Jan 06, 2019 03:05 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 821, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 174 hadi 177 ambazo zinasema:

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ حَتَّىٰ حِينٍ

Basi waache kwa muda. 

وَأَبْصِرْهُمْ فَسَوْفَ يُبْصِرُونَ

Na watazame, nao wataona.

أَفَبِعَذَابِنَا يَسْتَعْجِلُونَ

Je! Wanaihimiza adhabu yetu? 

فَإِذَا نَزَلَ بِسَاحَتِهِمْ فَسَاءَ صَبَاحُ الْمُنذَرِينَ

Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria ushindi wa haki dhidi ya batili na wafuasi wa Mitume dhidi ya makafiri na wakanushaji haki. Aya hizi tulizosoma hivi punde zinaendeleza maudhui hiyo kwa kumhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba: Jitenge nao na waache kwa muda kama walivyo washirikina na makafiri, ili ima wazinduke na kurejea kwenye haki au Mwenyezi Mungu mwenyewe awachukulie hatua kwa kuwateremshia adhabu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Wao, karibuni hivi wataona matokeo ya amali zao, na waumini watashuhudia pia kushindwa na kudhalilishwa kwa watu hao. Tab'an katika hali ya kutoamini wanayoambiwa, makafiri huwa kila mara wanakuuliza wewe Mtume kwa kejeli na stihzai: Hiyo adhabu unayoahidi, itakuja wakati gani? Wanasema hayo utadhani wana haraka ya kushukiwa na adhabu. Ilhali, wakati adhabu itakaposhuka, hakika itawabainikia; lakini kuitambua haki wakati huo hakutakuwa na faida yoyote tena kwao wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kujitenga na wapinzani kwa njia ya kuwasusia au kuwahofisha ni moja ya mbinu iliyokuwa ikitumiwa na Mitume. Katika mfumo wa malezi na urekebishaji watu wabishi na wakaidi, baadhi ya wakati inatakiwa uwasusie na kuwaacha kwa muda kama walivyo, huenda asaa wakatanabahi na kurejea kwenye njia ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwasusia wapinzani na kujitenga nao inapasa kufanyike kwa muda tu na kwa njia ya mantiki (kusiwe kwa kudumu au kwa madhumuni ya kuwakomoa na kuwalipizia kisasi), ili isije ikawa sababu ya kuwafungia njia ya kujirekebisha na kurejea kwenye haki watu wakaidi na waliokengeuka njia ya haki. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, wakanushaji na wanaoifanyia dini inadi, wataonja machungu ya kushindwa njama na uadui wao papa hapa duniani, ili liwe somo na ibra kwa wengine. Na waumini watashuhudia pia mwisho na hatima ya watu hao.

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 178 hadi 182 ambazo zinasema:

وَتَوَلَّ عَنْهُمْ حَتَّىٰ حِينٍ

Na waache kwa muda.

وَأَبْصِرْ فَسَوْفَ يُبْصِرُونَ

Na tazama, na wao wataona.

سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ

Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia.

وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ

Na amani kwa Mitume. 

وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Katika kutilia mkazo yale yaliyoelezwa katika aya zilizotangulia, aya hizi zinamhutubu tena Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini ya kwamba: Hao wanaofanya ubishi na ukaidi dhidi ya haki na hawako tayari kuisikiliza na kuikubali, waache kama walivyo kwa muda na usubiri Allah SW awalipe malipo ya amali zao. Aya zinazofuatia na ambazo ndizo aya za mwisho za sura hii ya Ass 'Affat zinasema: Izza, nguvu na qudra hasa ni za Mola wako Mlezi, na mwisho wa yote waumini ndio watakaokuwa na izza; na makafiri na washirikina wataionja ladha ya udhalili. Kama waumini watatawakali kwa Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye Mola pekee, wawe na hakika kwamba Allah atawawezesha kuwashinda makafiri. Yeye ni Mola aliyetakasika na kila nakisi na udhaifu na Mweza wa lolote lile atakalo. Historia imeshuhudia jinsi Allah SW alivyowahami na kuwasaidia kila mara Mitume wake na kuwateremshia amani na rehma zake. Kwa sababu hiyo inapasa kumhimidi na kumshukuru Mola huyo Mweye izza na adhama na mwendeshaji wa ulimwengu kwa hekima na tadbiri. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ahadi za Mwenyezi Mungu kuhusu adhabu za wanaoifanyia inadi haki ni ya hakika na haina shaka; na wala haifai muumini kuwa na shaka juu ya hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa izza ya kudumu na kuendelea ni ile itokayo kwa Allah Azza wa Jalla; na wale walio waja wake wa kweli watadumu kuwa na izza hapa duniani. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mola wa walimwengu wote ndiye pekee anayestahiki kuhimidiwa na kushukuriwa, kwa sababu yeye ni Mmliki na Mwendeshaji wa kila kitu katika ulimwengu wa viumbe na ndiye asili ya mazuri yote na ukamilifu wote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 821 ya Qur’ani imefikia tamati na ndiyo inayotamatisha pia tarjumi na maelezo ya sura hii ya 37 ya Ass 'Affat. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waelimikaji na watekelezaji wa yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags