Dec 24, 2018 11:18 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 800 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 77 hadi 79 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَرَ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ

Kwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!

وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ

Na akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?

قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ

Sema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila uumbaji. 

Kwa mujibu wa mapokeo ya historia mshirikina mmoja wa Makka alichukua kipande cha mfupa uliooza na kumwendea Bwana Mtume Muhammad SAW na kumuuliza: Nani atakayeweza kuuhuisha tena mfupa huu ulioko mkononi mwangu ambao kama nitaubinya utavurugika na kumung'unyika kuwa unga na kubadilika kuwa sehemu ya udongo? Suali hili huwa linajitokeza pale mtu anapoitakidi kwamba uwezo wa Allah Jalla Jalaluh una mpaka maalumu; na kwa kuwa kutokana na yale anayoyashuhudia mtu duniani tukio kama hilo halijawahi kutokea, ndipo anapodai kwamba haitowezekana pia kujiri jambo hilo Siku ya Kiyama. Kwa sababu hiyo, aya zinazofuatia zinatoa jibu kwa wakanushaji wa Maadi, yaani kufufuliwa viumbe kwa kusema: Vipi nyinyi mnadhani uwezo wa Mwenyezi Mungu ni wenye kikomo ilhali amemuumba kila mmoja wenu kutokana na tone dogo kabisa la mbegu ya uzazi? Hivi kweli Mungu huyo aliyekuwa na uwezo wa kukuumbeni nyinyi kwa mara ya kwanza wakati hapo kabla hamkuwepo asilani, atashindwa kulifanya hilo tena kwa mara ya pili? Nyinyi mnadhani kwamba Yeye hajui chembe zote za kila kiungo cha mwanadamu zimetawanyikia wapi ili aweze kuziunganisha tena na kuwapa uhai tena viumbe hao? Mwanadamu, ambaye ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu, ameweza, kwa kutumia sayansi na uwezo wake aliojaaliwa na wenye mpaka maalumu, kupandikiza na kukuza seli za mwanadamu au mnyama katika maabara ili kuendeleza mfumo wa seli hizo. Kama ni hivyo, Je Yeye Allah, Muumba wa yeye mwanadamu, tena mwenye uwezo mutlaki atashindwa kuziunganisha na kuzipandikiza chembechembe za viungo vya kila mwanadamu na kumpa uhai tena kiumbe huyo? Leo hii elimu ya mwanadamu imeweza kuthibitisha kuwa ndani ya molekuli za vinasaba, kitaalamu DNA za seli za mwili wa kila mtu kuna vitu vyote vya kijenetiki ambavyo vinahusiana na mtu huyo peke yake na wala havifutiki wala kutoweka katu. Leo hii maiti za watu walioshindwa kutambulika baada ya kupita makumi kwa makumi ya miaka tangu watu hao walipofariki dunia huwa zinajulikana kwa kuchunguza vinasaba vya seli zao na kuvilinganisha na vya watu wanaoaminika kuwa ni jamaa zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kumhasimu Allah na kukaidi kutii amri na mafundisho yake kunatokana na mtu kughafilika na kusahau asili ya kuumbwa kwake na Mola, ambayo ni kutokana na tone dogo na dhaifu la manii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wanaokanusha kufufuliwa, wao wana shaka na elimu, qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuumba viumbe mara ya pili, lakini hawatoi hoja yoyote ya kimantiki ya kuthibitisha kuwa maadi ni jambo lisilowezekana. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuna mambo mawili ya kuzingatiwa katika kadhia ya maadi. Moja ni uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuwaumba watu mara ya pili na jengine ni elimu na ujuzi wake mutlaki juu ya amali na matendo yao. Vilevile tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa kama kuuliza suali kunafanywa kwa madhumuni ya kutaka kufahamu na kujua, hilo ni jambo zuri lenye kupendeza na inapasa wajuzi na wenye elimu ya dini wayapatie majibu sahihi masuali na mambo ya kiitikadi yenye shubha na utata. Lakini kama uulizaji suali utafanywa kwa ghururi, inadi na ukaidi, lengo halitakuwa kuijua haki na ukweli ila ni kufanya stihzai na kejeli.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 80 ambayo inasema:

الَّذِي جَعَلَ لَكُم مِّنَ الشَّجَرِ الْأَخْضَرِ نَارًا فَإِذَا أَنتُم مِّنْهُ تُوقِدُونَ

Aliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnauwasha.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kuhusiana na qudra na uwezo wa Allah SW katika uumbaji, kwa kuashiria mfano mwengine wa kuvutia katika ulimwengu wa maumbile na kueleza kwamba: Kutokana na kanuni alizoweka Allah katika maumbile, athari za msuguano mkali wa matawi ya miti ya kijani kibichi husababisha kutoka cheche za moto. Ikumbukwe kuwa hapo kale kibiriti hakikuwepo, hivyo watu walikuwa wakitumia njia ya kugongesha mawe au kusugulisha vijiti vya miti na kuweza kupata moto kutokana na joto la msuguano wa vitu hivyo. Aidha ikiwa kimbunga na upepo mkali utasababisha mgongano mkali wa matawi ya miti, athari ya mkondo wa umeme inayojitokeza huzusha cheche za moto na kuifanya miti ya kijani kibichi itoe moto. Katika aya hii, japokuwa maji na moto hayafanyi kazi pamoja, lakini viwili hivyo vimejumuishwa pamoja. Kwa maneno mengine ni kuwa mti wa kijani kibichi ambao unabaki hai kwa kuwa na maji, unakuwa pia chanzo cha kupatikana moto unaokinzana na maji. Tab'an endapo mti huohuo utakauka na kuwa mkavu vijiti vyake hutumika kwa ajili ya kuwashia moto. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuyaelewa maumbile na kanuni zinazotawala ndani yake kunachangia kuifanya imani ya muumini kwa Allah na uwezo wake iwe imara zaidi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwanga na joto la jua vinavyoangaza kwenye matawi na majani ya miti halitoweki, bali huhifadhiwa ndani yake. Wakati mashina na matawi ya miti yanapowaka moto, huwa ile nishati ya jua iliyokuwa imehifadhiwa kwa miaka na miaka ndani ya mashina na matawi ya miti inatoka nje sasa katika sura ya joto la moto. Mchakato na mzunguko huo huwa ni mithili ya ufufukaji wa nishati ndani ya dunia hii. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 800 ya Qur'ani tukufu imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuzidishie maarifa ya kumtambua Yeye yatakayozifanya thabiti na imara zaidi imani zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags