Jan 20, 2019 01:10 UTC
  • Jumapili, Januari 20, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 13 Jamadil-Awwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 20 Januari 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele. Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo wa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali bin Abi Talib AS na Waisalmu wengine waliosabilia nafsi zao kwa ajili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na kulea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (saw) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchaji Mungu na elimu na alikuwa mfano na kigezo chema kwa Waislamu.

Siku kama ya leo miaka 1368 iliyopita, aliuawa Ibrahim Ibn Malik Ashtar, kamanda shujaa wa Kiislamu, katika vita na jeshi la Bani Umayyah. Ibrahim alikuwa mtoto wa sahaba na kamanda mkubwa wa Imam Ali Bin Abi Twalib (as). Akiwa kijana, Ibrahim alikuwa pamoja na baba yake katika vita ya Siffin akipambana na jeshi lililoongozwa na Muawiya Bin Abi Sufiyan ambapo katika vita hivyo, aliweza kuonyesha ushujaa na uhodari mkubwa wa kupambana na adui. Hata hivyo kilele cha ushujaa wake kilidhihiri katika harakati ya Mukhtar Thaqafi mjini Kufa mwaka 66 Hijiria. Katika mwamko wa harakati hiyo ya kulipiza kisasi kwa damu ya Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) na wafuasi wake waliouawa katika tukio la Karbala mwaka 61 Hijiria, Ibrahim alikuwa na nafasi muhimu ambapo baada ya ushindi, aliongoza mapambano ambayo yalipelekea kudhibitiwa mji wa Mosul, kaskazini mwa Iraq. Hata hivyo muda mfupi baadaye Mu's'ab Bin Zubair aliudhibiti mji wa Kufa na baada ya kumuua shahidi Mukhtar, alimtaka Ibrahim atoe mkono wa baia kwake. Ibrahim ambaye alikuwa akiona hatari ya utawala wa Bani Umayyah alikubali kutoa baia, hata hivyo akiwa katika vita dhidi ya jeshi la Abdul-Malikk Bin Marwan, aliuawa shahidi kufuatia uhaini wa mmoja wa makamanda wa jeshi lake.

Ibrahim Ibn Malik Ashtar.

Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, Mirza Fadhlu Ali Irwani, maarufu kwa jina la Swafa, alimu na mtaalamu mashuhuri wa fasihi wa Waislamu. Alijifunza tafsiri ya Qur'an, theolojia na hisabati. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf Iraq na kufanikiwa kukwea daraja kadhaa za kielimu na kufikia daraja ya ijtihad. Katika kipindi cha harakati ya katiba nchini Iran, Swafa alijiunga na wapigania uhuru ambapo alikamatwa na utawala wa wakati huo. Allamah Irwani mbali na kuwa msomi mkubwa, pia alikuwa hodari katika kusoma mashairi. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na 'Hadaaiqul-Aarifina', 'Kumbukumbu ya Safari yake ya Ulaya' na 'Misbaahul-Huda.'

Mirza Fadhlu Ali Irwani

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, aliaga dunia John Ruskin mwandishi, mwanafalsafa na mkosoaji mashuhuri wa Uingereza. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. Ruskin alizaliwa mwaka 1819 mjini London. Awali Ruskin alifunzwa na wazazi wake akiwa nyumbani kabla ya kujiunga na chuo cha mjini London na akiwa huko akaanza kutunga mashairi. Malenga huyo wa Uingereza alikuwa mkosoaji wa sekta ya sanaa na alibainisha mitazamo yake kuhusu sanaa katika kitabu chake alichokipa jina la "Modern Painters".

John Ruskin

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili na Nusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".

Federico Fellini.

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita yaani tarehe 30 Dei mwaka 1357 Hijria Shamsia, habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi. Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran.

Imam Khomeini (MA)

 

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khonsari, faqihi na marjaa mkubwa wa kidini. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali kwao alikozaliwa, alisafiri na kuelekea Isfahan na Najaf na kuhudhuria masomo na darsa za walimu watajika wa zama hizo. Baada ya hapo alianza kufundisha. Ayatullah Ahmad Khonsari alikuwa miongoni mwa wanazuoni waliokuwa wakimuunga mkono Imam Khomeini MA wakati wa harakati zake dhidi ya utawala wa Shah nchini Iran na alikuwa mstari wa mbele katika kusukuma mbele gurudumu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Alimu huyo ametoa wanafunzi wengi waliokuja kuondokea kuwa wasomi na wanazuoni mahiri kama Ayatullah Shahidi Murtadha Mutahhari, Imam Mussa Sadr, Sayyyid Ridha Sadr na wengineo. Ayatullah Khonsari hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi na kualifu vitabu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khonsari.

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita sawa na tarehe 30 Dei 1357 Hijria Shamsia, Mhandisi Mehdi Bazargan, Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifariki dunia. Mhandisi Bazargan alizaliwa mjini Tehran na kuhitimu masomo yake ya uhandisi wa magari huko nchini Ufaransa. Alikuwa mhadhiri pia katika Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika harakati za kisiasa wakati wa kujiri tukio la kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Muda mchache kabla ya mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Mehdi Bazargan alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na kwa pendekezo la baraza hilo alitakiwa kuunda serikali ya muda. Hata hivyo serikali yake ilidumu kwa muda wa miezi 9 tu kutokana na kuwa na tofauti za kimsingi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupenya katika serikali hiyo vibaraka waliokuwa dhidi ya Mapinduzi.  Hatimaye Bazargan aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua maradhi ya moyo.

Mhandisi Mehdi Bazargan

 

 

Tags