Jan 03, 2019 12:23 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani.  Hii ni darsa ya 814, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass’Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 106 hadi 108 ambazo zinasema:

إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْبَلَاءُ الْمُبِينُ

Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri.

وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ

Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu.

وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ

Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wakati Nabii Ibrahim (as) na mwanawe Ismail walipokuwa wameshajiweka tayari kutekeleza amri ya Allah, sauti ya mbinguni ilinadi kumhutubu Mtume huyo, ewe Ibrahim umetekeleza kwa ukamilifu wake yale tuliyokuamuru ndotoni, wala hujaonyesha ajizi au uelegevu wowote katika utekelezaji wake. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Makusudio ya Allah ya kumwamrisha Nabii Ibrahim amchinje mwanawe Ismail yalikuwa ni kumtahini Mtume wake huyo, na si kwamba Yeye Mola alitaka Ibrahim (as) amwage damu ya mtoto wake. Huo ulikuwa mtihani wa kubaini kama je Ibrahim, yuko tayari kuyavua moyoni mwake mapenzi makubwa ya mwanawe kwa ajili ya kutekeleza amri ya Allah au la? Ukweli ni kwamba lengo la Mwenyezi Mungu Mtukufu lilikuwa ni ya kuyakata na kuyachinja mapenzi ya kidunia ya moyo wa Ibrahim kwa mwanawe, si kukichinja na kukikata kichwa cha  mtoto huyo; na ndiyo maana alipoonyesha tu kuwa yuko tayari kwa hilo, Allah SW alimwamuru Mtume wake huyo amchinje kondoo katika njia ya Mola wake badala ya mwanawe Ismail, ili sunna hiyo ya Kiibrahim ibaki kuwa kumbukumbu yake katika zama zote za historia. Aidha ni kwa ajili ya kuwafanya mahujaji wa Nyumba ya Allah na watu wanaoshiriki katika ibada tukufu ya Hija, wakati wanapokuwa katika ardhi ya Mina wawakumbuke Ibrahim na Ismail kwa wao pia kuchinja katika njia ya Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuuvua moyo mapenzi ya kidunia ya mwana na mahaba ya baba kwa mtoto wake ni moja ya mitihani migumu ya Allah, ambao Ibrahim na Ismail (as) waliufuzu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuchinja katika njia  ya Mwenyezi Mungu ni moja ya sunna ya Nabii Ibrahim inayotekelezwa kila mwaka katika Sikukuu ya Mfungo Tatu yaani Idul-Adh’ha au Idul-Hajj huko Makka na katika nchi na miji mingine ya Waislamu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wakati mtu anapobakisha athari za heri na mwenendo mwema baada ya kuondoka duniani, si hasha wema huo ukalifanya jina lake litajwe na kukumbukwa milele na watakaokuja baada yake. Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 109 hadi 111 ambazo zinasema:

سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ

Amani kwa Ibrahim!

كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ

Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.

إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ

Hakika yeye ni katika waja wetu waumini.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia zilizoashiria rehma na fadhila maalumu alizopata Nabii Ibrahim (as) baada ya kufuzu mtihani aliopewa wa kuamrishwa kumchinja mwanawe na kuelezea rehma na amani za kudumu za Allah alizojaaliwa Mtume huyo katika zama zote za historia. Kisha aya zinaendelea kubainisha kwamba, rehma na fadhila hizo si makhsusi kwa ajili ya Nabii Ibrahim pekee, lakini hayo ni malipo atakayolipwa mtu yeyote yule kwa kadiri atakavyoivua nafsi yake na mapenzi ya kidunia ya mali, roho na kila akipendacho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kila mtu aliye muumini wa kweli, akajisalimisha na kuwa mja wa kweli wa Allah, naye pia kama alivyokuwa Nabii Ibrahim (as), atapata rehma na fadhila zake Mola, ambazo zitaendelea daima dawamu katika zama zote za historia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika Qur’ani, ni Mwenyezi Mungu Mwenyewe tu amewatakia Mitume wake amani na salama. Lakini kuhusu Bwana Mtume Muhammad SAW, Yeye Allah Mwenyewe na Malaika wake wanamtakia rehma na amani mtukufu huyo na anawataka waumini pia wawe kila mara wanamsalia na kumtakia rehma mbora huyo wa viumbe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, amali yoyote njema na ya heri ina malipo kwa Mola duniani na akhera. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, mfumo wa utoaji thawabu na adhabu wa Allah una kaida na kanuni maalumu; wala haufuati utashi au kuhusisha watu fulani tu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 112 na 113 ambazo zinasema:

وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَاقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ

Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema.

وَبَارَكْنَا عَلَيْهِ وَعَلَىٰ إِسْحَاقَ ۚ وَمِن ذُرِّيَّتِهِمَا مُحْسِنٌ وَظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ مُبِينٌ

Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi.

Katika aya zilizotangulia, Qur'ani tukufu imemwashiria mtoto wa Nabii Ibrahim, Ismail na kumtaja kama kijana chipukizi mvumilivu na mwenye subira. Lakini katika aya hizi tulizosoma ametajwa mtoto mwengine wa Mtume huyo, yaani Is-haq, ambaye Allah SW alimpa ahadi Nabii Ibrahim ya kumpa Utume mwanawe huyo. Ni Mtume ambaye, kama walivyo manabii wengine alikuwa mja mwema na bora wa watu wa zama zake; na kwa sababu hiyo akapata rehma na fadhila maalumu za Allah. Rehma ambazo Qur’ani tukufu imezitaja kwa kutumia neno baraka. Baraka zinajumuisha mambo yote, katika umri na maisha, watoto na kizazi pamoja na fikra na dini; kwa sababu maana ya baraka ni heri za kudumu na kuendelea. Na moja ya heri hizo za kudumu ilikuwa ni ya Mitume wa Bani Israili waliotokana na kizazi cha Nabii Is-haq (as). Tab’an Bwana Mtume SAW, yeye ametokana na kizazi cha Nabii Ismail (as). Kisha sehemu ya mwisho ya aya tulizosoma inasema: Bila shaka si watoto wote wa kizazi cha Is-haq walikuwa watu wema, lakini baadhi yao walikuwa madhalimu na waovu wafanya madhambi. Hili ni mojawapo ya mambo yaliyo kwenye irada, hiyari na chaguo la mwanadamu mwenyewe, kwamba pamoja na kutoka kwenye migongo na vizazi vya waja wema kiurithi, anaweza kuchagua kwa hiyari yake kufuata njia potofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika koo za Mitume yumkini wakawemo ndani yake watoto wabaya. Kuwa na mfungamano wa kinasaba au kiukoo na Mitume au waja wema na wateule hakumaanishi kwamba mtu mwenye mfungamano huo lazima ataongoka tu. Inawezekana baba akawa mja mteule wa Allah, lakini mtoto wake akaiacha haki na kufuata upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, dua ya Nabii Ibrahim kuhusu watoto na kizazi chake ilikuwa sababu ya kupata fadhila na rehma nyingi za Allah wanawe Ismail na Is-haq pamoja na vizazi vya baada yao. Kwa hivyo na sisi pia tuombe dua kila mara Allah awajaalie watoto na vizazi vyetu vijavyo viwe vya waja wema na wa heri. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 814 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuongoze sisi na vizazi vyetu katika njia ya haki na uongofu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags