Jan 30, 2019 08:17 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii (7)

Sehemu ya Sita: Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani. Msikilizaji mpenzi wa Radio Tehran, ni matumaini yangu kuwa hujambo popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha tena kusikiliza kipindi hiki kinachokujia kila wiki, siku na saa kama hii, kinachozungumzia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii. Endelea kuwa nami basi hadi mwisho wa mazungumzo yetu, ili kuweza kufaidika na yale niliyokuandalia katika mfululizo huu wa sita,

Kutokana na muelekeo wake wa kuzingatia umaanawi na kuhuisha dini na mielekeo ya kidini, katika dunia ambayo ilikuwa imetawaliwa na kuenea kwa kasi fikra za ulahidi, kujiweka mbali na Mungu, kumfanya mtu msingi wa kila kitu na kuvutiwa baadhi ya nchi duniani na mfumo wa kifikra na kisiasa wa Usekulari, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu si tu uliweza kubadilisha mahubiri ya kidini nchini Iran, lakini pia ulileta mazingira mapya, yaliyoonyesha kuwa, dunia inaingia katika kipindi tofauti na vipindi vilivyopita na zama zingine kabisa zenye hali za kipekee kidini na kimaanawi. Ukweli ni kwamba, katika dunia iliyokuwa imejaa nadharia za kimaada, Mapinduzi ya Kiislamu, mbali na kutoa mwanga wa kudhihirisha nguvu za umaanawi na itikadi za kidini na kimadhehebu kwa wafuasi wa dini nyinginezo, yaliwarejesha pia Waislamu kwenye dini yao ya Uislamu. Kwa kuasisiwa mfumo wa kisiasa nchini Iran unaotokana na Uislamu, Waislamu duniani walipata utambulisho mpya na kujihisi wana izza na shakhsia ya Kiislamu. Taathira hiyo ilizima njama za miaka na miaka zilizofanywa na madola ya kikoloni na kiistikbari za kuwadunisha na kuwadhalilisha Waislamu; na katika ulimwengu mzima, vuguvugu la kuvutiwa na Uislamu lilipata kasi na kuenea; na hata wanaharakati wa Kiislamu katika baadhi ya nchi walipiga hatua mpaka ya kukaribia kuunda serikali za Kiislamu katika nchi zao.

Katika taathira nyingine za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, tunaweza kuashiria pia sifa ya kuwa kwake mwito wa ulimwengu mzima, ambapo upeo wa mapinduzi hayo umevuka mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mapinduzi hayo yalimtunukia mwanadamu wa zama hizi mfumo wa kisiasa ambao msingi wake ni kupigania uadilifu, kumuelekea Mwenyezi Mungu na kushikamana na umaanawi; na kinyume na mapinduzi kama ya Ufaransa na Urusi, ambayo yalimpa mwanadamu bishara ya kupata saada na fanaka kwa kutegemea idiolojia ya kubuni, Mapinduzi ya Kiislamu yaliitangaza dini na idiolojia ya kidini, kama kigezo bora kinachotekelezeka na kinachoendana na maumbile ya mwanadamu. Taathira ya mapinduzi hayo ilisababisha kutokea mageuzi mengi kwa upande wa nadharia na vitendo, na mabadiliko kimataifa katika upeo wa kieneo na ulimwengu mzima kwa ujumla. Kutokana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa ni harakati pana ya kidini na inayoendana na fitra na maumbile safi ya mwanadamu, yaliweza kudhihirisha umuhimu wa ushawishi wa dini katika uga wa kimataifa na kuzitamadunisha thamani na tunu za kidini katika uga wa ndani, kieneo na kimataifa.

Imama Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliweza kuwa mwasisi wa anga ya mahubiri yaliyoleta utamaduni mpya katika mahusiano ya kimataifa. Mahubiri ambayo yalileta utawala wa kidini unaotokana na ridhaa ya wananchi, yakafufua fikra ya Kiislamu, ustaarabu wa Kiislamu katika upeo wa kimataifa, yakazipa nafasi kuu harakati za kiutamaduni, yakaimarisha harakati mpya za kijamii na kueneza utamaduni wa kupambana na uistikbari na kupigania kujitawala na kujitegemea. Kwa kutegemea ustawishaji wa utamaduni wa ndani na mabadilishano ya kiutamaduni na kiustaarabu nje ya nchi, Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kuanzisha anga ya mazungumzo na dunia ya nje kwa msingi wa kutaka kuleta mageuzi na marekebisho katika muundo na utendaji wa mfumo wa kimataifa na miundomsingi ya kieneo. Na kwa utaratibu huo, mapinduzi hayo yakaleta uono mpya katika mahusiano ya kimataifa uliojikita katika mageuzi ya uwezo na nguvu na mabadiliko ya aina ya wadau wake. Kwa kutoa mfano, katika uga wa siasa za nje, moja ya matunda na mafanikio muhimu zaidi yaliyopata Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kueneza mahubiri ya kupigania kujitawala na kujitegemea na kukataa kuwa na utegemezi kwa madola makubwa.

Kwa hakika tunaweza kusema kwamba, athari muhimu zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika uga wa uhusiano wa kimataifa ilikuwa ni kuupangua mfumo wa kambi mbili kuu uliokuwa ukitawala zama hizo. Tukichunguza fikra na mitazamo ya Mapinduzi ya Kiislamu itatudhihirikia kuwa, kwa upande wa kimataifa, kutokea mapinduzi ya Iran lilikuwa jibu na radiamali dhidi ya muundo wa mfumo wa kimataifa wa kambi mbili na hatua ya kuleta mabadiliko na mageuzi katika namna ya ugawanaji wa nguvu na ushawishi kati ya nchi mbalimbali. Na kwa kuzingatia kwamba mapinduzi ya Iran yalikuwa dhidi ya ukoloni na muundo uliokuwepo, tokea lilipoanza vuguvugu lake, yalisimama kupinga ushawishi na uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya Iran, na yakiitakidi kwamba utawala wa Kipahlavi ni serikali kibaraka na isiyokubaliwa na wananchi. Mapinduzi ya Iran yaliuangusha utawala wa Shah na kukata uingiliaji na ubeberu wa Marekani dhidi ya Iran; na hata baada ya kujitokeza ombwe, kwa kuhitimishwa ubeberu wa Marekani, mapinduzi hayo hayakutoa mwanya kwa kambi kuu ya pili, yaani Urusi ya zamani ya kuwa dola mbadala la kuingilia masuala ya ndani ya Iran. Mbali na hayo, kwa kutangaza kaulimbiu ya "Si Mashariki, Si Magharibi", Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kuasisi mfumo unaozingatia usawa baina ya nchi na tawala zote, na kudhaminiwa haki za kidini na kiutu za mataifa katika mfumo wa kimataifa. Na kwa kuhuisha uwezo na suhula zilizosahaulika za mataifa yasiyo na mfungamano na madola makubwa, sambamba na kupinga kunyongeshwa na kuhofishwa na uistikbari, mapinduzi hayo yalinuia kukata mizizi ya utegemezi wa mataifa kwa madola makubwa kimataifa.

Maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Kwa wakati mmoja, Mapinduzi ya Kiislamu yalisimama kupambana katika medani mbili za kupinga udikteta wa ndani na ukoloni wa nje na kukataa utegemezi. Na hilo ndilo lililopelekea kujitokeza utamaduni wa kupigania kujitawala na kupigania uhuru miongoni mwa matabaka mbali mbali ya watu, nchi na harakati za ukombozi. Sababu ni kuwa kigezo cha mfumo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu kilisimama kukabiliana na vigezo viwili vilivyokuwa vimezoeleka vya Uliberali na Usoshalisti; na kikatoa changamoto kwa misingi ya Usekulari, Umaada na Umwanadamu. Na hali hiyo ikapelekea kupungua mvuto wa idiolojia za Umaksi na Utaifa, ambazo wakati huo zilikuwa zikijulikana kama idiolojia za harakati za ukombozi za mataifa yanayopigania uhuru. Kwa hivyo kutokana na kufungua kambi ya tatu katika mfumo wa kimataifa au kutangaza njia ya tatu ya ufumbuzi katika dunia ya wapigania ukombozi, Mapinduzi ya Kiislamu yaliweza kukabiliana na mfumo wa kimataifa wenye mielekeo ya kimaada na kuanzisha utamaduni mpya kwa mataifa ya Ulimwengu wa Tatu katika uga wa harakati za kupigania kujitawala na kukabiliana na ukoloni. Lakini mbali na hayo, kubadilisha kanuni ya mchezo wa siasa katika ulingo wa kimataifa na hatimaye kuutibua mfumo wa kambi moja pekee uliokuwepo baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, na badala yake kurasimisha mfano mpya katika miamala ya kimataifa, ni taathira nyingine ya Mapinduzi ya Kiislamu katika uga wa uhusiano wa kimataifa.

Mpenzi msikilizaji, sehemu ya sita ya kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii, imefikia tamati. Usiache kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika sehemu ya saba ya mfululizo huu, ambapo tutaendelea kuzungumzia mambo yanayoyatafautisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa duniani. Nakushukuru kwa kunisikiliza na nakutakia usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags