Jan 15, 2019 06:44 UTC
  • Kongamano la miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu lililofanyika mjini Amman, Jordan
    Kongamano la miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu lililofanyika mjini Amman, Jordan

Sehemu ya Tano: Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani. Msikilizaji mpenzi wa Radio Tehran, ni matumaini yangu kuwa hujambo popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha tena kusikiliza kipindi hiki kinachokujia kila wiki, siku na saa kama hii, kinachozungumzia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii.

Endelea kuwa nami hadi mwisho wa mazungumzo yetu, ili kuweza kufaidika na yale niliyokuandalia katika mfululizo huu wa tano, tukiwa tunaendelea na maudhui yetu ya kubainisha sifa na mambo yanayoyapambanua na kuyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa yaliyotokea duniani.

*******

Tofauti nyingine muhimu zaidi iliyopo katika ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa duniani ni katika matokeo na taathira za mapinduzi hayo. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hayakuwa na taathira za ndani tu, bali yalikuwa na taathira pia kwa eneo na ulimwengu kwa ujumla, na hata taathira zenyewe pia zilikuwa tofauti. Ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ulikuwa ni kupigania uhuru na kupinga udikteta wa ndani, kupigania kujitawala na kupinga ubeberu wa nje dhidi ya Iran, sambamba na kuutumia Uislamu kwa ajili ya kuasisi muundo wa kisiasa unaodhamini uhuru, kujitawala na uadilifu. Ujumbe huo ulisikika katika mataifa mengi hususan mataifa manyonge duniani na kuwa chachu ya kuibuka vuguvugu la harakati na mapambano kadhaa katika upeo wa kieneo na kimataifa katika nchi kama Tunisia, Algeria, Morocco, Nigeria, Lebanon, Misri, Bahrain na nchi nyingine nyingi. Kwa kufuata kigezo cha mapinduzi ya wananchi wa Iran, wananchi wa nchi nyingi za Kiislamu walikuwa na mchango muhimu katika kuanzishwa harakati mbali mbali, ambazo ziliwatia hofu watawala wa zama hizo katika nchi zao pamoja na madola makubwa ya dunia, kwa sababu vuguvugu jipya la Kiislamu lililojitokeza, lilitoa changamoto kwa nidhamu na mfumo uliokuwa umetandikwa zama hizo katika eneo la Magharibi ya Asia.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika historia ya zama hizi ya Ulimwengu wa Kiislamu yalikuwa nukta ya kilele cha mabadiliko katika kuhuisha Uislamu na kurejea Waislamu kwenye utambulisho wao wa Kiislamu. Japokuwa utambulisho wa Kiislamu, ndio uliokuwa sababu ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, lakini kwa kuzingatia sifa yake ya kuwa ni harakati yenye wigo mpana wa ulimwengu mzima, kwa mtazamo mwengine, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulikuwa sababu ya kuhuika utambulisho wa Kiislamu na kujitokeza pia vuguvugu na harakati mbali mbali katika Ulimwengu wa Kiislamu. Na sababu ni kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa yamefungamana na harakati pana na jumuishi ya ulimwengu mzima, ambayo lengo lake ni kuhuisha roho ya Kiislamu, kuuamsha umma na kuuelekeza kwenye ukamilifu halisi wa jamii ya Kiislamu. Madhihirisho ya taathira hiyo yanaweza kushuhudiwa katika kuchipua na kushamiri harakati za Kiislamu sambamba na kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya Iran yakiwemo ya kujitengezea satalaiti na kuzirusha anga za juu bila ya msaada ya madola ya kigeni, yanawakasirisha sana maadui wa taifa la Iran

 

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ulikuwa sababu ya kuanza mapigano kati ya madola ya kitaghuti na tawala za kijabari kwa upande mmoja, na wananchi wa mataifa yanayonyongeshwa, yanayopigania uhuru na ukombozi kwa upande mwingine; na ni kwa sababu hiyo mapinduzi hayo yakawa kigezo na mwongozo kwa wapigania uhuru na ukombozi wote duniani katika nchi za Waislamu na nchi nyinginezo pia.

Baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, harakati za mwamko wa Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu, ziliingia kwenye awamu na marhala mpya kwa kujitokeza mabadiliko makubwa katika jiografia ya Kiislamu, ya ukomavu wa kifikra hususan miongoni mwa wananchi wa kawaida na matabaka yaliyokosa mwamko. Kiasi kwamba mwamko wa Kiislamu ulitoka kwenye hali ya harakati legevu ya kujihami tu na kupelekea kupata nguvu na kuimarika utambulisho mmoja wa kisiasa wa Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu unaofuata mafundisho asili ya Kiislamu. Kudhihiri mwamko wa Kiislamu na harakati zenye mielekeo ya Kiislamu huko Palestina, Lebanon, Uturuki, Misri, Bahrain, Libya, Yemen, Sudan, Pakistan, Kusini Mashariki ya Asia na maeneo mengine ya Ulimwengu wa Kiislamu, yote hayo ni ishara za wazi za kuhuika utambulisho huo wa Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu kulikosababishwa na athari za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Katika upande mwingine, hakuna shaka kwamba, kulipa sura ya Kiislamu suala la Palestina, ni moja ya madhihirisho makubwa ya taathira za Mapinduzi ya Kiislamu katika mahusiano na mabadiliko yaliyojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu, kwa ajili ya kuimarisha na kuupa sura moja utambulisho wa Kiislamu. Imam Khomeini (MA), kiongozi mkuu na jemadari wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran alikuwa akilizungumzia suala hilo kwa kusema: “Bila sisi kurejea kwenye Uislamu, bila kurejea kwenye Uislamu wa Mtume wa Allah, matatizo yetu yatabaki pale pale. Hatutaweza kutatua kadhia ya Palestina, wala ya Afghanistan wala za sehemu nyinginezo…. Inapasa kujifunza mafundisho ya Uislamu; na kama Uislamu ulivyoamrisha, waumini wa sehemu zote ni ndugu; na umeamrisha kwamba, shikamaneni na Kamba ya Allah na wala msifarikiane. (Sahifa ya Nuru, Juzuu ya 12, Ukurasa 282).

Sehemu ya maendeleo makubwa ya Iran katika kipindi cha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Kwa kuihuisha nafasi ya Uislamu ulimwenguni, hasa katika Ulimwengu wa Kiislamu na kuunda serikali inayotokana na mafundisho asili ya Kiislamu, ambayo kwa kushikamana na thamani za Kiislamu iliweza kuyapatia majibu mahitaji ya zama hizi, Mapinduzi ya Kiislamu yaliuarifisha na kuutambulisha Uislamu duniani kuwa ni dini iliyokamilika na ya ulimwengu mzima, yenye uwezo wa kuunda utawala na kuongoza jamii. Na hii ilikuwa ni katika hali ambayo, Ulimwengu wa Magharibi ulikuwa ukiamini kwamba, jitihada za kutaka kuunda utawala wa Kiislamu katika zama hizi haziwezi kuwa na tija yoyote; kwa sababu wao wakiitakidi kwamba, katika mafanikio makubwa kabisa uliyofikia Uislamu, yaani mnamo karne 14 nyuma, uliweza kuonyesha mbinu nzuri tu za kiutawala, lakini katika zama za sasa hauna uwezo wa kuendesha utawala wala kuyapatia majibu mahitaji ya zama hizi pamoja na mabadiliko yake ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwathibitishia watu wote kuwa, suala la kurejea kwenye Uislamu si dhana na nadharia tupu; bali ni jambo linaloweza kuthibiti kivitendo. Kwa kueneza na kutangaza malengo matukufu ya Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalionyesha kuwa, licha ya kupita muda mrefu na kupatikana ustawi mkubwa kwa mfumo wa Usasa, dini za mbinguni, na hasa dini ya Uislamu si tu haijafika ukingoni; lakini ingali ni njia bora zaidi ya kuwaokoa wanadamu na dhulma na uonevu.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya tano ya kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii, imefikia tamati. Usiache kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika sehemu ya sita ya mfululizo huu, ambapo tutaendelea kuzungumzia mambo yanayoyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa duniani. Nakushukuru kwa kunisikiliza na nakutakia usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu

 

Tags