote isipokuwa kama yeye mtu mwenyewe ataamua kujifungia milango ya rehma za Mola.

Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنُطْعِمُ مَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ أَطْعَمَهُ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ

Na wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tumlishe ambaye Mwenyezi Mungu angependa angeli mlisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.

Aya hii inaashiria moja ya mifano ya ufahamu potofu, wa inadi na ukaidi wa makafiri kwa kueleza kwamba moja ya maamrisho ya Allah kwa waumini ni kuwataka watoe mali zao kuwasaidia wahitaji, ambapo kila mtu mwenye akili timamu na insafu anafahamu na anakubali kwamba kufanya hivyo ni jambo jema na la kheri. Lakini baadhi ya makafiri wakaidi na wenye inadi wanahoji kuhusu amri hiyo ya Mwenyezi Mungu na kusema: Kwa nini Mwenyezi Mungu anakuamuruni ninyi muwasaidie watu wahitaji kwa kuwapa chakula na nguo? Kwa nini haifanyi kazi hiyo Yeye mwenyewe? Bila shaka Yeye mwenyewe hataki hao wahitaji wenye njaa washibishwe. Ni wazi kwamba kuhoji na kulitilia shaka suala hilo kunatokana na fikra zao mgando na sifa yao ya inadi na ukaidi; vinginevyo kila mtu anajua wazi kwamba vyote tulivyonavyo, na hata vile tunavyotoa kuwapa wahitaji vinatokana na riziki aliyotupa Allah SW, na sisi wenyewe hatuna hatunani. Kama ni akili, uhodari na nguvu za mwili, zote hizo ni atiya na neema za Mola tunazozitumia kama nyenzo za kutuwezesha kuwa na madaraka na utajiri. Ukweli ni kuwa Allah SW amewapa matajiri na wenye uwezo jukumu la kuwasaidia na kuwashibisha wahitaji na wenye njaa. Kama ambavyo jukumu la kukidhi mahitaji ya chakula cha mtoto mchanga amelikabidhi kwa mama na kumtayarishia mazingira ya kupata chakula hicho kupitia kwenye kifua chake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama tutaitakidi kuwa vyote tulivyonavyo ni riziki itokayo kwa Mola na si milki yetu tutakuwa wepesi wa kutoa na kuwasaidia wahitaji. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, moja ya alama ya imani ya kweli ni kutoa; na mtu asiyetoa alichonacho kwa ajili ya Allah huwa ni mfano wa mtu aliyekufuru. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mtazamo usio sahihi anaokuwa nao mtu kuhusu utoaji huyafanya yale ambayo kwa mtazamo wa watu ni mambo mema na ya heri yaonekane mbele ya macho yake yeye kuwa ni mambo batili na ya upotofu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 48 hadi ya 50 ambazo zinasema:

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?

 مَا يَنظُرُونَ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً تَأْخُذُهُمْ وَهُمْ يَخِصِّمُونَ

Hawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.

فَلَا يَسْتَطِيعُونَ تَوْصِيَةً وَلَا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ يَرْجِعُونَ

Basi hawataweza kuusia, wala hawatarejea kwa watu wao.

Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya zilizopita zilizoashiria hulka ya ubishi na ukaidi ya baadhi ya makafiri kwa maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba: Watu hao, wanafanya shere na stihzai kuhusu Siku ya Kiyama pia kwa kusema: Kama nyinyi hamuujui wakati hasa kitakaposimama Kiyama, kwa nini basi muda wote mnakuwa na hofu ya kutokea kwake na kujichunga na mnayoyafanya? Kama Kiyama kipo kweli, lini kitatokea ili na sisi pia tusubiri kuwadia kwake? Qur'ani tukufu inavijibu visingizio hivyo vya watu hao kwa kusema: kutojua wakati wa kujiri jambo si hoja ya kuthibitisha kwamba halitokei. Kwa mfano watu wanaoishi kwenye maeneo yenye matetemeko ya ardhi, huwa hawajui lini zilzala hiyo itatokea, lakini wana hakika ya kujiri kwake; na kwa hivyo huwa wamejiweka tayari muda wote. Kiyama kitatokea kulingana na elimu na qudra ya Mwenyezi Mungu, wala mwanadamu hana nafasi yoyote katika jambo hilo. Wakati wowote ule atakapotaka Yeye Mola, ni katika muda mchache kabisa, mbingu zote na ardhi zitaporomoka na kuvunjika na hakuna mtu yeyote atakayekuwa na uwezo wa kukizuia au kukimbia na kukikwepa. Kiyama kitatokea kwa kasi kubwa na kwa kushtukiza, kiasi kwamba hakuna mtu atakayeweza kuikimbilia familia yake au kuwahi kuacha wasia kwa watu wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wakanushaji wa Kiyama hawana hoja ya kusuta uwezekano wa kujiri kwake. Kwa hivyo hujaribu kuibua maswali haya na yale, ili kwa dhana yao walifanye kuwa ni jambo la kutiliwa shaka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Kiyama ni jambo aliloliahidi Mola, kwa hivyo kutobainishwa wakati hasa wa kujiri kwake si hoja ya kuonyesha kuwa hakitatokea. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kumalizika kwa dunia na kujiri Kiyama kutatokea huku watu wakiwa kwenye mizozano na pirikapirika za maisha yao ya kila siku. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kuwa utakapofika mwisho wa dunia mafungamano yote ya kidunia na mahusiano yote ya kifamilia yatatoweka. Siku ya Kiyama kila mtu atalipwa thawabu au adhabu yeye mwenyewe bila ya kuhusishwa baba na mama yake, wala mke na mtoto wake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 795 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags