Jan 03, 2019 11:42 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 811 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass’Affat.  Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 79 hadi 82 ambazo zinasema:

سَلَامٌ عَلَىٰ نُوحٍ فِي الْعَالَمِينَ

Amani kwa Nuhu ulimwenguni kote!

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ

Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa watendao mema.

إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ

Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.

ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ

Kisha tukawagharikisha wale wengine.

Aya tulizosoma katika darsa iliyopita zilieleza kwamba Nabii Nuh (as) na wafuasi wake walioabiri pamoja naye jahazini waliokoka na gharika ya tufani kubwa na ya kutisha na hatimaye wakafika kwenye pwani ya amani salama u salimini. Aya hizi tulizosoma zinasema: Makafiri na wakanushaji wote waliokadhibisha wito na risala ya Tauhidi ya Nabii Nuh na kuyafanyia kejeli na stihzai maneno ya Mtume huyo walifikwa na adhabu ya Allah wakaangamizwa. Rehma na amani ya Allah ziwashukie waumini wote wa kila zama za historia akiwemo Nuh (as) kwa sababu alifanya juhudi kwa muda wa miaka 950 kwa ajili ya uokovu wa watu wa kaumu yake, akafikwa na tabu na maudhi mengi na akaonyesha subira na uvumilivu usio na mfano katika njia hiyo. Kuna fahari gani kubwa zaidi kwa mtu kuliko kutakiwa rehma na amani na Allah zinazoendelea kudumu baina ya walimwengu mpaka ya Siku ya Kiyama!? Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Rehma na tunza hiyo ya Allah si makhsusi kwa Nabii Nuh pekee, bali waja wote wema watapata rehma, amani na uokovu maalumu wa Allah na malipo ya thawabu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume na mawalii wa Allah waliotawafu zinawafikia sala na salamu tunazowapelekea. Kwa sababu haileti maana sala na salamu na rehma za Allah zimfikie mtu asiyeweza kusikia chochote wala kufahamu anayosemezwa. Kwa hivyo kuwasalia na kuwatakia rehma Mitume na mawalii waliopita wa Allah ni amali ya kidini na yenye thamani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kaida na utaratibu alioweka Allah ni waja wema kupata rehma na malipo ya thawabu ikiwemo papa hapa duniani. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wema huwa na taathira unapoambatana na Imani, kama ambavyo imani huwa na tija inapofuatanishwa na amali njema. Kila moja peke halijitoshelezi. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, wakati wa kuteremshwa adhabu duniani, Allah SW huwaokoa waumini ijapokuwa watakuwa wamechanganyika na makafiri.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 83 hadi 87 ambazo zinasema:

وَإِنَّ مِن شِيعَتِهِ لَإِبْرَاهِيمَ

Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake,

إِذْ جَاءَ رَبَّهُ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ

Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo safi.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَاذَا تَعْبُدُونَ

Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

أَئِفْكًا آلِهَةً دُونَ اللَّـهِ تُرِيدُونَ

Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?

فَمَا ظَنُّكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ

Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote?

Kihistoria, kilipita kipindi kirefu kutoka zama za Nabii Nuh hadi zama za Nabii Ibrahim (Alayhima-Ssalam). Lakini kwa kuwa risala na wito wa Nabii Ibrahim ulikuwa ni wa uendelezaji risala na ujumbe wa Nabii Nuh na wa njia ileile ya Tauhidi na kumwabudu Mola mmoja pekee wa haki, Qur’ani imemtaja Nabii Ibrahim kuwa ni mfuasi wa Nabii Nuh na kujenga mfungamano baina yao kama kwamba hakikupita kitambo chochote baina ya Mitume hao. Sifa muhimu zaidi ambayo aya hizi zimeitaja kuhusu Nabii Ibrahim ni ya kuwa na “moyo safi”. Safi ni kwa maana ya uzima wa kusalimika na kutakasika na aina yoyote ya uchafu na shirki na pia kwa maana ya kujisalimisha kwa Allah SW. Kwa kuwa moyo wa Nabii Ibrahim (as) ulikuwa umetakasika na kila aina ya shirki na ukafiri, Mtume huyo asingeweza kunyamazia kimya vitendo vya kishirikina na kuabudu masanamu vya jamaa na watu wa kaumu yake. Kwa hivyo alisimama kuwapa miongozo na indhari watu wake na kuwataka waitikie wito utokao kwenye fitra na maumbile yao. Aliwauliza, inakuwaje mnayapigia magoti na kuyaabudu masanamu yasiyo na uhai? Vipi mnamwacha Mola wa walimwengu na kisha mnatarajia kupata fadhila na rehma zake? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wito wa Mitume wote ni mmoja, wala hakuna tofauti na mgongano wowote baina yao. Vitu kama zama na mahali havina taathira yoyote katika usuli na misingi wadhiha ya dini za mbinguni za Tauhidi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujiepusha na kila aina ya shirki na uchafu wa kiroho na kujisalimisha kwa Allah ndiyo sifa muhimu zaidi maalumu ya Mitume na wafuasi wao. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, mwanadamu ana jukumu na masuulia kwa wenzake na inampasa afanye juhudi za kuwaelekeza kwenye uongofu jamaa na watu wake wa karibu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, waja wa kweli wa Allah hawatekwi na mazingira maovu, bali hujitahidi kutumia njia mbalimbali ili kuyabadilisha mazingira hayo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 88 hadi 92 ambazo zinasema:

فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ

Kisha akapiga jicho kutazama nyota.

فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ

Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!

فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ

Nao wakamwacha, wakampa kisogo.

فَرَاغَ إِلَىٰ آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ

Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?

مَا لَكُمْ لَا تَنطِقُونَ

Mna nini hata hamsemi?

Baada ya aya zilizotangulia kuashiria masuali ambayo Nabii Ibrahim (as) aliwauliza waabudu masanamu, aya tulizosoma zinabainisha mbinu nyingine aliyoitumia Mtume huyo mteule kuwazindua washirikina na wapotofu hao. Watu wa mji wa Babil walikuwa na mazowea na desturi ya kutoka nje ya mji kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu zao. Usiku wa kuamkia siku hiyo walimwalika Nabii Ibrahim ajiunge nao katika sherehe yao hiyo. Nabii Ibrahim alikuwa akingoja apate fursa tu ili ayavunjilie mbali masanamu yao. Kwa kuwa watu wa Babil walikuwa na itikadi kwamba, nyota zina taathira katika majaaliwa yao, ili kuwafanya wakubaliane na udhuru wake wa kutoweza kuandamana nao hadi nje ya mji, alijifanya kama anaamini vile wanavyoitakidi wao, akaziangalia nyota na kusema: Nikubalieni udhuru wangu kwa sababu kutokana na hali ya nyota, natabiri kuwa kama nitatoka nje ya mji nitaumwa; afadhali nibaki hapa hapa mjini. Bila shaka Nabii Ibrahim hakuwa na imani kama waliyokuwa nayo watu wa kaumu yake kuhusu nyota, lakini ilibidi atumie hoja watakayoikubali wao. Alaa kulli hal, kwa kutumia kisingizio hicho hakuandamana na watu kwenda nje ya mji, hivyo akafanya maandalizi ya kutekeleza kazi aliyopanga. Akiwa amebaki peke yake, aliyaendea masanamu makubwa na madogo ya watu wake na kuyaambia: Kwa nini hamuli vile mlivyoletewa na washirikina kwa nadhiri walizoweka? Mbona hamnijibu wala hamzungumzi na mimi? Kwani hawa washirikina si wanaitakidi kwamba nyinyi mna taathira katika majaaliwa yao; kwa nini basi hamwezi kufanya chochote? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika tablighi ya kutangaza njia ya haki inapasa kuzungumza na watu kwa lugha yao. Kwa hivyo inahitajika kuelewa fikra, mila na desturi za watu ili kuweza kupata mbinu sahihi ya kutumia kwa ajili ya kuwaelekeza kwenye haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuna haja ya kufanya ubunifu kwa ajili ya kupambana na fikra na mienendo potofu katika jamii na kuzitumia kwa umahiri na umakini fursa za kufanikishia lengo hilo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mitume wanatumia mantiki wadhiha na ya wazi kwa ajili ya kuikana shiriki na kulingania tauhidi, ambayo inaendana na akili, fitra na maumbile ya mwanadamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 811 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags