Jan 09, 2019 07:46 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu; miaka 39 ya kusimama kidete dhidi ya mfumo wa kibeberu

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi, ambacho ni kipindi cha tangu kurejea Imam Khomeini kutoka uhamishoni hadi kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kipindi chetu cha leo kitajadili kusimama kidete mapinduzi haya kwa miaka 39 dhidi ya mfumo wa kibeberu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliopatikana 1979 ulihitimisha ubeberu na satwa ya Marekani kwa taifa hili lililokuwa chini ya utawala kibaraka wa Shah. Kwa maneno mengine ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalifungua ukurasa mpya wa taifa hili na kuweka hatima na majaliwa ya taifa hili katika njia mpya ya izza, heshima na utukufu. Tukio hili kubwa na adhimu liliifanyya Marekani na washirika wake ambao walikatwa mikono yao na kupoteza maslahi yao hapa nchini, waanzishe njama za kila upande za kutoa pigo dhidi ya mfumo mchanga wa Jamhuri yay Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo njama za Wamagharibi iwe ni katika kipindi cha vita vya kulazimishwa Iran vilivyoanzishwa na dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein au iwe ni katika zama za hatua za chuki na adawa baada ya vita hivyo, yote hayo hayakuweza kuwafungulia Wamagharibi mlango wa kurejea tena hapa nchini na kufanya watakavyo. Kama anavyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kwamba ni kuwa: Kukithiri vitisho dhidi ya taifa hili ni ishara ya uwezo na nguvu za mfumo wa Kiislamu, kwani kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingelikuwa na taathira kubwa, basi wanaolitakia mabaya taifa hili wasingehaha namna hii na kutafuta kila njia ili kukabiliana na mfumo unaotawala hapa nchini.

Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Hivi sasa inapita miaka 39 tangu Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapa nchini Iran mwaka 1979 kwa uongozi wenye busara na hekima wa Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini MA, na mapinduzi haya yangali ni kivutio na kiigizo kikubwa cha mataifa yaliyo macho, wapigania uhuru, mamlaka ya kujitawala, heshima na utukufu.

Noam Chomsky, mwanadishi mashuhuri na mwananadharia wa Kimarekani anaamini kuwa, uadui, njama na upinzani wa Marekani na madola ya Magharibi dhidi ya Iran sababu na chimbuko lake ni kutokubali kusalimu amri Iran mbele ya ubeberu na ukoloni.

Chomsky anasema:…Madhali Iran itaendelea kubakia kuwa ni dola lenye kujitegemea na kutopiga magoti mbele ya ubeberu wa Marekani, basi uadui na upinzani wa Marekani nao utaendelea kushuhudiwa.

Kwa hakika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwapatia walimwengu mapinduzi ya kwanza yaliyofanikiwa ya kisiasa na Kiislamu ili Waislamu na mataifa yaliyonyongeshwa na kudhulumiwa katika kona mbalimbali za dunia yaweze kunufaika na matunda yake.

Akihutubia katika mkutano wa 10 wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Mwamko wa Kiislamu, Katibu wa jumuiya hiyo alisema:

…Hii leo kwa baraka za Uislamu na thamani pamoja na matukufu ya Kiislamu, mwamko wa Kiislamu unaonekana dhahiri shahiri na kuvuka mtihani katika kiwango cha kieneo. Sauti za juu za malalamiko na kuonyesha chuki dhidi ya Uistikabri na mabeberu wa dunia, ni matunda ya kwanza na ya haraka zaidi ya mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati.  

Miongoni mwa picha za kihistoria za Mapinduzi ya Kiislamu

 

Kwa hakika, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran sambamba na kuwa na taathira kubwa katika mahusiano ya kijamii ya taifa hili na thamani zinazotawala katika jamii ya Wairani, yameleta mtetemeko na hali ya kulegalega kwa mfumo unaotawala ulimwenguni pamoja na hali inayoshuhudiwa hivi sasa na hivyo kuleta mabadiliko na mageuzi ya kimsingi. Si hayo tu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yametoa changamoto kubwa kwa kanuni na vigezo visivyo vya kiadilifu vinavyotawala katika mahusiano ya kimataifa na mfumo wa dunia.

Akihutubia katika moja ya mikutano yake na wanachuo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu alisema:

...mfumo wa kibeberu maana yake ni mfumo wa kambi mbili duniani ambapo, kambi ya kwanza ni ya kibeberu na kambi nyingine iko chini ya ubeberu.

Katika hotuba yake nyingine aliyotoa katika hafla ya kumuidhinisha Rais wa awamu ya kumi na mbili wa Iran, Ayatullah Khamenei alisema:

…kizazi kipya na vijana wa nchi hii, hawakukishuhudia kipindi cha kabla ya Mpainduzi ya Kiislamu, lakini nafasi muhimu ya wananchi katika utawala ni matunda makubwa sana ambapo Imam Khomeini aliweza kuifanya bahari ya wananchi ifanye harakati na hivyo akaleta mabadiliko ambayo yalihitimisha utawala wa Kifalme, wa kurithishana na uingiliaji wa madola ajinabi wa miaka na karne nyingi. Akaifanya harakati ya nchi kuelekea upande wa wananchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anaashiria njama mbalimbali katika kipindi cha miaka iliyopita dhidi ya taifa hili kwa kusema:

…Katika kipindi cha miaka yote hii baadhi ya watu kama viongozi wa sasa wa Marekani walilifanyia uadui wa wazi wazi taifa la Iran na njama za wengine zilikuwa kama za kuficha makucha ndani ya glovu za mahameli yaani siasa za kuuma na kupuliza. Lakini mipango yote hiyo haijawa na natija ghairi ya kuwafanya wananchi na viongozi wa taifa hili wajiamini zaidi na kutafuta njia za kukabiliana na njama za adui.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Wapenzi wasikilizaji, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliyafanya madola ya kibeberu yahangaike na kuhaha huku na kule kutokana na sababu kadha wa kadha. Kwa hakika mapinduzi haya kabla ya kila kitu yameonyesha kwamba, wananchi wa taifa fulani hata wakiwa mikono mitupu wanaweza kuwa chanzo na chimbuko la mageuzi makubwa hata katika mahesabu ya madola makubwa ulimwenguni.

Manuchehr Muhammadi ni mweledi na mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati yeye anaamini kuwa:

…Kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa mwanzo wa vita vikubwa baina ya Iran na Marekani. Jamhuri ya Kiislamu ukiwa mfumo wa kiadiolojia, ukaliweka suala la kupambana na ubeberu na Uistkbari katika ajenda zake kuu.

Kwa hakika Wamarekani walifanya kila wawezalo mwanzoni tu mwa Mapinduzi ya Kiislamu wakitumia njama mbalimbali ili kuyasambaratisha mapinduzi haya. Hadi sasa kumetekelezwa njama 17 dhidi ya Iran ambazo ni mjumuiko wa mapinduzi matatu, matukio matano ya uchochezi wa kikaumu, kuanzishwa makundi manne ya kigaidi kwa ajili ya kuwaua viongozi wa Iran, vita viwili na fitina tatu kubwa dhidi ya taifa hili la Kiislamu.

Licha ya njama zote hizi, lakini muelekeo wa sasa wa Mashariki ya Kati uko katika mhimili wa muqawama na mapambano ya wananchi na athari ya hili linaonekana wazi katika kushindwa mtawalia Marekani pamoja na vibaraka wake katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Alfajiri Kumi za kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini umefikia tamati. Msikose kujiunga nasi katika vipindi vyetu vingine.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags