Jan 05, 2019 08:33 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 817, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 133 hadi 136 ambazo zinasema:

وَإِنَّ لُوطًا لَّمِنَ الْمُرْسَلِينَ

Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume.

إِذْ نَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ أَجْمَعِينَ

Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,

إِلَّا عَجُوزًا فِي الْغَابِرِينَ

Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma.

ثُمَّ دَمَّرْنَا الْآخَرِينَ

Kisha tukawaangamiza wale wengineo. 

Baada ya aya za darsa kadhaa zilizopita za sura yetu hii ya Ass 'Affat kuzungumzia habari za baadhi ya Mitume, aya hizi tulizosoma zimeendeleza maudhui hiyo kwa kuzungumzia kwa muhtasari habari za Nabii Lut (as) na kaumu yake. Watu wa kaumu hiyo walikuwa wakiishi kaskazini mwa eneo la Hijaz katika njia inayotoka Makka kuelekea Sham. Kila siku misafara ya biashara ilikuwa ikipita njia hiyo na kando ya maskani na nyumba zao. Kwa mtazamo wa historia na kwa mujibu wa aya za Qur'ani, Nabii Lut (as) aliishi katika zama za Nabii Ibrahim (as) na alikuwa mlinganiaji na mfikishaji kwa watu mafundisho na hukumu za dini ya Mtume huyo. Aya hizi zinaashiria sehemu moja ya matukio ya mwisho yaliyowatokezea watu wa kaumu ya Nabii Lut na kueleza kwamba: Wakati adhabu ya Mwenyezi Mungu ilipowateremkia watu hao waovu na wafanya maasi, wale waliokuwa wamemwamini Mtume huyo, ambao wakihesabika kuwa ni ahali zake, walipata habari ya kushuka kwa adhabu hiyo. Watu hao walifuatana na Nabii Lut kwa kutoka nje ya mji, hivyo wakaokoka. Lakini waliobakia, ambao walikuwa watu waovu na waasi hawakupata habari ya adhabu hiyo. Walibaki majumbani mwao, wakafikwa na adhabu ya Allah iliyowashukia kutokea mbinguni na ardhini na kuwafanya waporomokewe na kufukiwa na vifusi vya nyumba zao. Kisha aya zinaendelea, kwa kuashiria kwamba kutokana na mke wa Nabii Lut kushirikiana na watu wafanya madhambi wa kaumu hiyo na kuridhia maovu yao, yeye pia alipatwa na hatima sawa na ya watu hao na wala uhusiano wake wa kifamilia haukuweza kumuokoa na adhabu. Kwa sababu kupata rehma au kufikwa na ghadhabu za Allah kunategemea jinsi mtu anavyochunga misingi na thamani za dini na akhlaqi; mafungamano ya kifamilia na kiujamaa hayana nafasi yoyote katika jambo hilo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuzungumziwa habari za kaumu zilizopita ndani ya Qur'ani, madhumuni yake hasa ni kubainisha utaratibu wa kudumu alioweka Allah katika historia ili kutoa ibra na mazingatio kwa vizazi mbalimbali vya wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hisabu ya Mitume ni tofauti na ya wake na watoto wao, na wala uhusiano wao wa kifamilia sio unaoainisha hatima zao. Kwa maneno mengine ni kwamba, mafungamano yao hayo pekee hayawezi kuwa sababu ya wao kuokoka. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, waumini na wafuasi wa fikra na matendo ya Mitume, hata kama watatokana na kaumu na asili nyingine za watukufu hao watahesabika kuwa ni watu wao na wa nyumba zao. Na kinyume chake pia ni kwamba, ikiwa mtoto na mke wa Mtume watakuwa si waumini, hawatohesabika kuwa ni watu wa nyumba ya Mtume huyo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 137 na 138 ambazo zinasema:

وَإِنَّكُمْ لَتَمُرُّونَ عَلَيْهِم مُّصْبِحِينَ

Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,

وَبِاللَّيْلِ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?

Katika maelezo ya aya zilizotangulia tulisema kuwa, watu wa kaumu ya Nabii Lut (as) walikuwa wakiishi katika eneo la njia inayopita misafara ya biashara inayotoka Makka kuelekea Sham. Aya tulizosoma zinasema: Baada ya kaumu hiyo kushukiwa na adhabu, watu waliokuwa wakipita kando ya mji huo walikuwa wakijionea namna gani wakazi wake walivyokufa wakiwa wamefukiwa na kufunikwa na vifusi. Watu wa kaumu ya Nabii Lut walikuwa wakilawitiana. Miongoni mwao walikuwemo pia watu ambao waliyanyamazia kimya machafu na maovu hayo, na wala hawakuchukua hatua ya kupambana na dhambi hiyo kubwa. Kwa hivyo wao pia walifikwa na adhabu. Kwa ujumla ni kwamba, hisia za kuiona liwati kuwa ni uovu na dhambi nzito zilikuwa zimewatoka watu wa kaumu ya Nabii Lut. Walifikia hadi hata wakamtisha Mtume wao huyo aliyekuwa akiwaonya na kuwatahadharisha na mwisho mbaya wa maovu hayo, na badala yake akawa anawashajiisha kufunga ndoa ili kukidhi matamanio yao ya kijinsia kwa njia ya kimaumbile. Ajabu ni kwamba baada ya kupita miaka elfu kadhaa tangu ilipoangamizwa kaumu hiyo, wanadamu wa leo wanaojinasibu kuwa wameendelea na kustaarabika na kuzituhumu dini kuwa zinaabudu na kufuata mambo ya khurafa na yaliyopitwa na wakati, wao wenyewe wametumbukia kwenye lindi la mwenendo huo duni, mchafu na wa kijahilia. La ajabu zaidi ni kwamba, kwa mtazamo wa hao wanaojigamba kuwa wanafuata ustaarabu mpya, kujuzisha na kuhalalisha kisheria uchafu na uovu huo ndani ya nchi zao, kwao wao ni alama na kielelezo cha maendeleo katika demokrasia na haki za binadamu. Inapasa tuzingatie nukta hii, kwamba haki halisi za binadamu, zinaendana na mahitaji ya kimaumbile ya mwanadamu na zinakubaliana na maumbile yake ya kimwili. Kwa mtazamo wa kifiziolojia, viungo vya sehemu za siri vya mwanamke na mwanamme vimeumbiwa mwenza wa jinsia tofauti, na wala havina mlingano wowote kimaingiliano na mwenza wa jinsia moja. Kwa hivyo hali yoyote iliyo kinyume na hiyo, inahalifu hali ya fiziolojia ya mwili wa mtu na mahitaji yake ya kimaumbile na kukinzana na mfumo wa uumbaji. Yumkini wako wanaoweza kutoa hoja kwa kusema: Lakini baadhi ya watu wanavutiwa zaidi na wenzao wa jinsia moja, hivyo si sawa kuwanyima kile kinachopendeza nafsi zao. Jawabu ya hoja hiyo iko wazi, nayo ni kwamba, je, katika masuala mengine ya hamu za kimwili na kinafsi kipimo kiwe ni kufuata wanayoyapenda watu? Mathalani turuhusu utumiaji madawa ya kulevya ambao unawavutia watu wengi, na kuufanya jambo linalojuzu na halali kisheria?! Kwa maneno mengine ni kuwa, sheria haiwezi kufuata utashi na hamu za watu; bali ni kinyume chake; kwamba moja ya wajibu wa sheria ni kukabiliana na matashi yasiyo ya kimaumbile. Kwa kutoa mfano, leo hii kuna baadhi ya watu wanasema, wanavutiwa na kupendezwa kuwa na maingiliano ya kimwili na baadhi ya wanyama; kama ni hivyo, tujuzishe kitendo hicho kiwe halali kisheria?! Ilhali watu wote wakiwemo watetezi wa haki za wanyama wanapinga jambo hilo, wakisema si la kawaida na linapingana na mfumo wa maumbile. Kwa hivyo hamu na utashi wa baadhi ya watu kwa jambo fulani, si hoja ya kulifanya jambo hilo liwe sahihi na la mantiki na wala haiwezi kuwa kigezo na kipimo cha kutungia sheria. Alaa kulli hal, japokuwa mwanadamu wa leo amepiga hatua kubwa katika nyenzo za maisha, kama mavazi, nyumba na magari pamoja na suhula za burudani na starehe lakini kwa masikitiko ni kwamba katika mahusiano ya kiutu hajapiga hatua ya maana, bali katika baadhi ya mambo ameporomoka na kurudi nyuma kabisa. Ndoa za jinsia moja ni mfano mmojawapo wa mambo hayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tupate ibra na mafunzo kwa ajili ya maisha yetu ya leo kwa kusafiri na kutembelea maeneo ya kale na ya kihistoria yaliyoachwa na kaumu zilizopita au kwa kutalii na kusoma habari za watu wa kaumu hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mambo ya kutupa ibra na mazingatio ni mengi. Tatizo ni kuwa tunayapita bila ya kuyajali na wala hatutafakari ili kupata ibra na mafunzo ndani yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 817 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuhifadhi na mienendo miovu na michafu iliyozagaa katika zama hizi na kutuwezesha kushikamana ipasavyo na mafundisho ya dini yake tukufu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags